Na Vincent Mpepo, Bagamoyo
Mratibu wa Manunuzi, Daudi Sospeter akifafanua jambo wakati wa kikao kazi cha tatu cha tathimini ya maendeleo ya mradi wa magezi ya kiuchumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kilichoanza leo Wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. (Picha na Vincent Mpepo, OUT).

Wanataaluma wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wametakiwa kufikiri namna bora ya matumizi ya rasilimali majengo yatakayopatikana kupitia mradi wa mageuzi ya kiuchumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ili kuwa na uhusiano wa moja kwa moja kati ya taaluma na maendeleo ya kiuchumi nchini..
Wito huo umetolewa leo na Mratibu Mkuu wa Mradi huo wa chuo hicho Profesa Deus Ngaruko katika siku ya kwanza ya kikao kazi cha siku tatu kinachoendelea Mkoani Pwani Wilaya ya Bagamoyo na kuwahusisha waratibu wa mradi katika idara zote na wakurugenzi wa vituo vya chuo hicho ambao mradi huo utafanyika katika vituo vya mikoa wavyoviongoza.
Alisema wanataaluma kwa ujumla wao wanapaswa kufikiria miradi endelevu yenye tija kwa kuongeza thamani na kuzalisha bidhaa na hudumua endelevu ambazo zitasaidia kuwa na progamu za kitaaluma zenye uhusiano wa moja kwa moja na ajira ili kuwa na wahitimu watakaoweza kujiajiri mara baada ya kuhitimu.
“Vyuo vikuu vinatakiwa kuwa chachu ya maendeleo kupitia programu mbalimbali ambazo zitasaidia kuandaa wahitimu wenye ujuzi wa vitendo”, alisema Profesa Ngaruko.
Mratibu wa Kituo cha Mkoa cha Chuo Kikuu HurIa cha Tanzania cha Mtwara, Mhadhiri Msafiri Njoroge alisema wamepokea mawazo hayo na kubainisha kuwa mazingira na muktadha wa kila mkoa unaweza kutoa fursa tofauti na mikoa mingine.
“Kwa asili ya muktadha wa maeneo ya vituo hivyo tunaweza kubuni miradi midogomidogo itakayotumia taaluma kupata pesa”, alsima Dkt.Njoroge.
Aidha alishauri kuwepo kwa mwendelezo wa majadiliano na ushirikishwaji na mahusiano mazuri kati ya wakurugenzi wa vituo vya chuo hicho na timu ya watekelezaji ili kupata matokeo mazuri zaidi kiutekelezaji.
Mratibu Msaidizi wa Mradi huo chuoni hapo, Mhandisi, Dkt. Timothy Lyanga alisema katika utoaji wa kandarasi za mradi huo masuala ya kisheria yamezingatiwa ikiwemo kuwa na makubaliano ambayo yanaweka bayana majukumu ya watekelezaji mradi huo katika kila hatua.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni moja ya taasisi za elimu ya juu kinachotekeleza mradi wa miaka mitano wa magaeuzi ya kiuchumi kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia wenye lengo la kukuza elimu ya juu, kukuza uchumi na kujenga uwezo wa vyuo vikuu ili kuchangia katika maeneo muhimu ya uvumbuzi, maendeleo ya kiuchumi ikiwemo uwekezaji katika uimarishaji wa miundombinu ya ufundishaji, utafiti na kuendeleza wahadhiri kitaaluma.
Leave a comment