Na Mwandishi Wetu

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Pius Lutumo Leo 17 Februari 2024 ameshiriki kutoa elimu ya haki jinai katika Kanisa la Pentekoste Kibaha ikiwa ni sehemu ya elimu kwa jamii (ushirikishwaji jamii) katika kutatua  uhalifu na wahalifu.

Kongamano hilo lililoandaliwa  na Pwani Pastors Network na Pastors Fellowship Kibaha maili moja, kamanda Lutumo alisema kuwa jukumu la viongozi wa dini ni kuhakikisha jamii inaishi kwa kufuata sheria na maadili mema yanayofundishwa na wachungaji katika nyumba za ibada ambapo wao ndio  viongozi.

Akifafanua juu ya mada hiyo kamanda alisema ni vema zaidi kushukuru kwa Mungu juu ya uumbaji wetu kuliko kuomba kila siku huku akisema chanzo cha uhalifu na wahalifu ni jamii kukosa maaadili yanayochochea vijana kuwa wezi, vibaka, majambazi au hata wauaji katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kujinufaisha na kujipatia kipato kwa njia zisizo halali.

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kukemea jamii kutofanya vitendo vya kihakifu kupitia mahubiri huku wakisisitiza matendo mema.

Kamanda Lutumo alisema serikali kupitia Kamati ya Haki Jinai iliyoundwa mwaka 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Daktari Samia Suluhu Hassan ikiongozwa na Jaji Mstaafu Chande Othman ilikusudia kusaidia jamii kupitia Jeshi la polisi kwa kuboresha utendaji wa kazi kwa kuongeza vitendea kazi, kuboresha hali ya maisha kwa kujenga nyumba za askari na kuwapandisha vyeo.

Sanjali na hayo kamati ilitoa maelekezo juu ya utolewaji wa dhamana kwa kila mtuhumiwa anapofikishwa kituo cha Polisi.

“Ubambikiaji kesi uishe maana unawakosesha haki wananchi”, alisema Kamanda Lutumo.

Kamati ilielekeza  ilisema dhamana ni haki ya kila mtuhumiwa na itolewe pasipo masharti magumu na vikwazo, maana  imekuwa tabia ya watu kupelekana Polisi kwa makosa ya kawaida yanayoweza kusuluhishwa na viongozi wa kijamii pasipo kufika Polisi.

Alisema utolewaji wa dhamana utapunguza mlundikano wa mahabusu walio na makosa yenye dhamana katika vituo vya Polisi

Posted in

Leave a comment