• Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda akiongea na wafanyakazi na wanafunzi wakati wa ufunguzi wa kambi ya siku mbili ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa iliyoanza Leo chuni hapo. Kulia kwake ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia mipango, fedha na utawala, Pfofesa Josiah Katani akifuatiwa na Mkurugezi wa Rasimaliwatu Bw.Francis Badundwa, wakati kushoto ni Mratibu wa Kitengo cha Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa chuoni hapo, Dkt. Wambuka Rangi na Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa Wilaya ya Bagamoyo, Rehema Kingu

    Na Vincent Mpepo

    Imeelezwa kuwa ulaji hovyo wa vyakula usiozingatia mlo kamili na kutofanya mazoezi ni baadhi ya visababishi vya magonjwa sugu yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

    Hayo yameelezwa na wataalamu wa afya waliopo kwenye kambi ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa kwa wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Kinondoni jijini Dar es salaam.

    Akitoa elimu ya afya kwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho leo, Mratibu wa Tiba Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Omary Mwangaza alisema kutofanya mazoezi na ulaji mbovu usiozingatia makundi muhimu ya vyakula ni mojawapo ya sababu ya magonjwa sugu yasiyoambukizwa.

     “Wapo ambao wamezoea kula kila wanaposikia njaa, wakati mwingine ruhusu mwili ujile wenyewe”, alisema Dkt.Mwangaza.

    Alibainisha baadhi ya tabia zenye faida kwa afya ya mwanadamu kuwa ni pamoja na kufunga, kufanya mazoezi na kupata mwanga wa jua wa asubuhi ambao una zaidi ya asilimia 85 za vitamin D zinazosaidia kutengeza kinga ya mwili.

    Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa Wilaya ya Bagamoyo, Rehema Kingu alisema tatizo la magonjwa yasiyoambukizwa kitakwimu linawagusa watu kwa asilimia 74 duniani, asilimia 86 katika maeneo ya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na asilimia 34 kwa nchi ya Tanzania.

    “Tumemua kuwafuata mahali walipo badala ya kuwasubiri waje hospitalini”, alisema Rehema.

    Kwa upande wake, Kaimu Afisa Lishe wa Wilaya ya Bagamoyo, Flora Boniface alisema ili kuwa na mlo kamili walaji wanatakiwa kuzingatia vyakula katika makundi ya nafaka, jamii ya kunde, asili ya wanyama, mbogamboga na matunda.

    “Mbogamboga zikiwekwa mafuta kiasi ni nzuri zaidi kuliko mboga isiyo na mafuta kabisa kwani ni sawa na kula makapi”, alisema Flora.

    Aidha, aliitahadharisha jamii dhidi ya ulaji wa matunda mchanganyiko kwa wakati mmoja kuwa si kitu chema kifaya kwa kuwa ulaji huo unaweza kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari.

    “Ulaji wa matunda kama tikiti na nanasi kwa wakati mmoja unaweza kuwa chanzo cha kisukari ikiwa mlaji hajui kiwango cha sukari katika mwili wake”, alisema Flora.

    Akifungua kambi hiyo ya upimaji chuoni hapo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda alikishukuru Kitengo kinachoghulikia Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa chuoni hapo kuwa kuratibu vizuri ujuo wa wataalamu hao.

    “Kila mtu anapaswa kutambua kuwa afya ndio mtaji wa kwanza na ikiwa kuna asiyetambua umuhimu na thamani ya afya njema atembelee hospitali”, alisema Profesa Bisanda.

    Mratibu wa Kitengo cha Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa chuoni hapo, Dkt. Wambuka Rangi aliishukuru menejeimneti ya chuo hicho na watalaamu hao kufanikisha kambi hiyo.

    Kwa mujibu wa Dkt. Rangi kambi hiyo ya upimaji ya siku mbili imeanza leo na itahitimishwa kesho kwa Dar es salaam na kwamba kitengo chake kinakusudia kuvifikia vituo vyote vya mikoa vya chuo hicho.

    Mratibu wa Kitengo cha Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa Chuo Kikuu Huria Tanzania Dkt. Wambuka Rangi akiongea na jumuiya ya wafanyakazi na wanafunzi wakati wa ufunguzi wa kambi ya siku mbili ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa iliyoanza Leo chuni hapo.

    Mfamasia Lina Laiton kutoka Wilaya ya Bagamoyo akitoa huduma kwa mfanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Petro Sanga katika siku ya kwanza ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa iliyoanza Leo chuni hapo (Picha zote na Vincent Mpepo).

  • Picha kwa msaada wa Akili Mnemba

  • Kwaya ya akiba baba wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe wakiimba wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka, (Picha na Vincent Mpepo).

    Na Vincent Mpepo

    Wakristo nchini wametakiwa kuendelea kutimiza wajibu wao katika nafasi mbalimbali ambazo Mungu amewajalia ili kumtumikia yeye na kuishi vyema katika jamii.

    Wito huo umetolewa na Mtheolojia, Esther Mshana wakati akihubiri katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka Leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe na kusisitiza kuwa ufufuo wa Yesu usiadhimishwe kwa mazoea bali kuwe na upya ili uwe na maana kwa mkristo na jamii kwa ujumla.  

    “Kama Yesu asingefufuka kungekuwa na namna isiyoelezeka katika jambo hilo na kwamba siku hii isingekuwa na maana”, alisema Mtheolojia Esther.

    Alisema ni muhimu kila mkristo kutimiza wajibu wake bila kujali changamoto anazopitia na dira yake iwe ni utimilifu wa malengo yaliyowekwa kwa utukufu wa Mungu akitolea mfano wanawake waliojihimu kwenye kaburi la Yesu ili kuupaka mwili mafuta na manukato ambao hawakukatishwa tamaa na vikwazo.

    “Tusiache kutimiza wajibu wetu kwa vikwazo tunavyowekewa, badala yake tusonge mbele”, alisema Mtheolojia Esther.

    Alisema wakati mwingine wakristo kama binadamu wanakatishwa tamaa na habari mbaya wanazopokea kuhusu wao wenyewe au watu wanaowahusu hivyo kutozipa nafasi habari hizo ili kazi na kusudi la Mungu litimie.

    Mtendakazi katika Mtaa huo, Anna Mauki aliishukuru Kamati ya Malezi na washarika kwa namna mbalimbali wanavyofanya kazi ya Mungu hususani malezi ya watoto ambao jana walitumika kufanya uinjilishaji kupitia vyombo vya habari vya Upendo ikiwemo Redio Upendo (107.7 FM).

    “Tuwekeze kwenye utumishi kwa ajili ya watoto na wala tusiwazuie katika masuala ya kikanisa”, alisema Mtendakazi Anna.

    Christina Bukuku aliwajulisha washarika kuwa katika Jumapili ya kwanza ya Mwezi Mei ambapo huadhimishwa siku ya wafanyakazi duniani kutakuwa na sadaka maalumu kwa ajili ya watumishi wa Mungu mtaani hapo.

    “Tuliwahi kufanya hivyo kwa miaka iliyopita na tumejisahau, Mwaka huu tuanze ule utaratibu na tuendelee nao”, alisema Christina.

    Kwa upande wake, Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwakumbusha washarika wa Mtaa huo kuacha ukristo wa Sikukuu na badala yake kurudi nyumbani kwa Bwana kutokana na tabia ya baadhi kuhudhuria kwenye ibada za siku za Sikukuu ikiwemo Pasaka na Noel.

    “Kuhusu sadaka ya ujenzi wa Kituo cha Mimataifa cha kulelea watoto wenye mahitaji Maalumu cha Kitopeni niwaombe tuendelee nayo kama mnavyofahamu 31/05/2025 ndio kilele na Baba Askofu atakuwepo kuopkea sadaka hiyo,” alisema Mwinjilisti Mzava.

    Naye, Mwenyekiti wa Ujenzi Mtaani hapo, Exaud Mchome aliwatakia heri ya Sikukuu ya Pasaka washarika wote mtaani hapo na kuwajulishwa kuwa ujenzi unaendelea vizuri.

    Kwaya wa watoto wa shule ya Jumapili wakiimba katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

    Alisema wamesimama kwenye eneo la uezekaji kutokana na kusubiri foleni ya upatikanaji wa bati ambazo zilishawekewa oda na kulipiwa katika kampuni ya Alaf na kwamba zikiwa tayari muda wowote kazi hiyo itafanyika.

    “Niwakumbushe tuendelee kumalizia ahadi zetu kwa awamu ya kwanza ya Januari-June 2025”, alisema Mchome.

    Akielezea umuhimu wa kuwa na jengo kubwa akihusisha idadi kubwa ya washarika siku za Sikukuu ambapo wakati mwingine inaweza kuwakosesha utulivu na ufuatiliaji wa ibada kutokana na hali ya hewa kama mvua ikiwa watakaa nje kama ilivyo sasa.

    Sikukuu ya Pasaka Mtaani hapo imesherehekewa kwa namna mbalimbali ikiwemo ujumbe wa neno la Mungu kupitia kwaya zote, simulizi na mistari ya moyo kutoka kwa watoto wa shule ya Jumapili na maigizo kutoka kwa akina mama wakiongozwa na Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava.

    Watoto wa Shule ya Jumapili wakihubiri kupitia simulizi katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

    Akina mama wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe ambao waliigiza wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka ambapo igizo lao liliangazia ufufuo wa Yesu Kristo. (Picha na Vincent Mpepo).

    Kwaya wa watoto wa shule ya Jumapili wakiimba katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

  • Na Farida Mkumba, Dodoma 

    Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo) kinatarajia kudahili wanafunzi 9,300 katika ngazi za stashahada, stashahada na ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

    Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa ameeleza hayo jana Aprili 16 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026.

    Alisema chuo hicho ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kimepanga kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 7.77 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mengineyo.

    “Shughuli zilizopangwa kutekelezwa na chuo hiki ni kudahili wanafunzi 9300 na kuanza kutoa mafunzo ya shahada ya kwanza ya nyaraka na kumbukumbu kwa kudahili wanafunzi 100 baada ya mtaala kukamilika” Alisema Mchengerwa.

    Alisema chuo kitazijengea uwezo mamlaka za serikali za mitaa 40 na taasisi tano kupitia mafunzo ya muda mfupi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

    Alisema shunguli nyingine zitakazofanywa na chuo hicho kwa kipindi hicho ni kufanya tafiti 6 na machapisho 30 ya kitaaluma katika majarida mbalimbali yenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika mamlaka za serikali za mitaa na wadau wengine.

    “Eneo lingine litakaloangaziwa ni ukarabati wa mabweni, nyumba za watumishi na miundombinu ya maji”, alisema Mh.Mhengerwa.

    Alisema kiasi cha shilingi milioni 575 kitatumika kufanya ukarabati wa mabweni manne ya wanafunzi, nyumba saba za watumishi ikiwa ni pamoja na miundombinu ya maji na umeme.

    Aidha, kuhusu kuwaendeleza watumishi wa chuo waziri Mchengerwa alisema kwa mwaka 2025/26 watumishi 27 wataendelezwa kielimu katika ngazi mbalimbali ambapo watano ni shahada, 11 Uzamili na Shahada ya Uzamivu 11.

    Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, Mh. Justine Nyamoga alisema kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 Chuo cha Serikali za Mitaa kilikadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 10.5.

    Aidha, aliipongeza serikali kwa utekelezaji wa ushauri, maoni na mpendekezo 13 yaliyotolewa na kamati yake.

    “Kwa maeneo ambayo hayajatekelezwa kikamilifu, kamati inasisitiza yaendelee kufanyiwa kazi ikiwemo suala la shule za mchepuo wa Kiingereza”, alisema Mh. Nyamoga.

  • Na Farida Mkumba, Dodoma  

    Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeomba Shilingi trilioni 11.78 kwa matumizi ya mwaka wa fedha 2025/2026.

    Katika hutuba aliyoisoma Leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa alibainisha kuwa Trilioni 3.95 zitakwenda kwenye miradi ya maendeleo, na Trilioni 7.84 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

    Waziri Mchengerwa alisema bajeti hiyo inakusudia kuleta matumaini na maendeleo kwa wananchi wote na kusisitiza ushirikiano kati ya serikali, mikoa, na wananchi.

    Aidha, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mwelekeo mzuri wa maendeleo kwa watanzania.

    Bajeti ya TAMISEMI kwa mwaka huu wa fedha imeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo ilikuwa trilioni 10.13.

  • Na Tabia Mchakama

    Wanawake TIRA wamejumuika na Wanawake wengine kutoka sekta ya Fedha Tanzania  kushiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka ulioandaliwa na jumuiya yao (TAWiFA) ambapo DKt. Doto Biteko alikua Mgeni Rasmi.

    Akisoma hotuba yake Mhe. Biteko alisisitiza juu ya elimu ya fedha kwa wanawake wa vijijini ili waepukane na mikopo umiza inayosababisha kuchukuliwa baadhi ya mali zao za ndani wanaposhindwa kurejesha mikopo hiyo.

    Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Bima Bi. Khadija Issa Said ameeleza namna sekta ya bima ilivyokua nchini huku wanawake katika sekta hiyo wakitoa mchango mkubwa kupitia uongozi makini lakini ufanyaji kazi wao katika nafasi mbalimbali.

    Bi. Khadija aliwataka wanawake kwenye sekta ya fedha kuendelea kujibiidisha kazini na kushirikiana ili waendelee kukuza sekta ya fedha.

    Aidha Bi. Fikira Mtomola, Rais wa TAWiFA alisema mkutano huo wenye kauli mbiu ya “Wekeza kwa wanawake ili kuchochea maendeleo” una lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji wa wanawake katika sekta ya fedha nchini na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wanawake ili kujumuishwa na kuongoza katika mambo mbalimbali ya kifedha.

    Mkutano Mkuu  huo uliofanyika Aprili 14, 2025 Jijini Dodoma ulihudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali akiwemo Dkt. Angela Kairuki  Mshauri wa Rais na Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma, Naibu Waziri wa Fedha, Bwn. Hamadi Chande na wengine wengi.

    Mkutano huo ulitanguliwa na matukio mbalimbali ambapo tarehe 11 Aprili 2025 kulikua na upandaji wa Miti ya Matunda zaidi ya 2000 katika Shule za Msingi za Mkoa huo, tarehe 12 Aprili 2025 utoaji elimu ya fedha kwa wanawake wajasiriamali iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zabibu, Dodoma.

  • Wanafunzi wakiuliza na kujibu maswali mbalimbali katika mafunzo yaliyotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.

    Na Okello Thomas

    Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetembelea wanafunzi na walimu wa shule mbalimbali za sekondari wilayani Mafia na kutoa elimu kuhusu vinasaba katika jinai ikiwemo upatikanaji wa haki kwenye matendo ya ubakaji, ulawiti pamoja na kuzifahamu kemikali na madhara yake.

    Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa alisema  madhumuni ya elimu ya vinasaba na kemikali kwa wanafunzi ni kuhamasisha wapende masomo ya sayansi na kuwa mabalozi katika kuelimisha jamii inayowazunguka kuhusu vinasaba na kemikali.

    Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa (aliyesimama) akielezea majukumu mbalimbali ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kirongwe Aprili 9, 2025

    “Kupitia elimu ya vinasaba, tunaamini wanafunzi wamepata uelewa juu ya nini cha kufanya ikitokea mwanafunzi mwenzao amekumbwa na tatizo la ubakaji au ulawiti pamoja na kutatua changamoto za ajali za kemikali,” alisema Mkapa.

    Afisa Elimu Maalumu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Musa Abdallah ameishukuru Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwafikia wanafunzi ambao ndio walengwa wa masuala mbalimbali katika jamii lakini pia kuwa viongozi na wanasayansi wa baadae.

    Naye mwalimu wa masomo ya sayansi katika shule ya sekondari Baleni, Eddy Mjige amesema ujio wa wataalam kutoka GCLA utakuwa na manufaa makubwa kwa walimu wa masomo ya sayansi hususani uendeshaji wa maabara na matumizi sahihi ya kemikali kwenye wakati wa elimu kwa vitendo.

    Sambamba na hayo, mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Kilindoni, Yahya Hafidhi ameiomba Mamlaka kuendelea na utoaji wa elimu kuhusu majukumu yao na mbinu za kuwawezesha wanafunzi kutoa elimu kwa jamii inaowazunguka.

    Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika kuanzia Aprili 9 hadi 10, 2025 kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.

    Mtumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Emmanuel Jacob, akitoa elimu kuhusu masuala ya alama na madhara ya kemikali kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidawendui Aprili 10, 2025

  • Sehemu ya wadahiliwa wapya wa fani mbalimbal na katika ngazi mbalimbali waliohudhuria mafaunzo elekezi siku ya Jumamosi katika Kituo cha Mkoa cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dodoma. (Picha kwa niaba ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Kituo cha Mkoa wa Dodoma).

  • Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo juu ya Chuo cha Serikali za Mitaa alipotembelea banda la chuo hicho wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi inayojihusisha na maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) yanayoendelea katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma uliopo Mji wa Kiserikali Mtumba yaliyoanza Tarehe 14 hadi 16 Aprili, 2025.

    Kauli mbiu katika mafunzo hayo ni “Ugatuzi wa rasilimali fedha katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa”(Picha na Farida Mkumba).

  • Na Vincent Mpepo

    Watu wenye mahitaji maalumu ni kundi la watu ambao hawawezi kujipatia mahitaji yao ya msingi wao wenyewe kutokana na changamoto kadha wa kadha.

    Changamoto hizo husababishwa na vitu mbalimbali kama vile ulemavu wa kimwili, kihisia, kitabia, au kujifunza au kuharibika ambazo husababisha mtu kuhitaji huduma za ziada au maalum au malazi kama vile elimu au burudani.

    Ili kundi hili lipate mahitaji huduma za msingi kama walivyo binadamu wengine ni lazima jamii ihusike kwa namna moja au nyingine ili kuhakikisha kuwa jukumu hili linatekelezwa.

    Utekekezaji wake huhusisha serikali, jamii, makundi mbalimbali, taasisi za dini, mashirika na taasisi za umma na binafsi.

    Ushirikiano wa taasisi mbalimbali unasaidia kuwa na nguvu ya pamoja ili kuhakikisha kundi hili muhimu linapata stahiki na haki za kibinadamu ili kuwa na jamii yenye ustawi bora, isiyo na wanaoachwa au kutengwa kwa namna yoyote.

    Ushirikiano huu unawaleta pamoja wadau mbalimbali kwa namna ya uwezo na aina ya huduma wanazotoa ili kwa pamoja kuwa na uwezeshaji wa hali na mali katika ngazi mbalimbali. Kwa mfano taasisi za elimu kama Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kina idara maalumu inayohusika na watu wenye mahitaji maalumu.

    Sanjali na kitengo hicho, idara ya sosholojia na ustawi wa jamii nayo imekuwa ikifanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna bora za kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

    Idara hiyo, imekuwa na makubaliano na taasisi za ndani na nje ya nchi ili kupata msaada wa kitaaluma wa namna ya kuongeza wigo wa maarifa kuhusu elimu ya watu wenye mahitaji Maalumu ikigusa eneo la ualimu wa elimu Maalumu na ufundishaji.

    Idara hiyo kupitia ushirikiano na vyuo vikuu vya nje ikiwemo Norway kupitia Mradi wa Norec ambao umesaidia masuala mbalimbali ikiwemo programu za kubadilishana uzoefu zinazowahuhisha wahadhiri, wanafunzi, maofisa maendeleo ya jamii na wadau mbalimbali wa maswala ya ustawi wa jamii.

    Kwa mujibu wa Daktari Mariana Makuu, mtoto mwenye mahitaji maalum awapo shuleni anatakiwa kulelewa vyema ili apate huduma tatu muhimu ikiwemo elimu, afya na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

    “Kundi la watoto wenye mahitaji maalumu linakabiliwa na ukatili wa aina mbalimbali unaosababisha watoto hawa kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia”, anasema Dkt.Mariana.

    Uwepo wa wataaam wa ustawi wa jamii shuleni wenye jukumu la kuangalia masuala ya kijamii kwa watoto hawa wakisaidiana na walimu utasidia kuibua na kuzuia ukatili na matatizo mengine yanayowakabili watoto hususani wenye ulemavu.

    “Serikali ione umuhimu wa kuaajiri wataalam hawa ili kuendana na mabadiliko ya jamii kwa sasa,” anasema Dkt. Makuu.

    Wakati huohuo, ushirikiano wa serikali na taasisi za dini nao una nafasi nzuri kuhaikisha jamii na husani ya wenye mahitaji maalumu wanajaliwa ili kuwa na jamii inayojali watu wote bila kujali ulemavu wa aina yoyote.

    Hivi karibuni tumeshuhudia mazungumzo kati ya kiongozi mkuu wa nchi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ulioongozwa na Mkuu kanisa na Mkuu wa Dayosisi hiyo Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa Ikulu jijini, Dar es Salaam.

    Katika mazungumzo hayo, Dkt. Samia pamoja na viongozi hao walijadili kuhusu utoaji wa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum hususan wenye changamoto ya afya ya akili.

    Viongozi kanisa wameipongeza na kuishukuru serikali kwa ushirikiano inaotoa kwa kanisa kwani serikali imeahidi kushirikiana na kanisa ili kujenga Kituo kikubwa zaidi kitakachohudumia watoto wenye changamoto ya afya ya akili ili watoto wengi waweze kupata huduma hiyo.

    Wakati serikali, taasisi za umma na binafsi za ndani na nje zikifanya kila linalowezekana kusaidia kundi la watu wenye mahitaji Maalumu swali ni kwa jamii tunafanya nini kuunga mkono kwa sehemu yetu?

    Ni dhahiri kuwa bado elimu inahitajika ili masuala ya watu wenye mahitaji Maalumu yapate wigo mpana wa kuelezwa kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari, mikutano mbalimbali na kila ambapo fursa ya kufanya hivyo itajitokeza.