• Sehemu ya wanakwaya wa USCF Mlimani CCT wakihudumu katika ibada ya kwanza katika anisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Mbezi Luis siku ya Jumapili, (Picha Vincent Mpepo).

    Na Vincent Mpepo

    Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam wameushukuru uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Luis kwa kuwapokea na kuwahudumia vizuri walipokua usharikani hapo kwa kambi Maalumu ya siku tatu.

    Shukrani hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kwaya ya USCF Mlimani CCT, Joshua Richard wakati wa ibada ya kwanza mbele ya washarika alipokuwa akitoa salamu za shukrani na kwamba wamefarijika kwa namna wa uongozi wa kanisa na vikundi mbalimbali walivyowakarimu.

    Alisema wametembelea sehemu nyingi kwa kambi lakini Usharika wa Mbezi Luis ni moja ya Sharika zilizowapokea na kuwakarimu vizuri kwani wameonja upendo na kujaliwa muda wote walipokuwa usharikani hapo.

    Alisema madhumuni ya kambi hiyo Maalumu ni kwa ajili ya maombi na masuala mbalimbli ya kiimani kwa vijana na kwamba ni utaratibu waliojiwekea kila mwaka wanafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kukulia kiimani kwani kanisani ndio mahali salama zaidi.

    “Vijana kujihusisha na masuala ya Mungu tunanakuwa salama zaidi kwani itatuepusha na mambo mengi yasiyofaa ikiwemo madawa ya kulevya”, alisema Richard

    Alisema vijana wakiandaliwa vyema kiroho familia, jamii na taifa kwa ujumla limepona kwa kuwa watajitambua na kuwa wanajamii wanatabua wajibu wao.

    Kambi hii ya maombi ilikuwa na vijana wa kike na wa kiume 132 tangu Ijumaa mpaka Jumapili, alisema Richard

    Mwalimu Gadielson Mfinanga katika mahubiri siku hiyo aliwakumbusha wakristo kutoruhusu changamoto wanozaopitia kubadili uhalisia wa Mungu katika maisha yao kwani kufanya hivyo kutawagharimu baada ya hali hiyo kuisha.

    Alisema Mungu ana tabia ya kuwabakiza watu ambao hata baada ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wataedelea kutembea nao katika nyakati za huzuni au furaha.

    “Ni muhimu sana kuwathamini wengine bila kuwahukumu au kuwadharau kwani huwezi kujua ni wakati gani watakufaa”, alisema Mwalimu Mfinanga.

    Alisema matokeo ya kila mmoja na alivyo ni mjumuisho wa namna wa watu aliokutana nao katika maisha yake.

    Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Mbezi Luis, Godlsiten Nkya aliwashukuru vijana wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwamba wanafanya kazi njema machoni pa Mungu.

    Aidha, aliwakumbusha wazazi wa Dar es salaam kujiuliza ikiwa vijana wao wanaosoma vyuoni hususani Chuo Kikuu cha Dar es salaam kama wanajishughulisha na masuala ya kiimani kwa kati ya vijana 132 walifika usharikani hapo hawakuzidi 10 kutoka Dar es salaam.

    “Ni wajibu wa wazazi kuwakumbusha vijana wao wasiende na maisha bila Mungu”, alisema Mchungaji Nkya.

    Alisema wakati vijana hao wakijishughulisha na kwaya na masuala ya kikanisa wapo wengine ambao wamejiingiza kwenye mambo yasiyofaa ikiwemo ulevi.

  • Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akihutubia wakati wa uzindizi wa programu tumizi ijulikanayo kama PFZ uliofanyika leo jijini Dar es salaam katika viwanja vya Soko Kuu la Kimataifa la Feri, (Picha na Vincent Mpepo).

    Na Vincent Mpepo

    Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imezindua programu tumizi ijulikanayo kama PFZ itakayorahisisha shughuli za uvuvi na kuwanufaisha wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa shughuli hizo ikiwemo wavuvi, wafanyabiashara, wachakataji, wachuuzi na wateja hivyo kuongeza tija itakayochochea ukuaji uchumi katika sekta ya uvuvi nchini.

    Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo Feri jijini Dar es salaam leo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede alisema programu tumizi hiyo itasaidia wavuvi kufanya shughuli zao kwa uhakika na kuondokana na uvuvi wa kubahatisha.

    “Uvuvi ni moja ya sekta ambayo inakuwa kwa kasi ikizingatiwa kuwa asilimia 75 ya mazao yake yanauzwa kwenye soko la Ulaya na imeendela kutoa mchango mkubwa kwenye lishe na chakula”, alisema Dkt. Mhede.

    Alisema baada ya kufanyiwa mjaribio mfumo umeonesha matokeo mazuri ya uhakika wa zaidi ya asilimia 75 kutambua aina ya samaki anaowahitaji kwa mahitaji ya soko, umbali walipo na hali ya hewa ili kuwa na uhakika wa usalama wao wakiwa baharini.

    “Mvuvi atajisajili bure na atatakiwa kuweka taarifa zake za msingi ikiwemo taarifa leseni ili atambuliwe na taasisi mbalimbali na kwamba taarifa zake zitalindwa kwa mujibu wa sheria”, alisema Dkt. Mhede.

    Alisema programu tumizi hiyo itarahisisha upatikanaji wa taarifa za wavuvi na utambuzi wao utasaidia kudhibiti uvuvi haramu na kutoa fursa kwa taasisi za fedha kuwakopesha wanawake, vijana na wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi.

    Alisema mfumo huo umefungamanishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hivyo kumhakikishia mvuvi kuwa na taarifa za hali ya hewa kitu kitakachomhakikishia usalama na namna bora ya kujilinda au kuepuka changamoto zitokanazo hali ya hewa hatarishi baharini.

    Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei alisema shughuli za utafiti zilianza Mwaka 2011 kupitia Mradi wa kutafuta maeneo ya uvuvi baharini kwa msaada na ushirikiano kutoka Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.

    Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alisema wavuvi watumie mfumo huo kwa kuwa ni wa serikali na kwamba anawapongeza watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari (ZAFIRI) kwa kazi hiyo nzuri.

    Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam, Helihuruma Mabelya alisema Soko Kuu la Kimataifa la Feri ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na kwamba kwa kuthamini mchango huo halmashairi itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa mindombinu ya msingi ili kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wateja.

  • Na Gabriel Alex Msumeno, Kibaha

    Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Phillip Mpango ameongoza wananchi na wakazi wa Mkoa wa Pwani katika sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa zilizofanyika Leo katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.

    Akizungumza wakati wa sherehe hizo Dkt.Mpango amewataka watanzania kutumia vizuri haki yao ya kidemokrasia kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika baadaye Oktoba 2025.

    “Kila mtanzania mwenye sifa atImize haki yake ya kikatiba KUmchangua kiongozi anayemtaka ili kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi yetu”, alisema Dkt Mpango.

    Aidha alibainishwa kuwa licha ya Mwenge wa Uhuru 2025 kuwa na kauli mbiu inayosema “Jitokeze kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu”, umebeba ujumbe kwa watanzania kuhusu masula mengine ikiwemo lishe bora kwa afya imara, mapambano dhidi ya rushwa, VVU/UKIMWI, dawa za kulevya na ugonjwa wa Malaria.

    Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbal wa chama na serikali wakiwemo Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Rais Mstaafu wa Tanzania wa awamu ya nne Dkt.Jakaya Kikwete, Naibu Spika wa Bunge la Jumhuri ya Tanzania, wakuu wa taasisi za umma, vyombo vya ulinzi na usalama, watumishi wa serikali na taasisi binafsi, wasanii na wananchi kwa ujumla.

    Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Mikoa 31 kwa muda wa siku 195 ukizindua miradi mbalimbali na katika Mkoa wa Pwani utazindua jumla ya miradi 64 yenye thamani ya shilingi Trilioni1.2.

  • Na Vincent Mpepo, Kwembe

    Jamii imetakiwa kuwakumbuka wahitaji na wenye mahitaji maalumu katika huduma mbalimbali ikiwemo mavazi, chakula na mahitaji mengine ya msingi ili waendelee kuishi vyema kimwili na kiroho kama sehemu ya wanajamii.

    Wito huo umetolewa Jumapili na Mwalimu Israel Mmari katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe wakati akihamasisha uchangiaji wa sadaka maalumu ya udiakonia kwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kipya kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu kinachotarajiwa kuhamishiwa Kitopeni Bagamoyo kutoka Kijichi jijini Dar es salaam kutokana na mahali kilipo sasa kuwa siyo salama.

    Alisema bado kuna namna ambapo kila mtu kwa nafasi yake au familia au mashirika iwe ya umma na binfasi yanatakiwa kuwakumbuka wahitaji kwa namna moja au nyingine ili kuwasadia katika kuhakikisha mahitaji yao ya msingi yanapatikana.

    “Kuna mahali ambapo maombi peke yake hayasaidii ni lazima ufanye kitu cha ziada ikiwemo sadaka na matendo ya huruma”, alisema Mwalimu Mmari.

    Alibainisha wahitaji wengine ambao wanahitaji misaada mbalimbali ya kibinadamu katika jamii kuwa ni pamoja na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, wajane, wafungwa na wagonjwa.

    Aidha aliitahadharisha jamii dhidi ya matumizi mabaya ya mitanadao ya kijamii na kwamba wapo ambao huitumia vibaya kuharibu wasifu na sifa za wengine.

    “Wapo watu ambao hugharimia mambo yanayowaumiza wengine kupitia mitandao ya kijamii”, alisema Mwalimu Mmari.

    Aidha aliwakumbusha wazazi na walezi kujuenga mazingira mazuri na wezeshi kwa watoto wao ili wakue katika namna njema badala ya mazingira ambayo yatakuwa magumu kwao.

    Mwalimu wa Shule ya Jumaipili, Thomas Lukindo akifundisha watoto kama alivyoonekana na mpiga picha wetu Siku ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

    Uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebaini kuwa matendo ya huruma kwa wanajamii huwa yanafanyika nyakati za mifungo ya kiimani mfano Kwaresma kwa wakristo na Mwezi Mtukufu wa Ramadani kwa waislamu wakati kiuhalisia mahitaji kwa watu wa Makundi Maalumu yapo muda wote.

    Mwandishi anadhani ifike  mahali jamii ione kuwa mahitaji kwa wahitaji ni sehemu ya maisha ya kila siku na siyo siku za mifungo au msimu tu hivyo jamii ibadilike na kuwathamini wahitaji nyakati zote na ikibidi wafanye kwa kudhamiria kutoka ndani siyo kwa maonesho na kujitangaza kama inavyofanyika sasa.

    Mwalimu Joyce Kamugisha wa shule ya Jumapili akifundisha watoto katika ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

  • Sehemu ya wanafunzi na walimu kutoka Norway wakifurahia zawadi kutoka Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii zilizotolewa leo katika hafla fupi ya kuwaaga katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania leo jijini Dar es salaam, (Picha na Vincent Mpepo,OUT).

    Na Vincent Mpepo, OUT

    Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeelezea kuridhishwa kwake na huduma za walimu na wanafunzi kutoka Norway ambao walikuwa nchini katika mafunzo kwa vitendo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya ushirikiano kati ya chuo hicho na vyuo vikuu kutoka nchini Norway.

    Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii ya Chuo hicho, Dkt.Mariana Makuu wakati wa hafla fupi ya kuwaaga walimu na wanafunzi iliyofanyika leo katika ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es salaam na kuhudhiriwa na wanataaluma na wanafunzi wa pande zote mbili.

    Alisema idara yake imepokea mrejesho chanya kutoka shule ambako wanafunzi na walimu hao walikuwa wanafanya mafunzo kwa vitendo na kwamba wameelezea kuridhishwa na huduma zilizofanyika kwa ajili ya walimu na watoto.

    “Walimu wametoa shukrani kwa ujuzi na maarifa mliyoyatoa ya namna ya kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu”, alisema Dkt.Mariana.

    Aidha alisema ushirikiano uliooneshwa na wanafunzi na wasimamizi wao umerahisisha kazi ya utekelezaji na tathimini ya kazi hiyo.

    Akizungumza kwa niaba ya walimu kutoka Norway, Mwalimu Anne Gutteberg alisema kwa muda aliokaa Tanzania amepata uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo utofatui wa kiutamaduni kati ya Norway na Tanzania.

    “Imekuwa fursa nzuri kwa wanafunzi kutoka Norway kujifunza kwa vitendo na kubadilisha uzoefu,” alisema Mwalimu Anne.

    Akitoa shukrani kwa niaba ya idara, Mkufunzi Msadizi, Fauzia Kitenge alisema washiriki kutoka Norway wamefanya kazi nzuri kwa juhudi na maarifa kitu ambacho kimeleta matokeo mazuri kupitia kazi zao.

    Mkufunzi Msadizi, Idara ya Sosolojia na Ustawi wa Jamii ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Fauzia Kitenge akitoa neno la shukrani kwa wageni kutoka Norway,kushoto ni Mkuu wa Idara hiyo, Dkt.Mariana Makuu. (Picha na Vincent Mpepo).

    Naye Mwanafunzi kutoka Norway, Ina Fagerdal aliwashukuru wenyeji wao ambao ni idara ya sosholojia na ustawi wa jamii kwa ukarimu na msaada wao wa karibu katika muda wote waliokuwa hapa nchini.

    Mwanafunzi Ina Fagerdal kutoka Norway akielezea uzoefu wake katika mafunzo kwa vitendo alipokwa hapa nchini, (Picha na Vincent Mpepo).

  • Na Tabia Mchakama

    Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki na kudhamini tuzo katika Mkutano wa Wadau wa elimu ulioandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Sinyamule uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii jijini Dodoma.

    Katika Mkutano huo, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware aliitaka jamii kukata bima kutokana na manufaa yake katika ulinzi wa afya zao, mali zao na za mali za serikali.

    “Bima ni sehemu ya kujiongezea kipato kwa kuwa wakala wa bima”, alisema Kamishna Dkt. Saqware.

    Mgeni Rasmi wa Mkutano huo alikuwa Dkt. Doto Biteko ambaye kutokana na majukumu mengine aliwakilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Sinyamule.

    Mkutano huo uaneda sanjali na utekelezaji wa kauli mbiu isemayo ‘Uwajibikaji Wangu ni Msingi wa Kuinua Ubora wa Elimu na Ufaulu Dodoma’ na ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu zaidi ya 2,000.

    Waliotunukiwa tuzo hizo ni walimu, wanafunzi, shule na Wilaya, zilizofanya vizuri katika mitihani ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha Sita kwa mwaka 2024 katika Mkoa wa Dodoma.

    Tuzo hizo zinatajwa kuwa chachu na hamasa kwa waliofanya vizuri na inatarajiwa kuwa chachu kwa wengine kuongeza bidii katika mitihani ijayo hivyo kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kiwilaya, kimkoa na kitaifa.

  • Hawa Mikidadi, Morogoro

    Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, Nuru Ngereja amewaomba waandishi wa habari kuendeleza ushirikiano na chama chake ili kuwatumikia wananchi katika utekelezaji wa ilani ya chama.

    Kauli hiyo aliitoa Tarehe 24.03.2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha na kuwatambua waandishi wa habari wa mkoa huo.

    “Katika kipindi ambacho nitakuwepo hapa ninaamini tutafanya kazi pamoja”, alisema Ngereja.

    Alisema kupitia kalamu zao wana kila sababu ya kushirikiana na chama ili kufanikisha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya wana Morogoro.

  • Mwalimu Israel Mmari wa KKKT Usharika wa Mji Mpya akihubiri jana katika Ibada katika Mtaa wa Kwembe (Picha na Vincent Mpepo).

    Na Vincent Mpepo, Kwembe

    Wakristo wametakiwa kuombea akili kwa kuwa ndiyo inayowezesha watu kufanya maamuzi katika masuala mbambali  iwe katika ngazi ya mtu binafsi, ngazi za familia, jamii na taifa kujiepusha na majanga au matokeo ya matumizi mabaya ya akili ambayo mara nyingi huwaingiza watu kwenye majuto na shida.

    Wito huo umetolewa leo na Mwalimu Israel Mmari wa Kanisa la Kiinjili la Kiutheri (KKKT) Usharika wa Mji Mpya jijini Dar es salaam wakati akihubiri katika Mtaa Kwembe na kwamba siyo kila matatizo dawa yake ni maombi au kufunga.

    Alisema zipo changamoto ambazo kimsingi zimetokana na matumizi mabaya ya akili na kutotambua majira na nyakati hivyo wakati mwingine kuaomba na kufunga ni kujitesa kwa kuwa shida imeanzia kwenye akili iliyofanya maamuzi mabaya.

    Alisema kila kitu katika maisha kimefungwa na nyakati na nyakati ni kibebeo cha mafanikio ambayo Mungu huachilia katika mafanikio ya mwanadamu hivyo busara, hekima na akili sahihi husaidia kufanya maamuzi sahihi kwa wakati husika ili kuwa na matokeo chanya.

     “Kuna majira na nyakati kwa ajili ya kujiliwa kwako na hata kama hukufanya maandalizi Mungu huachilia baraka zake sasa inategemea akili yako imetambuaje na kutumia vyema baraka hizo kwa nyakati hizo”, alisema Mwalimu Mmari.

     “Kabla ya mabaya Mungu huwa na tabia ya kutanguiza mema sasa akili na hekima zinaweza kuamua vyema kwa ajili ya baadaye lakini akili isiyoweza kuamua vyema huleta majanga”, alisema Mwalimu Mmari.

    Akitolea mifano ya ushoga, usagaji na wanaume wanaoishi na wanawake waliowazidi umri kwa kigezo cha kulelewa kuwa hayo yote ni matumizi mabaya ya akili na kwamba wanaotenda hayo wamefikia mwisho wa namna za kutumia akili zao.

    “Hata baadhi ya matatizo katika taasisi za umma, binafsi na kwa watu binafsi wakati mwingine yanatokana na uzembe wa baadhi ya waliopewa dhamana kutotumia akili ipasavyo katika maamuzi fulani”, alisema Mwalimu Mmari.

    Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Exaud Mchome aliwajulisha washarika wa Mtaa huo hatua ya ujenzi wa kanisa ambapo imefikia kwenye kuezeka na kwamba tayari kamati yake imeshalipia mabati kwa ajili ya jengo hilo.

    Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Exaud Mchombe akifafanua jambo wakati akizungumza na washarika wa KKKT Mtaa wa Kwembe Jana (Picha na Vincent Mpepo)

    Alisema kila mmoja anatakiwa kuwa sehemu ya historia katika ujenzi wa jengo hilo na aone fahari kwa jambo hilo la kumjengea Mungu mahali pa kuabudia. 

    Aidha, aliwakumbusha viongozi mbalimbali katika mtaa huo kuendelea kuwa mfano kwa washarika ili kuongoza vyema katika masuala mbalimbali ikiwemo uchangiaji katika ujenzi na kwamba kiongozi mzuri ni yule anayeongoza kwa mfano na matendo yake.

    “Kimsingi hakuna masikini anayeweza kukiri kuwa hana cha kumtolea Mungu kwa kuwa wema wake bado ni ushahidi kuwa bado tunapaswa kumrudishia yeye hata kwa kidogo alichotujaalia”, alisema Mchome.

    Katika hatua nyingine, wawakilishi wa watoto wa shule ya Jumapili katika ibada hiyo huku masuala mbalimbali yakiwekwa mikononi mwa Mungu ikiwemo amani na usalama wa nchi hususani wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu, waliwaombea viongozi mbalimbalimbali wa dini na wa kisiasa ili waongoze kwa hekma za kimungu.

    Wawakilishi wa watoto wa Shule ya Jumapili ambao walifanya maombi kwa niaba ya wenzao jana katika Mtaa wa Kwembe, nyuma yao ni Mwinjilisti Kiongozi wa KKKT Mtaani hapo, Emeline Mzava. (Picha na Vincent Mpepo).

    Maombi mengine yalielekezwa kwenye mamlaka mbalimbali zinazohusika na utoaji wa haki ikiwemo mahakama na magereza, ustawi wa familia na mtoto, umoja wa makanisa na Uchumi wa nchi.

    Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwakumbusha washarika wa Mtaa huo kuwa mawakili wema katika utoaji wa sadaka ya mfuko wa elimu na kwamba ikiwa kila mmoja atakuwa mwaminifu katika sadaka hiyo itasadia sekta ya elimu.

    Kwaya ya akinababa ya KKKT Mtaa wa Kwembe ikihudumu katika ibada ya Jumapili. (Picha na Vincent Mpepo).

  • Na Cartace Ngajiro, Tanga

    Menejimenti ya Bandari ya Tanga imewahakikishia wadau wa bandari hiyo kuendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kibandari ikiwa ni pamoja na utoaji huduma bora kwa wateja ili kuongeza tija na ufanisi.

    Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga Bw. Peter Millanzi hivi karibuni wakati akifunga kikao cha maboresho ya Bandari ya Tanga ‘Tanga Port Improvement Committee’ kilichofanyika jijini Tanga katika ukumbi wa mikutano ulipo katika jengo la Bandari House.

    “Ushirikiano uliopo uendelee kuwepo kwani ndio chachu ya mafanikio katika bandari hiyo kiufanisi”, alisema Millanzi.

    Aidha aliwaahidi wadau hao kufanyia kazi na kupatikana kwa ufumbuzi kwa changamoto zilizopo ili kuendelea  kuvutia wateja zaidi kutumia bandari hiyo.