Na Vincent Mpepo, Morogoro
Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ) Usharika wa Mji Mpya Jimbo la Morogoro wametakiwa kuwa makini na wahubiri wanaojulikana kwa majina ya mitume na manabii kwa kuwa wakati mwingine siyo wote wana karama za uponyaji kama wanavyojinasibu.
Tahadahari hiyo ilitolewa na Mchungaji wa KKKT Usharika wa Mji Mpya Jimbo la Morogoro, Sifu Dunia wakati wa mahubiri katika ibada ya kwanza katika usharika huo leo na kuwataka kusoma na kulielewa neno la Mungu.
Alisema neno la Mungu halihitaji msaada wowote kwa kuwa linajitosheleza hivyo wakisoma na kuelewa itakuwa siyo rahisi kurubuniwa na mahubiri ya mitume na manabii ambao wakati mwingine huwapotosha wakristo.
“Tusiwe wavivu kusoma neno la Mungu vinginevyo tutapokea vitu vya ajabu kwa kutegemea uponyaji na kufunguliwa”, alisema Mchungaji Sifu.
Aliwataka washarika kutofanya mzaha na neno la Mungu kwa kuwa lina nguvu ambayo huleta matokeo kwa kadiri ya maombi na mapenzi yake.
“Tuache mzaha na neno la Mungu kwani kufanya hivyo ni utani na Mungu mwenyewe”, alisema Mchungaji Sifu.
Aidha aliwakumbusha washarika kumalizia ahadi za mwaka 2023 na kwamba kila mmoja ashiriki kwenye sadaka ya fungu la kumi ambayo itafanyika kila Jumapili ya mwisho wa Mwezi.
“Kama Mungu hajakubariki usitoe kitu”, alisema Mchungaji Sifu.


Leave a comment