• Viziwi Hupenda Kuitwa Hivyo Badala ya Wasiosikia

    Na Vincent Mpepo        

    Imebainika kuwa jamii ya viziwi wanapenda kuitwa viziwi badala ya kuitwa wasiosikia au namna nyingine kwa kuwa majina mengine kuwarejelea wao huwa na maana zenye ukakasi na wakati mwingine kuwa na maana mbaya kitu ambacho si sawa.

    Hayo yamebanishwa na Mkufunzi wa Chuo Cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Malise Swila wakati wa mafunzo ya Siku moja ya Lugha ya Alama yaliyofanyika Leo jijini Dar es salaam na kuhusisha wahadhiri, watumishi waendehaji na mafundi, wakufunzi, viziwi na jamii ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

    Malisa alisema kimsingi viziwi hawapendi kuitwa majina mengine kwa kuwa majina hayo hayana uhalisia na wakati mwingine yanabeba tafsiri mbaya kuelezea hali hiyo na kuishauri jamii kuwaita viziwi kwa kuwa ni jina wanalolipenda.

    “Kwa mfano mkituita wasiosikia au bubu mnatukosea na ina tafsiri tofauti na tulivyo”, alisema Malise

    Mkalimani wa Lugha ya Alama ambaye ni mtumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Janet Phillip alisema madhumuni ya semina hiyo kujaribu kupunguza vizingiti vya kimawasiliano kati ya viziwi na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki.

    “Semina hii ni muhimu kwa kuwa kuna kundi la watu ambao tunawaacha nyuma kwa sababu ya lugha ili kurahisha utoaji wa huduma”, alisema Janet

    Alisema jamii ya viziwi wana changamoto mbalimbali na wakati mwingine inawawia vigumu kuwasilisha changaoto hizo kutokana na watumishi kutoelewa lugha ya alama hivyo imekuwa muhimu ili walao kupata maarifa ya awali ya namna ya kuwasiliana kati ya viziwi na watumishi.

    Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Mtaalamu wa Isimu na Lugha ya alama, Julius Taji alisema ni muhimu kwa jamii kuifunza namna mbalimbali za mawasiliano ili kurahisisha mawasiliano na viziwi katika jamii zetu ikiwa lugha ya alama itashindikana.

    “Tunapaswa kujua mwasiliano ya jumla yanayojumuisha mbinu zozote zitazakosaidia kiziwi kuelewa na kupata ujumbe ili apate mahitaji yake”, alisema Dkt.Taji

    Akifunga semina hiyo kwa niaba ya Mtiva wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Dkt.Halima Kilungu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Jiografia, Utalii na Ukarimu alisema semina hiyo ni muhimu sana kwa kuwa waliohudhuria wamepata maarifa tofauti na walivyokuja.

    “Nimegundua kuwa uwepo wa taa katika majengo yetu iwe kwenye huduma au majumbani ni muhimu kwa kuwa ni mwanzo mzuri wa kurahisha mawasiliano na viziwi”, alisema Dkt.Kilungu

    Alisema katika sekta ya utalii na ukarimu kuna changamoto za kimawasiliano kwa watalii viziwi kutokana na waongoza watalii kutokufahamu lugha ya alama na anadhani ni eneo linaloweza kufanyiwa kazi ili kuendelea kuwavutia watalii kutemebelea vivutio vya utalii hata kama ni viziwi.

  • Na Thomas Okello

    Fuatilia habari picha za matukio mbalimbali ya Maonesho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yaliyofanyika Mkoani Singida Aprili 28, 2025.

    Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete akizungumza katika hafla ya Maadhimisho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi katika viwanja vya Mandewa Mkoani Singida _ Aprili 28, 2025.

    Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Zuhura Yunus (kulia) akipata maelezo kuhusu majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutoka kwa Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Eliamini Mkenga alipotembelea banda la Mamlaka katika Maonesho ya Kitaifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi yanayoendelea katika vīwanja vya Mandewa Mkoani Singida kuanzia Aprili 24 hadi Aprili 30, 2025.

    Baadhi ya wageni walioshiriki Maonesho ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi katika hafla ya Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mandewa Mkoani Singida Aprili 28, 2025.

    Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Eliamini Mkenga (kati kati picha ya juu) na Saile Kurata (picha ya chini kushoto) wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya Vinasaba vya Binadamu.

    Wachezaji wa timu уа Afya wakifanya mazoezi mepesi kabla уа kuanza mchezo na timu ya Wizara ya Mambo ya Nje katika hatua ya robo fainali katika viwanja vya Aintel mkoani Singida Aprili 26, 2025. Kulia ni mtumishi wa Mamlaka Jackson Mwijage. Mambo ya Nje ilishinda kwa mikwaju ya penati.

  • Na Annamaria John

    Serikali itaendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuwa na mfumo madhubiti wa kusimamia miradi ya maji hususani katika maeneo ya vijijini kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

    Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Alex Tarimo wakati wa kikao kazi kati ya wizara yake na taasisi ya kidini ya Kanisa la Anglikana jijini Dodoma walipokwa wakijadili mfumo wa utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa na Taasisi hiyo katika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara.

    “Mfumo huu wa kushirikisha wadau ni pamoja na kutimiza azma ya serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 85 vijijini na 95 mjini “, alisema Tarimo.

    Aidha alisema lengo la kikao hicho ni kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika kufikisha huduma endelevu ya maji bila kikwazo kwa wananchi.

    Kiongozi wa taasisi hiyo Padre.Godfrey Monjera amesema pamoja na jitihada wanazofanya kufanikisha miradi hiyo bado uhitaji wa huduma ya maji upo.

    “Sisi kama taasisi ya kidini tumekuwa tukishughulika na miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya maji,lakini bila kushirikiana na serikali tusingeona matokeo mazuri” alisema Padre Monjera.

  • Na Sylvester Richard

    Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego ametembelea Kaburi la Shujaa Liti ambaye ni Malkia wa kabila la wanyuturu kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani.

    Dendego amefanya ziara hiyo Aprili 27, 2025 akiambatana na viongozi mbalimbali vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Zimamoto na Uokoaji.

    Akiwa kaburini hapo amewahamasisha wananchi wa Mkoa huo na wageni wanaofika kusherehekea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) kutemebelea kwenye kaburi la Shujaa huyo Mwanamke lililopo katika Kijiji cha Makuyu Singida

    “Mnakaribishwa kutemebelea maeneo mengine ya kihistoria yakiwemo makazi ya Mtemi Senge na Ziwa Kinda maeneo ambayo yanapatikana Manispaa ya Singida”, alisema Dendego.

    Alitumia fursa hiyo kuwaelekeza wananchi kumuenzi Shujaa Liti kwa kushiriki uchaguzi Mkuu 2025 na kuchagua viongozi bora huku pia akihaidi kujenga Chuo cha Nyuki kando ya Kaburi la Liti kwakuwa Malkia huyo alipambana na wakoloni wa Kijerumani kwa kutumia nyuki.

    Shujaa Liti alizaliwa mwaka 1860 na kufariki mwaka 1907 baada ya kukatwa kichwa na wakoloni wa Kijerumani ambao waliondoka na kichwa hicho hadi sasa ambapo Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kufuatilia kichwa hicho kirejeshwe kama kama kilivyorejeshwa cha Shujaa Mkwawa.

  • Na Annamaria John

    Imeelezwa kuwa mafunzo elekezi ni muhimu kwa wafanyakazi wapya ili kuwajengea uwezo kutambua misingi ya kazi, sheria, kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa umma.

    Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu Bi. Christina Akyoo jijini Ddodoma wakati akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na kusisitiza kuwa mafunzo hayo ya awali ni utekekezaji wa matakwa ya sheria kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma.

    “Kanuni hizo zitawawezesha waajiriwa wapya kutambua misingi ya utoaji wa huduma bora kwa wateja elimu kuhusu rushwa na madhara yake mahala pakazi na utunzaji wa siri”, alisema Bi. Akyoo.

    Alisema mafunzo yanasisitiza kufanya kazi kwa upendo, ushirikiano na umoja kipindi chote cha utumishi wa umma ikiwemo kufikia azma ya serikali ya kutoa huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 95 mIjini na 85 vijijini.

    Kada zilizoshiriki mafunzo hayo ya siku tatu ni pamoja na waendesha ofisi, wahandisi, madereva, na wataalamu wa ubora wa maji ikijumuisha watumishi 60 na yaliratibiwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma.

  • Na Vincent Mpepo

    Wanandoa wamekumbushwa kuendelea kuwa pamoja ili kuwa na umoja na mshikamano ambao ni afya kwa ustawi wa ndoa na familia kwa ujumla.

    Kauli hiyo imetolewa leo katika ibada ya Siku ya kwanza baada ya Pasaka na Mtendakazi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe, Anna Mauki wakati akihubiri kanisani hapo huku akisisitiza kuwa wapo wanandoa ambao hawana mazoea ya kuambatana pamoja kitu ambacho si chema.

    Alisema ni ajabu kuwa wapo wanandoa ambao waliwahi kutembea pamoja siku ile ya ndoa yao na baada ya hapo wamekuwa wakitembea tofauti kitu ambacho bado hakimpi Mungu utukufu.

    “Mnaweza kutoka na mwenza wako hata kwa gharama ndogo ili mpate muda wa pamoja”, alisema Mauki.

    Alisema kwa wakristo ndoa ni agano la kudumu na kwamba katika matembezi au safari hiyo ya ndoa ni muhimu kuwa pamoja kwa kuwa ni dawa na huwasaidia kujadili mambo yanayowahusu kwa ustawi wa maendeleo yao.

    Alisema matembezi ya pamoja yaanzie kwenye familia kwa kuwa wazazi na watoto wanaweza kwa pamoja wanaweza kuwa na mazungumzo ambayo ndiyo msingi katika malezi.

    Aliwakumbusha wakristo waumuhimu wa kuwalea watoto katika maadili ya kikristo kwa kuwa ndio malezi bora kwa kuwa watakua wakimjua Mungu na kuwa wanajamii wema tofauti na hapo ni changamoto.

    “Tuwasaidie watoto watembee katika Jina la Yesu kwa kuwa ndio njia salama”, alisema Mauki.

    Aidha, aliwaasa wakristo kuacha tabia ya umbea kwa kuzungumzia watu wengine badala yake wajenge mazoea ya kuwafikishia wahusika mambo yanayowahusu.

    Mwakilishi wa Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (UKWATA) Beatrice Vales kutoka Shule ya Sekobdari ya Kwembe aliushukuru uongozi wa mtaa huo, wazazi na walezi kwa kuwawezesha kuhudhuria kongamano la Pasaka ambapo wamejifunza vitu vingi.

    Beatrice Vales kutoka Shule ya Sekobdari ya Kwembe akitoa mrejesho kwa niaba ya wanafunzi wenzake kuhusu safari yao kwenye Kongamano la Pasaka, kulia na kushoto kwake ni alioambatana nao. Nyuma yao ni Mwinjiisti Kiongozi wa Mtaa huo, Bi.Emeline Mzava kushoto zaidi mwisho ni Mtendakazi Bi Anna Mauki, (Picha na Vincent Mpepo).

    “Tulihudhuria na na kufundishwa masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya uzazi, mahusiano, afya ya akili na masuala ya kujiandaa nayo kabla ya kuoa au kuolewa”, alisema Beatrice.

    Aliomba washarika wa mtaa huo kuwawezesha ili wapate Mwalimu wa kwaya ili wafanye mazoezi na wakati mwingine waweze kuimba na kuonesha talanta zao kama baadhi ya shule ambazo walifanya hivyo kwenye kongamano hilo.

    Mwenyekiti wa Ujenzi wa Mtaa huo, Exaud Mchome aliwajulisha washarika kuwa mabati yatakuwa tayari wiki ijayo na kwamba hatua inayofuata baada ya kuezeka ni kupiga lipu (plasta) na upakaji wa rangi ya awali (skimming).

    Aliwashukuru washarika kwa sadaka hiyo na kuwaomba waendelee kumtolea Mungu ili kukamilisha ujenzi huo na kwamba awamu ya kwanza ya utoaji wa sadaka hizo itaisha Mwezi Juni 2025.

  • Na Vincent Mpepo

    Kwa kawaida tumesikia ikizungumzwa kuwa afya bora ndio mtaji wa kwanza. Kauli hii inaangazia umuhimu wa kuwa na afya njema kwani ndiyo inakuwezesha kufanya mambo mengine ikwemo kufanya kazi au shughuli ambayo itakuingizia kipato.

    Kutokuwa na afya njema husababisha mambo mengi kutoenda vyema au kukwama kwa masuala mbalimbali ikiwemo shughuli za uzalishaji, utoaji huduma na za kujiingizia kipato kama biashara, kushindwa kufanya kazi kama ni muajiriwa au hata kazi binafsi

    Athari za changamoto za kiafya husababisha kushusha pato la mtu mmojammoja, familia na jamii kwa ujumla kutokana na kushuka kwa uzalishaji iwe ni kwa siku, wiki, mwezi au hata muda mrefu zaidi.

    Ndio maana serikali, jamii na hata katika ngazi ya mtu mmojammoja ni muhimu kuwekeza katika afya kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwa na bima za afya zitakazokusaidia kupata matibabu muda wowote utakapokuwa na changamoto ya kiafya, kuwekeza katika lishe bora, kufanya mazoezi na wakati mwingine kutoruhusu unywaji wa dawa za viwandani bila kufuata ushauri wa wataalamu.

    Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Emmanuel Mallya aliwahi kusema ni muhimu kwa jamii hususani vijana kuwekeza katika afya kwa kuwa ndio mtaji wa kwanza kabla ya vitu vingine.

    Maneno ya Dkt.Malya yanaungwa mkono na Daktari Julius Mchelele kutoka Kliniki ya Path Labs jijini Dar es salaam kuwa jamii inatakiwa kujenga utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kuwa na uhakika wa maendeleo ya kiafya badala ya kusubiri vipimo wakati wa homa.

    Katika kuhakikisha mtu anakuwa na afya bora suala la lishe ni muhimu kwa kuwa hatupaswi kula kila kitu na wakati wote bali ni kujua unakula nini, wakati gani na kwa kiasi gani na hii inaenda sanjali na mitindo ya maisha itakayosaidia kulinda na kuimarisha kinga ya mwili.

    “Wapo ambao wamezoea kula kila wanapohisi njaa, wakati mwingine ruhusu mwili ujile wenyewe”, anasema Dkt.Mwangaza.

    Kumbe wakati mwingine kukaa bila kula kuna faida kwa kuwa huupa mwili namna ya kustahimili changamoto mbalimbali.

    Kinga ya mwili dhidi ya magonjwa wakati mwingine himarishwa kwa aina ya mitindo ya maisha ambayo wataalamu wanashauri, kwa mfano kufanya mazoezi ambayo yataushughulisha mwili na kuzingatia mlo kamili.

    Kwa mu`jibu wa Dkt. Omary Mwangaza amabye ni Mratibu wa Tiba Manispaa ya Kinondoni anasema kutofanya mazoezi na ulaji mbovu usiozingatia makundi muhimu ya vyakula ni mojawapo ya sababu ya kudhoofisha mwili zinazosababisha magonjwa sugu yasiyoambukizwa.

    Dkt. Mwangaza anabainisha baadhi ya mitindo ya maisha yenye faida kwa afya ya mwanadamu ikiwemo kufunga, kufanya mazoezi na kupata mwanga wa jua wa asubuhi ambao una zaidi ya asilimia 85 za vitamin D zinazosaidia kutengeza kinga ya mwili.

    Kwa mujibu wa Rehema Kingu ambaye ni Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa Wilaya ya Bagamoyo anasema tatizo la magonjwa yasiyoambukizwa kitakwimu linawagusa watu kwa asilimia 74 duniani, asilimia 86 katika maeneo ya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na asilimia 34 kwa nchi ya Tanzania.

    Hivyo tatizo la magonjwa sugu yasioambukizwa nalo ni changamoto inayoathiri afya za watu wengi duniani, Afrika na Tanzania.

    Kutokana na changamoto hiyo taasisi mbalimbali za afya za umma na binafsi zimejaribu kutafuta namna ya kuwafikia watu mahalai walipo kwa ajili ya kutoa elimu, ushauri na vipimo ili kusaida jamii.

    “Tumemua kuwafuata mahali walipo badala ya kuwasubiri waje hospitalini”, anasema Rehema.

    Pamoja na masuala ya asili ya namna ya kulinda afya yanayohusisha kufanya mazoezi na mengineyo suala la lishe linabaki kuwa muhimu sana katika kuhakikisha afya zinaimarika.

    Mtaalamu wa lishe ambaye ni Kaimu Afisa Lishe wa Wilaya ya Bagamoyo, Flora Boniface anasema ni muhimu kwa mlaji kuwa na mlo kamili unaozingatia vyakula katika makundi ya nafaka, jamii ya kunde, asili ya wanyama, mbogamboga na matunda.

    “Mbogamboga zikiwekwa mafuta kiasi ni nzuri zaidi kuliko mboga isiyo na mafuta kabisa kwani ni sawa na kula makapi”, alisema Flora.

    Aidha, anaitahadharisha jamii dhidi ya ulaji wa matunda mchanganyiko kwa wakati mmoja kuwa si kitu chema kifaya kwa kuwa ulaji huo unaweza kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari.

     “Ulaji wa matunda kama tikiti na nanasi kwa wakati mmoja unaweza kuwa chanzo cha kisukari ikiwa mlaji hajui kiwango cha sukari katika mwili wake”, anasema Flora.

    Picha zote ni msaada wa akili mnemba

  • Na Tabia Mchakama

    Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki mahafali ya 41 ya Kidato cha sita ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani na kuelezea nia yake ya kuendelea kushirikiana na shule hiyo kongwe.

    Akizungumza katika mahafali hayo kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania, Meneja wa TIRA Kanda ya Mashariki, Zakaria Muyengi aliupongeza uongozi wa shule hiyo na wanafunzi kwa ufaulu mzuri katika mitihani ya taifa kwa miaka mbalimbali.

    Alisema TIRA itatoa msaada wa samani mbalimbali zikiwemo meza na viti kulingana na upungufu uliopo na kwamba itasaidia baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupata bima za afya na kusaidia ujenzi wa jengo la kulia chakula ikiwa ni changamoto zilizoainishwa.

    Aidha, mamlaka hiyo iliwataka walimu, wazazi na wanafunzi kutumia bidhaa mbalimbali za bima ikiwemo bima ya maisha na bima za kawaida ili kujikinga na majanga yasiyotarajiwa na kwamba walikaribishwa katika ofisi za mamlaka hiyo kupata elimu zaidi kuhusu kuhusu masuala ya bima.

    Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Bi. Bhoke Nyagonde aliishukuru TIRA kwa ushirikiano walioonesha na msaada uliotolewa huku akibainisha kuwa malengo ya walimu katika shule hiyo ni kuongeza uzalendo na kutoa elimu bora ili kujenga wasichana wazalendo kwa taifa lao na ili wawe viongozi bora.

    Moja ya mikakati ya mamlaka hiyo kutoa elimu ya bima kwa makundi mbalimbali kupitia warsha, mikutano, na semina ili kuhakikisha elimu ya bima inaufikia umma wa watanzania.

    Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani ni miongoni mwa shule kongwe nchini Tanzania iliyoanzishwa Mei 28, 1928 na inapatikana katikati ya jiji la Dar es salam eneo la Jangwani karibu na soko la kimataifa la la Kariakoo.

  • Na Gabriel Msumeno

    Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Pwani wametakiwa kuweka mikakati ya kuimarisha maadili kwa watoto shuleni.

    Wito huo umetolewa April 23 na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala alipokuwa akifungua mkutano mkuu CWT Mkoa wa Pwani uliofanyika mjini Kibaha.

    Twamala aliwataka walimu kutafakari namna bora za kuwafundisha na kuwashauri watoto shuleni ili shule ziendelee kuwa sehemu muhimu ya kuzalisha jamii inayotambua na kuishi katika maadili kama ilvyokuwa katika miaka ya nyuma.

    “Tutafakari kuhusu maadili ya watoto tunaowalea na baadae kushauri kwenye shule zetu Ili wakue katika maadili mema kwani kwa sasa maadili yameporomoka”, alisema Twamala.

    Aiidha, aliwataka walimu kuchagua kuchagua viongozi bora wenye sifa na watakaosimamia masuala ya walimu katika uongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano.

    Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susan Shesha aliishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi ya walimu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

    Alisema pamoja na mafanikio hayo walimu bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutolipwa stahiki zao licha ya kuhakikiwa tangu Mwaka 2017.

    Aliainisha changamoto hizo kuwa ni kutolipwa fedha za uhamisho, likizo na nauli huku kukiwa na walimu ambao hawajapandishwa madaraja pamoja na kukidhi vigezo.

    Changamoto nyingine ni kutozingatiwa kwa mabaraza ya wafanyakazi na pia uhaba wa walimu katika shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa huo.

    Mkutano Mkuu wa chama hicho Mkoa hufanyia baada ya kufanyika mikutano mingine ngazi ya Wilaya ambayo iliambatana na uchaguzi wa viongozi.

  • Na Gabriel Msumeno

    Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga Omary Mwanga amewataka wakazi wa Wilaya hiyo kuongeza thamani ya mazao ya nyuki ili kuwa bidhaa bora ambazo zitakuwa na tija katika kukuza uchumi wao.

    Wito huo aliutoa hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya siku ya nyuki yaliyofanyika Wilayani humo na kuhusisha vikundi mbalimbali vya wafugaji nyuki.

    “hii siyo kwenye asli tu ni bali hata bidhaa nyingine zinazopatikana kwenye asali uwe na uwezo wa kuziongezea thamani ili bora kiushindani katika biashara”, alisema Mwanga.

    Alisema ni muhimu kujitangaza kupata ili kuapata wateja huku serikali ikitafuta namna ya kuwasogezea fursa zinazopatikana kwenye ufugaji wa nyuki.

    Kadhalika Katibu Tawala huyo alisema ni vema kubadilisha mfumo wa maadhimisho kama hayo Ili yaweze kuwa na tija kwa washiiriki kwa kuwa kikao kazi na kutengeneza maazimio ya namna ya kuinua ufugaji.

    Aidha, alishauri wataalamu kuyatumia maadhimisho kama hayo kwa nyakazi zijazo kama fursa ya kutoa ujuzi kwa wafugaji nyuki ili waboreshe shughuli hizo kwa faida zaidi.

    Mkuu wa Kitengo cha Uhifadhi na Utunzaji Misitu Wilaya ya Mkuranga, Asted William alisema kwa kipindi cha miaka mitano wamefanikiwa kuwa na mizinga ya kisasa 1,015 na mizinga ya kienyeji 72 yote ikizalisha ikizalisha zaidi ya tani 3000 ya asali.

    “Tunaishukuru serikali kwa namna iliweka kipaumbele suala la ufugaji nyuki kwa kuhakikisha inatengenezwa mazingira wezeshi ya soko la asali kuuuzwa katika masoko ya nje ya nchi ikiwemo China na nchi nyingine duniani,” alisema William

    Sanjali na hayo alisema Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mkutano mkubwa unaowakutanisha wadau wa ufugaji nyuki duniani.

    Kwa mujibu wa Asted kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi, yanayotokana na uchomaji wa moto mazinga na mbinu za uvunaji zisizo za kitaalamu.