• Na Vincent Mpepo

    Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeendesha mafunzo ya uelewa na utambuzi wa Lugha ya Alama kwa watumishi waendeshaji wanaohusika moja kwa moja na utoaji wa huduma kwa wateja ikiwemo viziwi ili kurahisisha mawasiliano na utoaji wa huduma.

    Akifungua mafunzo hayo juzi jijini Dar es salaam, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Teknolojia za Kujifunzia na Huduma za Mikoa, Profesa Leonard Fweja alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanadhihirisha dhamira ya chuo kutoa huduma ya elimu kuwa jumuishi na kwamba taarifa ndio nguzo ya mawasiliano miongoni mwa jamii.

    “Kama tunavyofahamu katika jamii tupo watu wenye kila aina ya changamoto lakini huwa zipo namna za kupata suluhisho kwa changamoto hizo kupitia mawasiliano”, alisema Profesa Fweja.

    Alisema mawasiliano hurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma na kuwezesha akili kufanya kazi kwa ubora zaidi.

    Mkuu wa Idara ya Isimu na Taaluma za Fasihi chuoni hapo, Dkt. Zelda Elisifa aliwataka waliohudhuria kuendelea kufanyia kazi walichofundishwa ili kukuza uelewa wao katika lugha hiyo kwani bila kufanya hivyo watasahau na mafunzo hayo hayatakuwa na tija.

    Alisema chuo kimekusudia kujumuisha ukalimani wa Lugha ya Alama katika huduma na programu zote za chuo hicho kufikia Juni 2026.

    “Ili kufanikisha jambo hili idara yangu iliona umuhimu wa kuwapa kipaumbele makatibu muhtasi na wafanyakazi wa mapokezi fursa hii ya ujuzi wa msingi wa Lugha ya Alama ya Tanzania (LAT)”, alisema Dkt. Elisifa.

    Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Kurugenzi ya Huduma za Wanafunzi, Mwanawetu Mbonde alishukuru idara na Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii cha chuo hicho kwa kuandaa na kuendesha mafunzo hayo kwani yanawasaidia kupata msingi wa kuielewa Lugha ya Alama ambayo itawasaidia katika utoaji huduma na watu wa Makundi yote.

    Mbonde alishauri mafunzo hayo yaongezewe muda na ikiwezekana yafanyikie nje ya eneo la kazi ili washiriki wapate kumakinika nayo tofauti na hilo inakuwa ngumu kwani wengine wanalazimika kwenda ofisini kufanya kazi na kurudi tena kitu ambacho kinapoteza makini kwa wafanyakazi hao.

    Mtumishi wa Kurugenzi ya Maktaba ya chuo hicho, Khadija Katele alisema idadi ya washiriki kutoka kurugenzi hiyo iongezwe kwenye mafunzo wakati ujao kwa kuwa ni eneo linalohudumia watu wote ikiwemo viziwi.

    Mafunzo hayo ya siku mbili yalikuwa na malengo mahususi matatu ambayo ni kuongeza ufahamu na uelewa kwa washiriki kuhusu uziwi, Lugha ya Alama na mahitaji ya msingi ya mawasiliano ya jamii ya viziwi.

    Malengo mengine ni pamaja na kuwawezesha washiriki kuwa na mbinu za msingi za mawasliano ya kila siku na viziwi ili kuondoa vizuizi vya mawasiliano na viziwi katika jamii ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na kuwapa washiriki mikakati ya kutengeneza mazingira wezeshi kwa mawasiliano jumuishi.

  • Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas More Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es salaam, Padre Aidan Mubezi na watoto waliopata sakramenti ya Kipaimara Siku ya Jumamosi jijini Dar es salaam mara baada ya adhimisho la misa takatifu ya kipaimara Parikiani hapo, (Picha na Francis Mpepo).

    Na Vincent Mpepo

    Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo amesema umaskini na utajiri kiroho unahusisha namna ambavyo mkristo ana uhusiano na Mungu na kwamba umaskini wa mali siyo siyo tatizo hapa duniani.

    Mwadhama Kadinali Pengo alieleza hayo juzi wakati wa adhimisho la misa takatifu ya kipaimara katika Parokia ya Mt. Thomas More -Mbezi Beach Jimbo Kuu la Dar es salaam ambapo vijana 22 walipokea sakramenti ya Kipaimara,

    Alisema kipaimara ni kumbukumbu halisi ya siku ya Pentekoste ambapo mitume walijazwa Roho Mtakatifu na kuata nguvu ya kueneza injili na kwamba baada ya kupakwa mafuta kwa wanakipaimara hao 22 wanapaswa kufanya kazi ileile ya kupeleka injili duniani.

    “Kwa sakramenti ya Kipaimara mnajazwa Roho Mtakatifu na kupewa majukumu ya kuhubiri habari njema kwa maskini kama alivyofanya Kristo mwenyewe” alisema Mwadhama Pengo.

    Alisema leo hii ukienda kuwahubiri maskini habari njema watadhani ni mradi au utawapa fedha kitu ambacho si sahihi.

    Akirejelea maneno ya Mtakatifu Agustino, Mwadhmama Pengo alisema wakristo wengi wa sasa hudhani kuwa wao si maskini kwa kuwa wana pesa, chakula na mahali pa kuishi na kusisitiza kuwa umaskini unaotajwa kiiroho ni hali ya mwanadamu kutokuwa na mahusiano na Mungu.

    “Huenda sisi ni maskini zaidi ya wanaolala nje kwa kukosa mahali pa kulala, chakula na mahitaji mengine”, alisema Kadinali Pengo.

    Alisema matajiri wanaweza kutoa sadaka au vitu ghali likini wanasahau neno la Mungu na kwamba utajiri wa kweli ni ule wenye uhusiano na Mungu.

    “Umaskini halisi ni ule wa kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu”, alisema Kadinali Pengo.

    Aidha, Kadinali Pengo alielezea masikitiko yake kutokana na wanadoa kuachana baada ya miaka mingi ya kuishi pamoja na kusema kuwa si jambo jema na kwamba ni kinyume na mpango wa Mungu.

    Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas More Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es salaam, Padre Aidan Mubezi alisema nia za ibada siku hiyo kuwa ni adhimisho la misa takatifu ya kipaimara na pongezi kwa Kadinali Pengo kwa kutimiza miaka 54 ya upadre.

    Alisema Kadinali Pengo alifika Parokiani hapo Mwaka 2015 kwa Kipaimara cha kwanza na juzi alifika kwa Kipaimara cha kumi.

    Alitumia fursa hiyo kumpngeza kwa kutimiza miaka 54 ya upadre na kuongoza waumini katika utoaji wa salamu za pongezi kwake.

    Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo akimpaka mafuta mmoja wa watoto Daniela Francis wakati wa adhimisho la misa takatifu ya kipaimara Parokiani hapo, nyuma yake ni msimamizi wake (Picha na Francis Mpepo).

    Mmoja wa watoto akipokea sakramenti ya ekaristi takatifu kutoka kwa Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo wakati wa adhimisho la misa takatifu ya kipaimara Parokiani hapo, nyuma yake ni msimamizi wake (Picha na Francis Mpepo).

  • Na Mwandishi Wetu

    Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watafiti na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini mahitaji halisi ya huduma za afya nchini.

    Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kongamano la 13 la kisayansi la chuo hicho lililofanyika kwa siku mbili juzi na katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.

    Alisema mapendekezo hayo yawasilishwe serikalini na kuzitaka Wizara za Afya, Elimu na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kushirikiana na MUHAS kupanga namna bora ya kuboresha mitaala ambayo itakayosaidia kuzalisha wataalam mahiri kwenye tafiti za dawa, chanjo na vifaa tiba.

    Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na uboreshaji wa huduma za afya, ambapo kupitia MUHAS wataalam na watafiti wengi wamezalishwa na wanalisaidia taifa.

    Alisema kuna umuhimu wa sekta za umma na binafsi kujadiliana kwa kina na kupitia machapisho ili kuishauri serikali namna ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika vita dhidi ya magonjwa na imani imani potofu.

    Alisema wakati tunajivunia upatikanaji wa huduma bora za afya nchini, mageuzi ya viwanda yanayochangiwa na ukuaji wa teknolojia yameleta chachu ya kuimarisha mifumo na ubora wa sekta za afya kote duniani suala linalotia moyo.

    “Tunafarijika kuona taasisi zetu za vyuo vikuu na zinazotoa huduma  zinajitahidi kwenda  kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia  ikiwa ni pamoja na utumiaji wa akili bandia,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

    Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, alisema Chuo hicho kimeendelea kuwa kinara wa mabadiliko katika elimu ya afya, si tu kwa kutoa mafunzo bora, bali pia kwa kuchangia katika kufanya maamuzi ya kisekta yanayozingatia ushahidi.

    Alisema wanatambua na kuthamini mchango wa Chuo hicho katika kuanzisha na kuendeleza majukwaa hayo ya kisayansi ambayo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha mawasiliano kati ya wanasayansi na watunga sera hivyo kuendeleza maendeleo yenye msingi wa kisayansi.

    Alieleza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia   inahakikisha maeneo ya kujifunzia kwa vitendo yanapatikana ili kuongeza tija ya miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na shughuli mbali mbali zinazofanywa na chuo hicho.

    “Uwekezaji wa teknolojia katika matumizi ya Tehama umesaidia kuleta mageuzi kwenye sekta ya afya na kurahisisha utoaji wa huduma na MUHAS imekuwa kinara kwenye matumizi hayo na upatikanaji wa matokeo chanya,” alisema Prof. Mushi.

    Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema kongamano hilo liliwaleta pamoja watafiti na wadau ili kujadili na kutoa mapendekezo   kwa kutumia bango kitita ili Wizara ya Afya ione fursa za namna inavyoweza kutumia teknolojia katika utoaji wa huduma na mafunzo katika sekta ya afya ili kuimarisha afya za wananchi.

    Kwa upande wake, Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Bruno Sogoye, alisema kongamano hilo lilihudhuriwa na watafiti na wataalamu zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya nchi.

    watafiti hao waliwasilisha tafiti zao kwenye maeneo nane ambavyo ni magonjwa yasiyoambukiza, afya ya mama na mtoto, ubunifu katika kuboresha maisha ya wananchi, magonjwa yanayoambukiza kama vile malaria na Ukimwi, mifumo ya afya pamoja na lishe.

    Kwa mujibu wa Profesa Sogoye kongamano hilo lilihusisha watafiti kutoka nchi za Marekani, Norway, Kenya na wenyeji Tanzania.

  • Na Vincent Mpepo

    Imeelezwa kuwa matatizo mengi wayapatayo wakristo katika jamii muda mwingine ni kutokana na kiburi au kupuuzia sauti ya Roho Mtakatifu ndani yao wanapofanya maamuzi katika masuala mbalimbali.

    Hayo yameelezwa jana na Mwinjilisti, Thomas Mwakatobe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Buguruni wakati akihuburi katika ibada ya Siku ya Bwana ya Utatu Mtaa wa Kwembe na kusisitiza kuwa athari za kupuuza sauti ya Roho Mtakatifu ni kubwa kwani mara nyingi huwa ni majuto.

    Alisema kwa mkristo aliyemkiri Bwana kuwa Mwokozi wa maisha yake kuna namna ambayo Roho Mtakatifu hufanya kazi ndani yake ikiwemo kumkumbusha, kumshauri na wakati mwingine kumpa tahadhari za mambo anayokusudia kuyafanya na ikiwa atatii ni wazi kuwa atafanya maamuzi sahihi.

    “Roho Mtakatifu ni ukamilifu wa Mungu Mwenyewe na kuna nguvu ambayo huiachilia kwetu ikiwa tutatembea katika kusudi la Bwana”, alisema Mwinjilisti Mwakatobe.

    Alisema Roho Mtakatifu yupo kwa ajili ya kuwakumbusha, kuwapa nguvu na kuwafundisha na kwamba hawawezi kutenda kazi ya Mungu pasipo nguvu za Roho Mtakatifu ndani yao.

    “Mara ngapi Roho Mtakatifu amekusemesha kwa namna mbalimbali hata kupitia ndoto na ulifanya nini kutii au kupuuza sauti hiyo?, aliuliza Mwinjilisti Mwakatobe

    Alisema miujiza inayotendeka ni kutokana na nguvu za Roho Mtakatifu na kwamba mtu yeyote asijaribu kumwekea mikono mtu mwingine ikiwa hana nguvu ya Roho Mtakatifu kwani atapata shida.

    Aidha aliwataka washarika kumakinika na ibada wakiwa kanisani badala ya kuwepo tu kama picha huku mawazo yao yapo nje ya ibada.

    Kwa upande mwingine aliwaasa vijana wa vikundi vya kusifu na kuabudu kutengeneza kwanza mambo yao kabla ya kwenda mbele za Mungu na kwamba makosa yao yanaweza kusababisha uwepo wa Mungu kutojidhihirisha katika ibada.

    MwinjilistI Kiongozi wa Mtaa wa Kwembe, Emeline Mnzava aliwakumbusha wazazi kuendelea kuwahimiza watoto kujisomea kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya kupima ufahamu ambayo itafanyika kwa watoto wa mwaka wa kwanza.

    Mwinjilsti Mnzava aliwashukuru washarika kwa kuendelea kumtolea Mungu kupitia sadaka mbalimbali ikiwemo ile ya ujenzi wa kituo cha watoto wennye mahitaji Maalumu Kitopeni Bagamoyo na kuwa kazi hiyo si ya bure na kwamba hakuna aliyewahi kumtolea Mungu akaachwa.

    “Pamoja na kuwa tumeshatoa bado tunaalikwa kuendelea kumtolea Mungu hata kwa kuanzia kwa cha kiwango cha shilingi 1,000 kwani bado rasilimali fedha inahitajika”, alisema Mwinjilisti Mnzava

    Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi Mtaani hapo, Exaud Mchome aliwajulisha washarika kuwa kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na aliwakumbusha waliohaidi katika awamu ya kwanza ya utoaji ya Januari-Juni 2025 kukamilisha ahadi zao hadi kufikia mwishoni mwa Mwezi Juni kupisha awamu ya pili na mavuno.

    “Pesa zilizopatikana zimefanya kazi na kila mmoja anaweza kujionea kwa kutembelea eneo la ujenzi”, alisema Mzee Mchome.

    Alisema kipaumbele cha kwanza kwa sasa katika Mtaa wa Kwembe ni ujenzi.            

    Mjumbe wa Kamati ya Malezi mtaani hapo, Chiristina Bukuku aliwakumbusha wazazi na walezi kuhusu maandalizi ya vijana watakaoshiriki katika Tamasha la Twen’zetu Kwa Yesu kuwahi siku ya Jumamosi kwa ajili ya usafiri wa pamoja ulioandaliwa.

    “Mnapaswa kufika hapa kanisani saa 12 kasoro atakayechelewa na akiachwa atalazimika kusafiri mwenyewe”, alisisitiza Bukuku.

  • Na Mwandishi Wetu

    Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) anayesimamia Uhimilivu wa Kifedha na Uendeshaji wa Sekta ya Fedha, Sauda Msemo amesema sekta ya fedha nchini inapaswa kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani ili kulinda usalama wa kiuchumi na kuchochea maendeleo.

    Msemo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano lililohusisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka katika taasisi zinazohusika na mnyororo wa fedha na teknolojia.

    “Teknolojia inakua kwa kasi sana, taifa haliwezi kubaki nyuma, hatuwezi kuwa salama  kama hatutakuwa sehemu ya ukuaji huo na ni  lazima tushirikiane kukuza teknolojia yetu kwa kuzingatia vigezo vya usalama na uendelevu,” alisema Msemo.

    Alisema katika juhudi za kuimarisha usimamizi wa bidhaa mpya za teknolojia ya kifedha, Benki Kuu ya Tanzania imeanzisha mazingira maalumu ya majaribio (sandbox), ambayo yanalenga kuwapa wabunifu fursa ya kujaribu bidhaa zao kabla ya kuziingiza rasmi sokoni.

    “Hatutaki bunifu ziingie sokoni zikiwa hazijajaribiwa kisha zikaleta madhara bali tunataka ziwe katika mazingira salama kwa kujaribiwa, zikidhi vigezo, ndipo zihidhinishwe kwa ajili ya matumizi ya umma,” aliongeza Msemo.

    Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Impact Advisory, Angel Mbogoro, alisema kampuni yao imekuwa mstari wa mbele kusaidia taasisi na watu binafsi kujenga uwezo katika maeneo ya uongozi, teknolojia na uendelevu.

    “Tumeona kuna pengo la utaalamu nchini ndiyo maana tumeanzisha programu za kuwajengea watu uwezo wa kuongoza taasisi, kutumia teknolojia na kuongeza ujasiri wao katika uwajibikaji ili kuchochea kasi ya maendeleo,” alisema Mbogoro.

    Aidha, alibainisha changamoto ya viongozi kutotoa ushirikiano kwa wafanyakazi wao na pindi wanapoondoka ofisini hivyo kuacha pengo kubwa kwa kampuni kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi wakati wapo wenye uwezo lakini hawakuibuliwa.

    Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na sanaa, uongozi kwa wasichana na mabadiliko ya tabia nchi, Small Hands Big Change, Akoth Okeyo, alisema teknolojia ina mchango mkubwa kwa vizazi vijavyo ikiwa watapatiwa elimu sahihi mapema.

    Alisema watoto wanapaswa kufundishwa matumizi Chanya teknolojia ili kuwasaidia wasichana kupata taarifa kupitia akili unde (AI) kwa ajili ya miradi ya tabia nchi na kwamba anaamini teknolojia ni njia sahihi ya kuleta mabadiliko katika jamii.

    Kongamano hilo liliibua hoja nyingi kuhusu umuhimu wa kushirikiana kati ya sekta ya umma na binafsi katika kukuza teknolojia bunifu zenye kuzingatia maslahi ya taifa, wadau walisisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja ndiyo njia pekee ya kusukuma mbele ajenda ya maendeleo jumuishi na endelevu.