• Na Vincent Mpepo

    Mtaalamu wa huduma za ushauri wa kitaalamu Innocent Deus amewataka wasomi katika fani za sanaa na sayansi za jamii kudhihirisha mchango wao katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kupitia eneo la ushauri wa kitaalamu.

    Aliyasema hayo wakati wa mafunzo ya kitaalamu kwa wanataaluma na waendeshaji  katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es salaam.

    “Changamoto za kijamii zinahitaji utatuzi kutoka kwa wasomi katika fani hizi na kwamba uwepo wenu utaleta tija ikiwa mtasaidia jamii kukabiliana na changamoto”, alisema Deus.

    Akizungumzia uandishi miswada ya kazi za ushauri wa kitaalamu alisema kuna umuhimu wa waandishi kuzingatia masuala kadhaa ikwemo namna ya uandishi, ushawishi na namna ya uwekaji malengo ya mradi na kutojifungia ofisini badala yake kuonesha umahiri wao ili jamii itambue.

    Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii chuoni hapo, Dkt. Mariana Makuu mafunzo hayo yanalenga kubadili mtazamo wa kufikiri na utendaji kutoka tafiti za kinadharia kwenda kwenye huduma za ushauri wa kitaalamu zenye matokeo halisi kwa jamii.

    “Wakati umefika kwa wanataaluma kugeuza maarifa na nadharia wanazozalisha kuwa vitendo vinavyogusa maisha ya wananchi kupitia huduma za ushauri wa kitaalamu,” alisema Dkt. Makuu.

    Aidha, aliwahimiza washiriki kuyafuatilia mafunzo hayo kwa umakini ili kupata ujuzi na umahiri  utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali za kijamii kwa maslahi mapana ya taifa.

    Mratibu wa Ushauri wa Kitaalamu na Uhusiano wa Jamii wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii (FASS), Celia Muyinga alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wafanyakazi wa kitivo hicho ili kuwajengea uwezo na kujiamini katika kutafuta fursa mbalimbali za kazi za huduma za ushauri wa kitaalamu.  

    “Tathmini za hivi karibuni zinaonesha kuwa ushiriki wa wanataaluma katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii (FASS), katika uandaaji wa maandiko ya miradi na kushiriki katika zabuni za ushauri wa kitaalamu bado ni mdogo”, alisema Celia.

    Alisema hali hiyo inatokana na mtazamo kuwa taratibu za kiufundi ni ngumu, pamoja na ukosefu wa kujiamini katika kushindana kwenye mazingira ya ufadhili yenye ushindani mkubwa.

    Alibainisha athari za changamoto hizo kuwa ni kukwamisha kitivo katika kuvutia rasilimali za nje na kutoifikia jamii kwenye huduma za ushauri wa kitaalamu na kutotumika ipasavyo kwa wataalamu waliopo katika kitivo hicho.

  • Na Vincent Mpepo

    Wanataaluma katika taasisi za elimu ya juu nchini wametakiwa kufanya tafiti zenye kuleta matokeo chanya, ikiwemo kutatua changamoto mbalimbali za kijamii na kubadili maisha ya wananchi, badala ya kuzihifadhi kabatini mara baada ya kuhitimu.

    Wito huo umetolewa na washiriki wa mafunzo ya ushauri wa kitaalamu ya siku mbili yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yamewakutanisha wanataaluma na waendeshaji kutoka Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii pamoja na vitivo vingine vya chuo hicho.

    Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mtiva wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii, Dkt. Mariana Makuu, alisema kuwa wakati umefika kwa wanataaluma kugeuza nadharia kuwa vitendo ili kutatua changamoto za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.

    “Mafunzo haya yanalenga kubadili mtazamo wa kufikiri na utendaji kutoka tafiti za kinadharia pekee kwenda kwenye tafiti zenye matokeo halisi,” alisema Dkt. Makuu.

    Aliongeza kuwa matarajio ya kitivo ni kuona mafunzo hayo yakileta matokeo chanya kwa washiriki mmoja mmoja na kwa taasisi kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuchochea umahiri katika kazi za ushauri wa kitaalamu.

    Aidha, aliwahimiza washiriki kufuatilia mafunzo hayo kwa makini ili kupata ujuzi utakaosaidia kuongeza uelewa na mchango wao katika eneo la ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya utatuzi wa changamoto mbalimbali za jamii kwa maslahi mapana ya taifa.

    Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo, Innocent Deus, alisema kuwa wasomi, wanataaluma na watafiti wanapaswa kuwa na mawazo bunifu yatakayosaidia kutatua changamoto za jamii kupitia tafiti wanazozifanya, ili kuhalalisha uwepo na mchango wao katika jamii.

    Akizungumzia masuala ya ushauri wa kitaalamu, alisema ni muhimu kwa watafiti na wataalamu kuanza kushirikiana na taasisi zenye uzoefu katika fani husika ili kujijenga kitaaluma, kutengeneza taswira chanya na kuvutia wadau mbalimbali wa kushirikiana nao siku zijazo.

    Hata hivyo, alisisitiza kuwa kazi za ushauri wa kitaalamu na tafiti katika taasisi za elimu ya juu zinapaswa kujumuishwa katika mipango mkakati ya taasisi husika ili kuwepo na mifumo ya kupima na kutathmini utekelezaji wake.

    Akichangia mada katika mjadala wa siku ya kwanza ya mafunzo hayo, Dkt. Janeth Laurean kutoka Idara ya Uchumi na Maendeleo ya Uchumi wa Jamii chuoni hapo, alishauri kuwepo kwa utaratibu wa kuwatambua na kuwathamini wanataaluma watakaobuni miradi na tafiti zitakazoingizia chuo mapato, jambo litakalowahamasisha wengine kushiriki katika kazi hizo.

    Wakati mjadala huo ukiibua changamoto mbalimbali katika mfumo wa elimu na tafiti zinazofanyika bila kuzaa majibu ya moja kwa moja kwa jamii, ilibainika kuwa bado mtazamo wa baadhi ya wanafunzi na wasomi ni kuhitimu na kuvaa joho la mahafali, badala ya kuona elimu na tafiti kama nyenzo ya kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.

  • Chuo cha serikali za mitaa warejea na makombe saba (7) na medali za kutosha katika mashindano ya SHIMIVUTA 2025 yaliotamatika 22 Disemba, 2025 mkoani Tabora. Makombe hayo ni pamoja na kombe la mpira wa pete (mshindi wa kwanza) na kwa wanaume ( mshindi wa pili) kombe la mpira wa mikono kwa wanawake (mshindi wa tatu), kombe la kukimbia na gunia kwa wanaume (mshindi wa tatu), ‘pool table’ kwa wanawake (mshindi wa kwanza) na kombe la draft kwa wanawake (mshindi wa pili). (Picha zote na Farida Mkumba, Tabora).

  • Na Vincent Mpepo

    Watanzania wanaosafiri kuelekea maeneo mbalimbali nchini, hususan washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), wametakiwa kuwa waangalifu nyakati za mwisho wa mwaka kutokana na changamoto mbalimbali za usafiri.

    Wito huo umetolewa na Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa wa Kwembe, Emeline Mnzava, jana wakati wa ibada ya Siku ya Nne ya Majilio iliyofanyika katika mtaa huo. Alisisitiza umuhimu wa wanaosafiri kubeba nyaraka au cheti cha utambulisho kinachoonyesha wanakotoka ili kurahisisha upatikanaji wa msaada popote watakapokwenda.

    “Ni muhimu sana kuchukua cheti cha utambulisho wa safari kwa kuwa kitakusaidia kupata msaada wowote utakapohitajika,” alisema Mwinjilisti Mnzava.

    Aidha, aliwataka washarika wa mtaa huo kuendelea kuimba na kumtukuza Mungu hata pale ambapo vyombo vya muziki havifanyi kazi, akisisitiza kuwa Walutheri wana nyimbo zao zinazoweza kuimbwa bila kuhitaji vyombo vya muziki.

    Akihubiri katika ibada hiyo, Mtendakazi wa Mtaa huo, Anna Mauki, alizungumzia umuhimu wa jamii kuwajali wahitaji, hususan katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka ikiwemo Krismasi na Mwaka Mpya, kama sehemu ya kutekeleza maandiko kwa vitendo.

    Alisema maandiko yanahimiza matengenezo ya mioyo na kuhudumiana, na kwamba ili kuishi kulingana na neno la Mungu, kuna ulazima wa wanajamii ikiwemo Wakristo kuwakumbuka wahitaji kama vile wajane, yatima na watu wenye mahitaji maalumu.

    Anna alieleza kuwa matengenezo ya kiroho wakati wa Majilio yanapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya kimwili, ikiwemo kuwajali na kuwakumbuka wenye mahitaji katika jamii, akisisitiza kuanza katika familia na kwa majirani.

    “Hakuna asiyejua maana ya Noeli kutokana na maandalizi ya kimwili yanayofanyika kila mwaka,” alisema.

    Aliongeza kuwa pamoja na maandalizi hayo, sikukuu yoyote huwa na maana zaidi endapo watu wote wana afya njema. “Unaweza kuwa na kila kitu, lakini ukawekewa masharti ya kula au kutokula vitu fulani kutokana na afya,” alisisitiza.

    Pia aliwakumbusha Wakristo kufanya tathmini ya mahusiano yao na Mungu kwa kipindi cha mwaka mzima ili kubaini mwenendo wao katika masuala mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa ahadi na huduma katika nafasi walizonazo, iwe ni mtu binafsi au katika vikundi kama kwaya.

    “Kutotunza ahadi, ikiwemo kutofanya mazoezi, wakati mwingine kunatukosesha baraka,” alisema Mtendakazi Anna.

    Mwisho, aliwapongeza washarika wa mtaa huo, hususan wanawake, kwa mchango wao mkubwa katika utunzaji wa mazingira ya kanisa.

  • Na Mwandishi wetu, Nachingwea

    Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka ameahidi kuwalipia bodaboda zaidi 300 shilingi Elfu tano (5000) kwa Kila bodaboda atakayekwenda kununua kofia ngumu kwenye duka maalum alilolipendekeza.

    Akizungumza katika kikao kazi na bodaboda hao hivi karibuni, Mbunge Liwaka alisema kuwa ameamua kuwaunga mkono kwa kiasi hicho cha fedha kwa lengo kuwaondolea adha ya kukamatwa na polisi wa barabarani pamoja kujikinga na ajali za barabarani.

    “Napokea simu kutoka kwa bodaboda juu ya kukamatwa na polisi wa barabarani kwa kosa la kutokuwa na kofia ngumu hivyo kama Mbunge wenu nimeamua kuwachangia kiasi hicho ili kila mmoja wenu aweze kulimiki kofia ngumu yake”, alisema Mbunge Liwaka.

    Aidha aliliomba Jeshi la Polisi wilaya ya Nachingwea kuwapa muda mfupi ili kila bodaboda aweze kununua kofia ngumu kwa ofa aliyoitoa ya kuwachangia kiasi tajwa.

    Kwa upande wake, mmoja wa waendesha bodaboda Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Rashidi alimshukuru Mbunge kwa ahadi hiyo ya fedha ambayo itawawezesha bodaboda kupata kofia ngumu na  wapo tayari kumuunga mkono kwa kununua kofia hizo kama alivyo waelekeza.