Na Vincent Mpepo, OUT

Watanzania wametakiwa kujenga utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kuwa na uhakika wa maendeleo kiafya badala ya kusubiri  vipimo wakati wa homa.

Wito huo ulitolewa na Daktari Julius Mchelele kutoka Kliniki ya Path Labs wakati wa tukio la ufunguzi wa mbio za Marathoni lilioandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wakazi wengi wao vijana.

“Watu walijitokeza kwa wingi na wamepima afya zao”, alisema Dkt.Mchele

Aliushukuru uongozi Uongozi wa vijana wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kuwaalika katika tukio hilo na kuwataka kuendelea na ushirikiano huo kwa matukio mengine kwa wakati ujao.

Alisema chagamoto kubwa kwa baadhi ya washiriki wa mbio hizo baada ya vipimo ni shinikizo la damu la juu na la chini ambalo linatokana na mtindo wa maisha na masuala ya ulaji.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Damu, Kitengo cha Damu-Muhimbili, Richard Massam alisema mwitikio siyo mbaya kwa kuwa wapo minongoni mwa washiriki waliojitokeza kutoa damu huku akiwakumbusha watanzania kuendelea kuchangia damu kutokana na mahitaji makubwa.

 “Ili kuokoa wagonjwa wenye uhitaji wa damu ni lazima binadamu mwingine akubali kuchangia damu”, alisema Massam.

Alisema kitengo chake huwa kina matukio ya kukutanisha watu ya mara kwa mara ili wanaokubali wachangie damu kutokana na ukweli kuwa hakuna kiwanda cha kuzalisha damu.

“Ninaomba ambao wapotayari waungane nasi kwa siku zote mitaani, shuleni na nyumba za ibada ili tuendelee kuokoa uhai wa wahitaji wa damu”, alisema Massam

Mwenyekiti wa Taasisi ya Eduthon Elite Suuport, Anwari Said alisema dhima ya taasisi yake ni kuhakikisha inatengeza na kushirikisha vijana fursa mbalimbali za kuchumi, kijamii na kisiasa ili waweze kujikwamua.

Mshauri katika masuala ya uongozi na utawala ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Emmanuel Mallya alisema vijana wanatakiwa kuwekeza katika afya zao kwa kuwa ndio mtaji wa kwanza kabla ya vitu vingine.

“Usifikirie cheo kwanza kwa kuwa utachanganyikiwa na kupata msongo wa mawazo na kuhisi wanapendeleana”, alisema Dkt.Mallya.

Ufunguzi wa mbio hizo za Marathoni ni maandalizi ya uzinduzi wa mbio zitakazofanyika 04 May, 2024 zenye lengo la kukusanya pesa ili kusaidia wanafunzi wa chuo hicho ambao wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa ada.

Posted in

Leave a comment