Na Vincent Mpepo, OUT

Chuo kikuu Huria cha Tanzania kitaendelea kushirikiana na taasisi za elimu ya juu za ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha kuwa kinaendeleza majukumu yake ya msingi ya ufundishaji,kufanya utafiti na huduma kwa jamii kwa maslahi ya pande zote na jamii kwa ujumla.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii cha chuo hicho Dkt. Dunlop Ochieng wakati akihutubia jopo la wanafunzi na wahadhiri wa Chuo kikuu Huria cha Tanzania na wageni kutoka vyuo vikuu viwili kutoka Norway iliyofanyika jana katika ukumbi wa chuo hicho jijini Dar salaam.

Alisema chuo chake kinathamini sana uhusiano na taasisi za elimu ya juu kutoka nje kwa sababu ushirikiano huo una faida ikiwemo kudumisha na kuendeleza maarifa na ujuzi katika ufundishaji hususani mafunzo kwa vitendo kupitia huduma kwa jamii kitu ambacho kinadhihirisha mchango wa taasisi za elimu ya juu kwa jamii.

‘Watoto wenye mahitaji maalumu na wenye ulemavu wana mahitaji maalumu na maafisa ustawi wa jamii wanafanya kila wazezalo ili kuhakikisha watoto hao wanapata haki zao ambazo wakati mwingine hukiukwa”, alisema Dkt. Ochieng

Alisema ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo umesaidia kuwapa wahadhiri na wanafunzi wa kitanzania na Norway jukwaa la kutekeleza kwa vitendo wakifundisha na kusoma darasani katika mazingira halisi ya jamii.

Mwanafunzi Mtanzania ambaye ni mkufunzi katika idara ya ustawi wa jamii ya Chuo kikuu Huria cha Tanzania, Fauzia Kitenge alisema akiwa nchini Norway alifunza vitu vingi ikiwemo suala la ustaarabu na zaidi namna ya kuishi na watu wa tamaduni za tofauti huku wito wake uikwa ni kueleza au kusimamia ukweli kwa jambo ambalo anaamini ni kweli.

Alisema licha ya utofauti mkubwa wa kimaendeleo kati ya Norway na Tanzania bado misingi ya ubinadamu ya kujali wengine imekuwa nguzo kuu katika nchi zote mbili kama sehemu ya kuthamini ubinadamu.

Aidha alisifu mtindo wa matibabu Norway ambao umejikita katika kuangalia tatizo la mgonjwa katika huduma za kitabibu za kibingwa na ubobevu katika maeneo mbalimbali ya afya tofauti na Tanzania ambapo wakati mwingine masuala ya matibabu huchukuliwa kwa ni kwa ujumlaujumla.

Mwakilishi wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Himolde, Karoline Lie alisema uwepo wao nchini Tanzania wamejifunza vitu vingi ikiwemo tafsiri na matumizi ya nguvu katika ufundishaji au utoaji wa adhabu kwa watoto kitu ambacho ni tofauti katika utekelezaji wa sera na sheria za ufundishaji katika nchi hizo mbili.

Alisema nchini Norway, kuna sera na mifumo thabiti ambayo imeanisha ya aina ya huduma ambazo kila raia anastahili kuzipata kama haki yake katika maeneo ya afya, elimu na huduma za ustawi jamii ambazo ni tofauti na Tanzania.

“Kwa mfumo wa Norway, kila darasa la wanafunzi wa shule za awali na msingi linapaswa kuwa na idadi ya wanafunzi kati ya 20 na 30 na walimu zaidi ya mmoja katika kipindi kimoja”, alisema Karoline.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii ya Chuo kikuu Huria cha Tanzania, Dtk.Mariana Makuu ushirikiano kati ya taasisi hizo unahusisha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo cha Patandi kwa Tanzania wakati kwa Norway  ni Chuo Kikuu cha Molde na Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Shirikishi cha Western.

Posted in

Leave a comment