Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) zimesaini mkataba ili kutekeleza Mradi wa Uhifadhi wa Maeneo Oevu na Baioanuwai ya Kidakio cha Katuma, Mpanda.
Mradi wa IKI Katuma utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kwa gharama ya kiasi cha Euro 4,000,000.00 zitakazotolewa na Serikali ya Ujerumani.
Lengo la mradi IKI Katuma ni kuzijengea uwezo taasisi mtambuka za Sekta ya Maji katika kuimarisha ushirikiano na kubadilishana maarifa ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji ili kuhakikisha huduma za mifumo ya ikolojia zinatumika kwa maendeleo endelevu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika Kipindi cha miaka minne ya serikali imefanikiwa kupunguza mrundikano wa wafungwa na mahabusu kwenye magereza hapa nchini ambapo amesema magereza hapa nchini zina uwezo wa kuchukua wafungwa na mahabusu 28,000 nchi nzima.
Waziri Dkt. Ndumbaro ametoa taarifa hiyo leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara yake katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita Jijini Dodoma.
Alisema kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) jumla ya halmashauri 180, kata 1,907 na vijiji/mitaa 5,702 zilifikiwa na jumla ya wananchi milioni 2,698,908 walifikiwa na kupata elimu na huduma za kisheria kupitia mikutano ya ana kwa ana.
Lalisema Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekamilisha uhakiki wa mwisho wa Sheria Kuu 300 kati ya 446 zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Hii ni sehemu ya jitahada za serikali katika kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria na kuimarisha misingi ya utoaji haki” alisema Dkt. Ndumbaro.
Alisema mashauri yenye umri mrefu mahakamani ni 2,780 sawa na asilimia 4 ya mashauri yote yaliyobaki mahakamani hivyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zenye mrundikano mdogo wa mashauri mahakamani.
Sanjari na hayo, Waziri Dkt. Ndumbaro amesema mahakama inafanya utaratibu wa kutumia mfumo wa kutafsiri katika mahakama zote zenye miundombinu ya mtandao (intaneti) nchini ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na gharama nafuu.
Wanataaluma na watafiti katika taasisi za elimu ya juu barani Afrika wametakiwa kufanya tafiti zitakazotoa majawabu ya matumizi endelevu ya rasilimali za bahari barani humo ili kutekeleza dhana ya uchumi wa bluu kwa vitendo na tija katika kuchochea uchumi na maendeleo ya Afrika.
Wito huo umetolewa na washiriki katika mjadala wa kitaaluma uliofanyika leo katika ukumbi wa Hotel ya Johari Rotana, jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wasomi, wanataaluma viongozi wa serikali, taasisi binafsi na wanadiplomasia wa ndani na nje ya Afrika.
Akizungumza wakati akichangia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mjadala huo, Rais Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA), Dr. Thabo Mbeki alisema bado kuna changamoto ya kueleweka kwa dhana ya uchumi wa bluu kivitendo.
“Asilimia kubwa ya watu wetu bado hawana maarifa sahihi kuhusu uchumi wa bluu na kwamba hatuna budi kuwaelimisha ili uchumi wa bluu ufahamike”, alsiema Rais Mstaafu Mbeki.
Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt.Dunlop Ochieng alisema kutokana na mjadala huo mojawapo ya vitu vya msingi ambavyo utekelezaji wa aina yoyote ya maendeleo unapaswa kuzingatia ni kuwaangalia wananchi wa kawaida watafaidikaje.
“Tunawekaje mazingira ya usalama wao kwani tumeona mara kadhaa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi ikiwemo uwekezaji wananchi wamekuwa ni walaji wa mabaki na vinono vikisafirishwa kwenda nje”, alisema Dkt.Ochieng.
Alisema tunafamu umuhimu wa Mto Nille kwa nchi ya Misri na kwamba dhana ya uchumi wa bluu wakati mwingine ni msamiati tu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku alisema Afrika inahitaji vinara watakaofanya kazi mstari wa mbele ili kuhakikisha malengo ya kujikomboa kifikra na kujiamini yanatimia.
“OAU imesaidia nchi za Afrika kupata Uhuru wake lakini kwa sasa AU na Afrika ya sasa ni kulikomboa Bara hilo katika nyanya zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii”, alisema Butiku.
Aidha alimshukuru Rais Thabo Mbeki kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mjadala huo uliosaidia kufanya tathimini ya thamani ya uchumi wa bluu katika bara la Afrika na kuanisha mikakati ya kutumia rasilimali za bahari kujikomboa kiuchumi.
Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa masuala ya rasilimali za bahari, Dkt. Narriman Jiddawi alielezea mabadiliko ya kiutamaduni na kifikra yanayoonesha kukua kwa ushiriki wa wanawake wa Zanzibar kwenye uchumi wa bluu na kwamba wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato zinazoambatana na rasilimali za bahari.
Madereva wa magari ya serikali mkaoni Dodoma wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya usalama barabarani wanapokuwa wakiendesha magari hayo.
Rai hiyo imetolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Katabazi wakati akizungumza na madereva hao kwenye kikao maalumu alichokiitisha katika ukumbi wa Polisi jamii Jijini Dodoma kilicholenga kuzungumza nao juu ya utii wa sheria za usalama barabarani kwani baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa kukiuka sheria hizo.
“Kikubwa ni kuwataka madereva wa serikali kuzingatia sheria na taratibu zinazohusiana na usalama barabarani”, alisema Kamanda Katabazi.
Alisema Jeshi lake limekusudia kuwakumbusha na kuwaelimisha kuhussu sheria hizo, taratibu na kanuni lakini pia kuwaonya baadhi yao ambao hawazingatii sheria hizo kwa makusudi hivyo kuhatarisha usalama wao na wengine.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali, Issa Kisebengo alisema elimu waliyoipata kwenye kikao hicho imewasaidia kutambua majukumu na wajibu wao kwenye utumishi wa umma na kutoa wito kwa madereva wenzake kuzingatia yale yote waliyofundishwa.
“Sisi ni vioo kwa madereva wengine lakini pia tunabeba watumishi wa serikali na kuna watumiaji wengine wa barabara na wote hao wanatutegemea sisi kwa usalama wao hivyo, mafunzo tuliyoyapata tutaenda kuyafanyia kazi”, alisema Kisebengo.
Sanjali na kukumbushwa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani kikao hicho pia kiliambatana na mafunzo mbalimbali yaliyotolewa kwa madereva hao ili kuendelea kuwakumbusha sharia hizo kwani kuwa madereva wa magari ya serikali si kigezo cha kuvunja sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Mwatumai Mwanjota amewataka wanaume kutokwepa wajibu kwa familia zao katika masuala mbalimbali ya kiimani ikiwemo kuhudhuria na waume zao kwenye huduma na sakramenti muhimu.
Hayo ameyasema leo baada ya ubatizo wa watoto katika Mtaa wa Kwembe na kwamba anakerwa na baadhi ya wanaume kuwaacha wake zao kwenda ibadani kwa ajili ya ubatizo wa watoto wao huku akihoji umuhimu wa shughuli walizoenda kufanya ambazo ni zaidi ya tukio kama ubatizo.
“Ubatizo ni kitu chenye thamani sana na alihoji kwa nini wapange safari siku ya ubatizo?”, alihoji Mchungaji Dkt. Mwanjota.
Alisema ikiwa kuna matatizo ya kuumwa mpaka kulazwa walao hapo wataeleweka vinginevyo wanakwepa wajibu wao kama wazazi na viongozi wa familia.
Aidha aliwataka akina mama hao wakaombe msamaha na kutengeneza na waume zao ikiwa kuna hitilafu ili mambo yawe mazuri kwa wakati ujao.
Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava akihubiri kwa kutumia maandiko kutoka kitabu Zaburi alisema ni kitabu chenye hazina kubwa ndani yake kwa kuwa unaweza kutunga nyimbo ukaimba, ukasifu na kushangilia ukuu wa Mungu.
Alisema kila kiumbe hakina budi kumsifu Mungu kwa kuwa ndiye aliyekipa uhai na uwepo wake hapa duniani.
“Kila kiumbe kina namna ya kumshukuru Mungu kwa ajili ya uumbaji wake ndio maana vitu kama Jua na Mwezi vinamsifu Mungu”, alisema Mwinjilisti Mzava.
Alisema mwadamu anapaswa kuimba wimbo mpya kila siku kwa kuwa ndiye aliyempa uhai na kwamba kuimba ni sehemu ya kushukuru na moyo unaoweza kushukuru ni ule uliojaa shukrani.
“Kama unaweza kumsifu mwanadamu ikiwa amekufanyia jambo fulani jema, je Mungu si zaidi ya mwanadamu?”, alisema Mwinjilisti Mzava.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ujenzi Mtaani hapo, Exaud Mchome akitoa mwendelezo wa kazi ya ujenzi wa kanisa alisema kazi ya uwekaji bati inaendelea licha ya kusimama kutokana na hali ya hewa.
Aliwakumbusha washarika kuendelea kumtolea Mungu ili kufikia malengo kwa awamu ya kwanza ya January hadi Juni kwa kiasi walichokubaliana.
“Roho ya kupenda ikusukume ufanye jambo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Bwana”, alisema Mchome.
Ibada ya leo siku ya nne baada ya Pasaka kiliturujua ni maalumu kwa ajili ya uimbaji ikitambulika kwa jina na la ‘Domino Kantate’ na mtaani Kwembe ilipamwa na kwaya mbalimbali za mtaani hapo lakini pia uwepo wa Kwaya Kuu ya Umoja kutoka Mtaa wa Malamba Mawili ulinogesha na kufanya iwe siku ya Baraka tele.
Kwaya Kuu ya Umoja kutoka Mtaa wa Malamba Mawili ikihudumu katika ibada ya Leo, Siku ya nne baada Pasaka katika Mtaa wa Kwembe.
Sanjali na hilo huduma mbalimbali za kichungaji ikiwemo ubatizo, meza ya bwana na kuweka wakfu kwa vifaa vilivyoletwa kanisani kwa ajili ya kazi ya Mungu zilifanyika.
Umoja wa Wanawake Wanaofanya kazi Sekta ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) wametembelea Bandari ya Tanga na kuridhishwa na utendaji kazi katika bandari hiyo baada ya kukamilika kwa mradi wa maboresho ya bandari.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Umoja huo Mhandisi Fortunata Makoye Kakwaya alisema maboresho hayo yameleta mapinduzi makubwa katika bandari hiyo ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo meli kubwa zilikuwa haziwezi kufunga gatini kutokana na changamoto ya kina cha maji kuwa kifupi.
“Kama wadau katika sekta ya bahari tunapongeza kwa maboresho haya kwa kuwa yameleta mapinduzi makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuifanya bandari hii ikidhi viwango vya kimataifa katika kuhudumia meli na mizigo”, alisema Mhandisi Kakwaya.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari, Afisa Mkuu anayeshughulikia utekelezaji Gwakisa Mwaibuji aliwataka wadau hao kuwa mabalozi wazuri wa Bandari ya Tanga ili bandari hiyo iendelee kupokea shehena kubwa zaidi na mapato makubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase.
Na Gabriel Msumeno, Pwani
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salim Morcase amekutana na wamiliki wa viwanda wa Mkoa huo ili kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili na kujadiliana nao namna bora za kuzitatua ili wafanye shughuli zao za uwekezaji vyema.
Mkutano huo ulifanyika leo kwenye ukumbi wa Polisi Kibaha mjini ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano na makundi mbalimbali katika jamii na mwendelezo wa vikao na wafugaji, wafanyabiashara, waganga wa tiba asili, watu wenye ulemavu, maafisa usafirishaji, wawekezaji na wajasiriamali.
Alisema jeshi hilo linaendeleza falsafa ya Polisi Jamii kwa kukutana na watu wa makundi mbalimbali ili kuendelea kuimarisha mahusiano mema yatakayosaidia katika ulinzi na usalama kwa kuondoa matukio ya uhalifu.
Wamiliki wa viwanda walielezea changamoto zao za kiusalama, ikiwemo maeneo ya viwanda kuzungukwa na mapori, ubovu wa miundombinu ya barabara, na ukosefu wa vituo vya Polisi vya karibu, hali inayochangia kuongezeka kwa uhalifu hususani nyakati za jioni na usiku.
Baadhi ya wawakilishi viwanda mbalimbali Mkoani Pwani
Mwakilishi wa Wamiliki wa Viwanda Mkoa wa Pwani, Habibu Juma Issa kutoka kiwanda cha Bagamoyo Sugar alilishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kufanya mkutano nao kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya uwekezaji na kusaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji.
“Hii ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza kipato, kuboresha doria na ulinzi maeneo ya viwanda ili tuweze kufanya kazi saa 24 kwa kupokezana usiku na mchana pasipo hofu ya kufanyiwa uhalifu na vibaka”, alisema Habibu.
Aidha, wamilki hao wa viwanda waliomba Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa wawekezaji wageni kuhusu sheria na maadili ya kitanzania katika kazi ili kuepusha udhalilishaji na ukatili mahali pa kazi.
Akijibu baadhi ya hoja za washiriki katika mkutano huo, Kamanda Morcase alisisitiza kuwa kikao hicho ni fursa muhimu kwa Jeshi la Polisi kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhu kwa pamoja na kuhaidi kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto zinazowezekana kutatuliwa mara moja.
Kwa changamaoto zilizopo ndani ya uwezo wetu tutazishughulikia lakini ambazo zitahitaji kushirikiana na na idara tutafanyia kazi baada ya kushirikisha mamlaka husika, alisema Kamanda Morcase.
Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mkoa ya uwekezaji wenye takribani jumla ya viwanda 1,533 ambapo 33 kati yake ni viwanda vikubwa.