Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akipata maelezo juu ya Chuo cha Serikali za Mitaa alipotembelea banda la chuo hicho wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na taasisi inayojihusisha na maboresho ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) yanayoendelea katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma uliopo Mji wa Kiserikali Mtumba yaliyoanza Tarehe 14 hadi 16 Aprili, 2025.
Kauli mbiu katika mafunzo hayo ni “Ugatuzi wa rasilimali fedha katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa”(Picha na Farida Mkumba).
Watu wenye mahitaji maalumu ni kundi la watu ambao hawawezi kujipatia mahitaji yao ya msingi wao wenyewe kutokana na changamoto kadha wa kadha.
Changamoto hizo husababishwa na vitu mbalimbali kama vile ulemavu wa kimwili, kihisia, kitabia, au kujifunza au kuharibika ambazo husababisha mtu kuhitaji huduma za ziada au maalum au malazi kama vile elimu au burudani.
Ili kundi hili lipate mahitaji huduma za msingi kama walivyo binadamu wengine ni lazima jamii ihusike kwa namna moja au nyingine ili kuhakikisha kuwa jukumu hili linatekelezwa.
Utekekezaji wake huhusisha serikali, jamii, makundi mbalimbali, taasisi za dini, mashirika na taasisi za umma na binafsi.
Ushirikiano wa taasisi mbalimbali unasaidia kuwa na nguvu ya pamoja ili kuhakikisha kundi hili muhimu linapata stahiki na haki za kibinadamu ili kuwa na jamii yenye ustawi bora, isiyo na wanaoachwa au kutengwa kwa namna yoyote.
Ushirikiano huu unawaleta pamoja wadau mbalimbali kwa namna ya uwezo na aina ya huduma wanazotoa ili kwa pamoja kuwa na uwezeshaji wa hali na mali katika ngazi mbalimbali. Kwa mfano taasisi za elimu kama Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kina idara maalumu inayohusika na watu wenye mahitaji maalumu.
Sanjali na kitengo hicho, idara ya sosholojia na ustawi wa jamii nayo imekuwa ikifanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna bora za kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.
Idara hiyo, imekuwa na makubaliano na taasisi za ndani na nje ya nchi ili kupata msaada wa kitaaluma wa namna ya kuongeza wigo wa maarifa kuhusu elimu ya watu wenye mahitaji Maalumu ikigusa eneo la ualimu wa elimu Maalumu na ufundishaji.
Idara hiyo kupitia ushirikiano na vyuo vikuu vya nje ikiwemo Norway kupitia Mradi wa Norec ambao umesaidia masuala mbalimbali ikiwemo programu za kubadilishana uzoefu zinazowahuhisha wahadhiri, wanafunzi, maofisa maendeleo ya jamii na wadau mbalimbali wa maswala ya ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa Daktari Mariana Makuu, mtoto mwenye mahitaji maalum awapo shuleni anatakiwa kulelewa vyema ili apate huduma tatu muhimu ikiwemo elimu, afya na msaada wa kisaikolojia na kijamii.
“Kundi la watoto wenye mahitaji maalumu linakabiliwa na ukatili wa aina mbalimbali unaosababisha watoto hawa kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia”, anasema Dkt.Mariana.
Uwepo wa wataaam wa ustawi wa jamii shuleni wenye jukumu la kuangalia masuala ya kijamii kwa watoto hawa wakisaidiana na walimu utasidia kuibua na kuzuia ukatili na matatizo mengine yanayowakabili watoto hususani wenye ulemavu.
“Serikali ione umuhimu wa kuaajiri wataalam hawa ili kuendana na mabadiliko ya jamii kwa sasa,” anasema Dkt. Makuu.
Wakati huohuo, ushirikiano wa serikali na taasisi za dini nao una nafasi nzuri kuhaikisha jamii na husani ya wenye mahitaji maalumu wanajaliwa ili kuwa na jamii inayojali watu wote bila kujali ulemavu wa aina yoyote.
Hivi karibuni tumeshuhudia mazungumzo kati ya kiongozi mkuu wa nchi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ulioongozwa na Mkuu kanisa na Mkuu wa Dayosisi hiyo Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa Ikulu jijini, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Samia pamoja na viongozi hao walijadili kuhusu utoaji wa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum hususan wenye changamoto ya afya ya akili.
Viongozi kanisa wameipongeza na kuishukuru serikali kwa ushirikiano inaotoa kwa kanisa kwani serikali imeahidi kushirikiana na kanisa ili kujenga Kituo kikubwa zaidi kitakachohudumia watoto wenye changamoto ya afya ya akili ili watoto wengi waweze kupata huduma hiyo.
Wakati serikali, taasisi za umma na binafsi za ndani na nje zikifanya kila linalowezekana kusaidia kundi la watu wenye mahitaji Maalumu swali ni kwa jamii tunafanya nini kuunga mkono kwa sehemu yetu?
Ni dhahiri kuwa bado elimu inahitajika ili masuala ya watu wenye mahitaji Maalumu yapate wigo mpana wa kuelezwa kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari, mikutano mbalimbali na kila ambapo fursa ya kufanya hivyo itajitokeza.
Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametakiwa kuendelea kumtolea Mungu sadaka bila kukata tamaa huku wakiziombea ili zifanye kazi yake na pia wapate baraka kupitia sadaka hizo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Ujenzi wa Madarasa ya Watoto na Ofisi za Usharika wa Betheli Dayosisi ya Dodoma, Makao Makuu Lilian Uroki wakati akihamasisha utoaji wa sadaka hiyo katika ibada ya kwanza usharikani hapo Jumapili.
Alisema washarika wenyeji na wageni wanapaswa kufanyia kazi suala hilo na kwamba hawapaswi kuiita michango bali ni sadaka.
“Ni muhimu sana kuhakikisha kabla ya kutoa unaziombea ili Mungu afanye kitu kwa ajili yako”, alisema Lilian
Mhubiri wa Siku hiyo, ambaye ni Katibu wa Usharika huo, Dkt.Denis Ringo aliwaasa wakristo kutokujisahau kwa kuwanyenyekea watumishi badala ya Mungu aliyewatuma na kwamba wanatumika ili kusudi la Mungu litimie.
“Ni hatari kumwamini aliueagizwa badala ya aliyemuagiza”, alisema Dkt.Ringo
Alisema kuna wakati wakristo hujisahau hususani wanapopata kitu iwe ni baraka ya kichumi, kupanda cheo au manufaa fulani badala ya kumtumikia Mungu hurudi nyuma kwa sababu mbalimbali ikwemo madai ya kukosa muda wa kufanya zake na matokeo yake huwa ni kusahaulika.
“Ni mara ngapi tunatumika kwa Bwana kwa nafasi zetu, vyeo vetu au hali njema tulizonazo?” Aliuliza Dkt.Ringo
Alisema Mungu hutumia watu au vitu vya kawaida au vinyonge ili kusudi lake litimie badala ya watu wenye mamlaka au umaarufu ambao wakati mwingine hutumia nafasi zao ili tu wapate sifa na kusahau kuwa Mungu ndiye aliyewapa nafasi hizo.
Alisema mkristo anapoitwa kutumika na ikiwa atatumika sawasawa na kusudi la Mungu atainuliwa na kuheshimishwa.
Alisema wakristo wanapopitia katika nyakati ngumu busara, hekima, unyenyekevu na upole vitaendelea kuwa ndiyo silaha nzuri na kwamba Mungu anajua kesho yao hivyo waendelee kumtegemea yeye na wasiondoke katika kusudi la Mungu.
Mchungaji kiongozi wa Usharika huo, Gershon Ngewe aliwashukuru washarika kwa sadaka mbalimbali ambazo wanaendelea kuzitoa na kuwaombea kwa Mungu ili afanyike Baraka kupitia sadaka hizo.
Sehemu ya wadahiliwa wapya waliohudhuria mafunzo elekezi katika Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Mkoa wa Arusha Leo, (Picha na Amos Majaliwa).
Na Vincent Mpepo, Dodoma
Wanafunzi wapya wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania waliodahiliwa katika shahada ya awali ya Mawasiliano ya Umma wameelezea matarajio yao katika muda watakaokuwa masomoni na kuainisha sababu za kukichagua chuo hicho.
Wakizungumza katika nyakati tofauti kupitia mahojiano ya kimtandao hawakusita kuelezea hisia zao.
Upendo Sumary wa kituo cha chuo hicho Mkoa wa Ruvuma ambaye ni mdahiliwa wa shahada ya mawasiliano ya umma alisema aliamua kusoma katika chuo hicho kwa kuwa ni chuo cha umma kinachotambulika kitaifa na kimataifa na kwamba anaamini kupitia chuo hicho atafikia ndoto zake.
“Nimependa kusoma OUT kwa kuwa ni chuo chenye sifa nzuri ya ufundishaji na ninaamini kufanikisha ndoto zangu”, alisema Upendo.
Alisema anategemea kufanya vyema katika masomo yake kwani atajitahidi kufuatilia masomo kwa kadiri ya uwezo wake na atakuwa makini ili afanikishe malengo yake.
Esther Nurben wa Dar es salaam ambaye ni mdahiliwa wa shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa umma alisema alifikia uamuzi wa kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutokana na sifa za kuaminika kwa kutoa wahitimu mahiri kwenye kwenye fani mbalimbali siyo tasnia ya habari pekee.
“Ni mategemeo yangu kuwa nitahitimu shahada yangu kwa muda muafaka bila ya changamoto zozote”, alisema Ester.
Alisema sababu nyingine muhimu ambayo ilimvutia kusoma chuo hicho ni fursa ya kuendelea na masomo huku anafanya kazi na unafuu wa ada.
Anjela Mhilu wa Kituo cha Mkoa cha Ilala alisema aliamua kusoma katika chuo hicho ili kujiongezea maarifa na ujuzi kwenye programu aliyoomba na ni katika harakati za kujiongeza na kutafuta zaidi.
Kwa upande wake, Abishagi Mpoki alisema uwezekano wa kufanyia mitihani mahali popote atakapokuwa hata akiwa na majukumu ya kikazi nje ya kituo chake cha kazi ndiyo sababu iliyomvutia kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
“Elimu bora na kuniwezesha kusoma huku nafanya kazi ni kitu kilichonifanya nikichague chuo hiki”, alisema Abishagi.
Mwandishi amebaini kuwa taarifa za matangazo ya chuo hicho zinaufikia umma kupitia matangazo kwa njia za mitandao ya kijamii, wanafunzi wanaoendelea na masomo na kupitia wahitimu wa chuo hicho ambao ni wafanyakazi katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Ni ukweli usiopingika kuwa chuo hicho kina deni na wajibu wa kutimiza ili kuendana na matarajio ya wadahiliwa hao kwa kuboresha huduma zake ikiwemo huduma ya mtanado ambayo ndiyo uti wa mgongo wa elimu masafa, uboreshaji wa mifumo ya Tehama na huduma kwa wateja.
Ujumbe wa watu 12 kutoka Eswatini ukiongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Nchi hiyo Madala Mhlanga umezuru ofisi ndogo za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dar es salaam kwa lengo la kupata uzoefu wa masuala mbambali ya kibima ikiwemo usimamizi wa soko na maswala ya kisheria.
Akiongoza kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania, Mkurugenzi wa Usimamizi kutoka TIRA, Christopher Mapunda aliwapitisha wageni hao katika mada mbalimbali ikiwemo hali ya soko la bima nchini, usimamizi wa soko la bima, sheria zinazotumika kusimamia soko la bima, mamlaka ya kamishna kwenye kusimamia soko la bima na mifumo ya tehama.
Aidha mjadala ulijikita kwenye kwenye vipaumbele mbalimbali vya mamlaka vikiwemo utekelezwaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI) na Uanzishwaji wa konsotia ya bima ya kilimo (TAIC).
Awali Naibu Spika wa Nchi hiyo Madala alieleza kuwa wapo katika mchakato wa uboreshaji wa sheria ya nchini humo na hivyo wamechagua Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri katika masuala ya bima ili kujifunza.
“Zaidi tunaishukuru TIRA kwa elimu na uzoefu mliotupatia na tunahaidi kuendeleza ushirikiano kwa siku zijazo”, alisema Naibu Spika Madala.
Baadhi ya wageni hao ni viongozi katika bunge la nchi hiyo, wizara ya fedha na mamlaka ya masuala ya huduma za fedha zisizo za kibenki ambapo waliungana na wataalamu wengine kutoka TIRA ili kubadilishana na kupeana uzoefu wa namna ya usimamizi na udhibiti katika soko la bima kwa pande zote mbili.
Utendaji mzuri wa kazi hupimwa kwa matokeo yanayopatikana, na ili matokeo yaonekane lazima kuwepo na waangalizi, wasimamizi na wafuatiliaji wa utekelezaji kutokana na kile walichokiona kwa macho na sio kusikia na kuangalia katika makaratsi.
Moja ya vipimo hivyo vinaweza kuonekana kupitia thamani ya fedha iliyo tumika kwa kulinganisha na uhalisia wa kazi yenyewe.
Katika masuala ya ujenzi wa miradi ya maji na kufikisha huduma ya maji kwa wananchi, Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan akamtwika dhamana Waziri wa Maji Jumaa Aweso (Mb) ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani, mkoani Tanga kuiongoza wizara hii inayogusa maisha ya wananachi moja kwa moja ili kuhakikisha azma ya serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini na mjini inatimia bila kikwazo.
Katika kufanikisha hilo Wizara ya Maji inatumia taasisi zake ambazo ni Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa maeneo ya mijini, Wakala wa Usambazaji Maji Vijijini (RUWASA), Mfuko wa Taifa wa Maji, Pamoja na Chuo cha Maji ili kufanikisha huduma ya upatikanaji wa maji kwa maeneo ya vijijini kufika asilimia 85 na mijini asilimia 95 ifikapo mwezi Disemba 2025.
Matokeo mazuri katika Sekta ya Maji kumechagizwa na usimamizi mzuri unaoitofautisha sekta hiyo ilipotoka na inapoelekea kupitia Kamati ya Kudumu ya Maji na Mazingira inayoongozwa na nahodha wake Mwenyekiti Jackson Kiswaga (Mb) ambaye ndiye mwakilishi wa wakazi wa Kalenga katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kamati hiyo inaundwa na jumla ya wajumbe 21 kutoka Bungeni.
Moja ya kazi kubwa ya kamati hii ni ukaguzi wa miradi ya maji ili kujionea utekelezaji wake katika maeneo mbalimbali nchini ikilinganisha na bajeti ya mwaka wafedha husika, kiasi kilichotengwa na kutumika, kushauri na kuweka msukumo katika masuala yanayohusu maji safi na usafi wa mazingira.
Kwa kipindi hiki kamati imetembelea miradi ya maji katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi ili kujionea utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika mkoa wa Tabora pamoja na sifa ya kuzalisha asali kwa wingi kwa upande wa suala la maji mkoa upo vizuri. Miradi iliyotekelezwa na kutoa huduma ya maji kwa wananchi na ile inayoendelea na utekelezaji wake ikiwemo Bwawa la Uyui ambapo kamati ilipata fursa ya kufanya ukaguzi.
Bwawa hilo linajengwa kwa fedha za ndani na kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni nne na lina uwezo wa kuhifadhi maji kwa mwaka lita za ujazo bilioni 5.1 na likinufaisha zaidi ya wananchi elfu 90 na hivi sasa utekelezaji wa ujenzi wa bwawa hilo umefika asilimia 60 na kukamilika kwa bwawa hili kutaongeza hali ya upatikani wa maji katika mkoa wa Tabora.
Umbali wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine katika kukagua utekelezaji wa miradi ya maji hilo halikuwa kikwazo kwa wajumbe wa Kamati ya Maji na Mazingira, na safari iliendelea hadi mwisho wa reli mkoani Kigoma. Safari hii ilikuwa mahususi kufika kukagua ujenzi wa mradi wa maji Munanila-Nyakimue Wilayani Buhigwe, mradi ambao utanufaisha vijiji nane.
Hadi sasa, katika mradi huu kazi zilizofanyika ni pamoja na ununuzi na ulazaji wa bomba, ujenzi wa nyumba tatu za mitambo ya kusukuma maji na ujenzi wa vituo vya umma vinne vya kuchotea maji.
Hadi sasa mradi umefikia asilimia 67 huku fedha zilizoleta mabadiliko hayo ni za ndani kiasi cha Shilingi bilioni 14.9 na jambo la kutia moyo ni kuwa hadi kufikia Oktoba 2025 mradi huu unatarajiwa kuwa umekamilika.
Aidha, kutokana na Kamati ya Maji na Mazingira kuona jiografia ya mkoa wa Kigoma ilipendekeza umuhimu wa kutumia chanzo cha ziwa Tanganyika kuwa chanzo cha uhakika cha maji kwa mkoa huo na mikoa jirani ikiwamo Katavi.
Hivyo, Wajumbe wa kamati hiyo katika kuhakikisha huduma ya maji inafika kwa wananchi walipita pori la Kigoma kwenda Katavi kwa umbali wa kilomita 249 bila kukata tamaa, kwa mvua au jua.
Wajumbe wa kamati walipata wasaa wa kuona kazi inayofanyika eneo la ujenzi wa mabwawa ya kutibu majitaka katika manispaa ya Mpanda. Maji safi yanapotumika kiasi kikubwa kinachobaki ni majitaka, huo ndio ukweli. Hivyo miundombinu ya majitaka nayo ni muhimu.
Wataalam wamasuala ya huduma ya maji wanasema kuwa asilimia 80 ya majisafi hubadilika na kuwa majitaka hivyo kutokuwepo kwa miundombinu ya uchakataji majitaka kutaleta athari za kimazingira ambazo ni hatari kwa binadamu na viumbe wengine.
Uchafunzi wa mazingira kutokana na majitaka unaweza kuwa ni chanzo cha kuharibu mazigira wezeshi kwa viumbe hai ikiwemo binadamu. Inaweza kuwa ni chanzo cha magonwa ya mlipuko kama kipindipindu.
Mabwawa yaliyokaguliwa yana uwezo wa kupokea lita za ujazo 600,000 kwa siku na kutokana na mchakato wake, taka hizo zinaweza kuzalisha mbolea itakayoweza kutumika katika shughuli za kilimo. Thamani ya mradi ni kiasi cha Shilingi bilioni 1.197
Mradi wa majitaka katika manispaa ya Mpanda umejikita katika matumizi ya magari na lengo la serikali ni kujenga mtandao ya majitaka moja kwa moja kutoka katika makazi ya wananchi kuelekea kwenye mabwawa hayo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeridhishwa na miradi ya maji katika mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora imetoa pongezi kwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb) na wataalam wa Sekta ya Maji nchini kwa kazi ya kuwafikishia wananchi huduma ya maji safi na salama.
Juhudi hizo zinakwenda sanjali na adhma ya serikali ya kuwafikishia wananchi huduma hiyo muhimu kufikia asilimia 85 vijijini na 95 mjini ikiambana na na kauli mbiu inayotambulika kama “Kumtua mama ndoo ya maji kichwani” inatimia.
Msisitizo umetolewa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji nchini ni kujenga utamaduni wa kulinda na kutunza miundombinu na vyanzo vya maji na kila mwananchi aone ana wajibu wa kufanya hivyo faida ya kizazi cha sasa na badae.
Utamaduni wa kulinda na kuhifadhi vyanzo na miundombinu ya maji utasaidia kuepuka athari hasi za mabadiliko ya tabia nchi yatakayosababisha ukame na changamoto ya nyingine za kimazingira. Ni wazi kuwa kila mmoja anakiri kuwa ‘maji ndio uhai wetu’ kwa kuangalia umuhimu wake katika maisha yetu na viumbe hai wengine.
Watanzania wametakiwa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
Wito huo umetolewa na Mkimbiza Mwenge Kitaifa, Ismail Ali Ussi akiwa katika Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani ambako anaendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru.
“Kila mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 anapaswa kushiriki uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025”, alisema Ussi.
Mwenge wa Uhuru umezindua miradi 5 na kuweka jiwe la Msingi kwenye mradi mmoja na kufanya jumla ya miradi iliyotembelewa katika Wilaya ya Kibaha ikiwa na thamani ya zaidi yaTsh Milioni 748.
Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 inasema “Jitokeze kushiriki uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa amani na utulivu”.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi akipanda mti kama ishara ya kutunza mazingira na uboreshaji wa nishati ya jua katika Hospital ya Mchukwi.
Na Gabriel Msumeno, Pwani
Mwenge wa uhuru umezindua miradi sita ya maendeleo katika sekta za elimu na afya Wilayani Kibiti Mkoani Pwani yenye thamani ya shilingi milioni 600.
Akizindua miradi hiyo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi aliwataka wananchi kuitunza ili iwe na manufaa kwa kizazi cha sasa na cha vizazi vijavyo ili kuboresha maisha.
Miradi iliyozinduliwa ni ya ujenzi wa matundu sita ya vyoo na vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Kibiti.
Miradi mingine ni pamoja na uzinduzi wa mashine mbili za kisasa za kubangulia korosho katika chama cha vijana cha Kibiti Cashernuts, uzinduzi wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Kibiti na mradi wa maji katika kata ya Bungu.
Aidha, Kionbgozi wa Mbio za Mwenge Kitafia alishiriki upandaji mti ikiwa ni ishara ya kutunza mazingira na uboreshaji wa nishati ya jua katika Hospital ya Mchukwi.
Sehemu ya wanakwaya wa USCF Mlimani CCT wakihudumu katika ibada ya kwanza katika anisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Mbezi Luis siku ya Jumapili, (Picha Vincent Mpepo).
Na Vincent Mpepo
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam wameushukuru uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Luis kwa kuwapokea na kuwahudumia vizuri walipokua usharikani hapo kwa kambi Maalumu ya siku tatu.
Shukrani hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kwaya ya USCF Mlimani CCT, Joshua Richard wakati wa ibada ya kwanza mbele ya washarika alipokuwa akitoa salamu za shukrani na kwamba wamefarijika kwa namna wa uongozi wa kanisa na vikundi mbalimbali walivyowakarimu.
Alisema wametembelea sehemu nyingi kwa kambi lakini Usharika wa Mbezi Luis ni moja ya Sharika zilizowapokea na kuwakarimu vizuri kwani wameonja upendo na kujaliwa muda wote walipokuwa usharikani hapo.
Alisema madhumuni ya kambi hiyo Maalumu ni kwa ajili ya maombi na masuala mbalimbli ya kiimani kwa vijana na kwamba ni utaratibu waliojiwekea kila mwaka wanafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kukulia kiimani kwani kanisani ndio mahali salama zaidi.
“Vijana kujihusisha na masuala ya Mungu tunanakuwa salama zaidi kwani itatuepusha na mambo mengi yasiyofaa ikiwemo madawa ya kulevya”, alisema Richard
Alisema vijana wakiandaliwa vyema kiroho familia, jamii na taifa kwa ujumla limepona kwa kuwa watajitambua na kuwa wanajamii wanatabua wajibu wao.
Kambi hii ya maombi ilikuwa na vijana wa kike na wa kiume 132 tangu Ijumaa mpaka Jumapili, alisema Richard
Mwalimu Gadielson Mfinanga katika mahubiri siku hiyo aliwakumbusha wakristo kutoruhusu changamoto wanozaopitia kubadili uhalisia wa Mungu katika maisha yao kwani kufanya hivyo kutawagharimu baada ya hali hiyo kuisha.
Alisema Mungu ana tabia ya kuwabakiza watu ambao hata baada ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wataedelea kutembea nao katika nyakati za huzuni au furaha.
“Ni muhimu sana kuwathamini wengine bila kuwahukumu au kuwadharau kwani huwezi kujua ni wakati gani watakufaa”, alisema Mwalimu Mfinanga.
Alisema matokeo ya kila mmoja na alivyo ni mjumuisho wa namna wa watu aliokutana nao katika maisha yake.
Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Mbezi Luis, Godlsiten Nkya aliwashukuru vijana wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwamba wanafanya kazi njema machoni pa Mungu.
Aidha, aliwakumbusha wazazi wa Dar es salaam kujiuliza ikiwa vijana wao wanaosoma vyuoni hususani Chuo Kikuu cha Dar es salaam kama wanajishughulisha na masuala ya kiimani kwa kati ya vijana 132 walifika usharikani hapo hawakuzidi 10 kutoka Dar es salaam.
“Ni wajibu wa wazazi kuwakumbusha vijana wao wasiende na maisha bila Mungu”, alisema Mchungaji Nkya.
Alisema wakati vijana hao wakijishughulisha na kwaya na masuala ya kikanisa wapo wengine ambao wamejiingiza kwenye mambo yasiyofaa ikiwemo ulevi.