Na Vincent Mpepo, OUT
IMEELEZWA kuwa baadhi ya sheria, taratibu na kanuni za manunuzi nchini ni kikwazo kinachokwamisha utelekezaji wa miradi kwa muda uliopangwa na kusababisha wananchi kutopata huduma kwa muda uliopangwa.
Hayo yamebainishwa na Mratibu Mkuu wa Mradi wa Mageuzi ya kiuchumi, Profesa Deus Ngaruko katika siku ya pili ya kikao kazi cha siku tatu kinachoendelea Mkoani Pwani Wilaya ya Bagamoyo na kuhusisha waratibu wa mradi katika idara zote na wakurugenzi wa vituo vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambao mradi huo unatekelezwa katika vituo vya mikoa wanavyovisimamia.
Alisema taratibu, kanuni na sheria za manunuzi zinaleta ugumu katika kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo miradi wa mageuzi ya kiuchumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
“Fedha zipo lakini tunashindwa kuzitumia kutekeleza mradi kwa wakati kwa sababu kuna taratibu ambazo zinatumia muda mrefu kukamilika, kuna haja kuangaliwa kwa taratibu hizi,”alisema Profesa Ngaruko.
Mratibu wa uhuishaji mitaala, Dkt. Halima Kilungu alisema utekelezaji wa miradi kama huu wa mageuzi ya kiuchumi unahitaji wafanyakazi wa taasisi husika kutoka idara na vitengo vyote kushirikiana ili kuhakikisha kuwa changamoto za ndani zinatatuliwa ili kwa pamoja kuhakiksha mradi unatekelezeka kwa faida ya taasisi na taifa kwa ujumla.
“Ni muhimu kwa wafanyakazi wa idara zote ndani ya taasisi kushirikiana ili kuhakikisha kuwa mradi unafanikiwa kwani ukifeli ni taasisi na taifa limefeli”, alisema Dkt.Kilungu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Manunuzi wa Mageuzi ya kiuchumi chuoni hapo, Daudi Sospeter alisema ni muhimu kufuata taratibu, sheria na kanuni za manunuzi ili kuondokana na changamoto za kiuhasibu na mahesabu.
“Sheria za manunuzi zinaweza kuwa na tasfiri tofauti na ilivyokusudiwa”, alisema Sospeter.
Alisema lengo la kusimamia sheria, kanuni na taratibu za manunuzi ili yaende kwenye mamlaka husika
Mradi wa mageuzi ya kiuchumi wa miaka mitano kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia una lengo la kukuza elimu ya juu kama chachu ya uchumi mpya wa Tanzania ikihusisha kupanua uwezo wa vyuo vikuu katika maeneo muhimu ya uvumbuzi, kuongeza soko la ajira na kwa kuwekeza katika miundombinu inayohitajika kwa ufundishaji na utafiti wa kisasa.

Leave a comment