Waandishi wa Habari wanawake wameshauriwa kuungana na kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi jambo ambalo litawasaidia kuwa na kipato mbadala na kuondokana na utegemezi wa kazi moja.
Mwenyekiti wa umoja wa waandishi wa Habari mkoa wa Arusha Jamillah Omar ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa chama hicho cha ARUSHA WOMEN IN MEDIA ulioenda sambamba na semina elekezi iliyohusisha masuala ya ujasiriamali na fursa za mikopo zitolewazo na benki ya CRDB,Usalama wa mitandaoni kwa wanawake mada iliyotolewa na TCRA,maadili ya uandishi wa Habari na malezi bora ya Watoto.
Jamilah amesema serikali chini ya mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetoa Fursa nyingi za kuwawezesha wanawake ikiwemo mikopo isiyokuwa na riba hivyo imefika wakati sasa kwa waandishi wa Habari wanawake nao kutumia fursa hiyo kujiingiza katika ujasiriamali ili waweze kuwa na chanzo kingine cha mapato.
Amesema kutokana na kupanda kwa gharama za Maisha na mara nyingi wanawake ndio wamekuwa kukabiliwa na majukumu mengi ya malezi ya familia wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kipato hivyo wakati mwingine kusababisha kuzidiwa na majukumu ambapo kwa kutumia fursa ya umoja huo itawasaidia kuungana na kunufaika na fursa mbalimbali.
“Siku zote sisi kama waandishi wa Habari tumekuwa vianara wa kuripoti matukio mbaimbali ikiwemo hizi fursa za mikopo kama ya Halmashauri inayotolewa kwa ajili ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu lakini sisi kama waandishi wa Habari wanawake tumetumia vipi fursa hiyo?alihoji Jamillah
“Imefika wakati sasa waandishi wa Habari wanawake tubadilike kwanza tumechelewa sana kila mtu anatushangaa tulikuwa wapi hadi leo hatuna umoja wa kama huu”alisema
Mgeni Rasmi katika hafla hiyo mfanyabiashara mjasiriamali wa sekta ya utalii Genevive Mollel amewapongeza waandishi wa Habari wanawake mkoa wa Arusha kwa kuanzisha umoja huo ambapo amewatoa hofu kuwa ujasiriamali si kitu kigumu na kusisitiza kuwa wanaweza kutokana na tasnia na uwanda mpana katika kila sekta.
“katika sekta yenu ya Media inafursa nyingi sana mnakutana na watu wengi sana kila siku kila mahali kwa mfano kwenye sekta ya utalii hatuwezi kupanda bila media kuna vivutio vingi ambavyo vinatanganzwa kwa kupitia media hii ni fursa”alisema Genevive
Awali mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa Habari mkoa wa Arusha Cloud Gwandu akizungumza katika hafla hiyo amewapongeza waandishi wa Habari wanawake kwa kuungana na kusema kuwa dunia ya sasa bila kuungana huwezi kufanya kitu chochote kikubwa hata kama unakili au uwezo kama nani.
“Ninawaomba waandishi wa Habari ambao hawajajiunga kujiunga na chama hicho ili kiwe na nguvu ili wawe na sauti moja itakayosikika itakayowasaidia kuwafikisha mbali”alisema Gwandu
Amesema hivi sasa tasnia ya uandishi wa Habari inakabiliwa na changamoto kubwa ya kazi zao nyingi kufanywa na maafisa Habari wa serikali jambo ambalo limepunguza wigo wa waandishi kupata kazi za kufanya hivyo kwa umoja huo itawasaidia kubadilishana Mawazo na kutumia vyema fursa mbadala kujikwamua kiuchumi.
Gwandu amesema waandishi wengi wa Habari hawana ajira hivyo uhakika wa kipato chao ni mdogo hali inayowazalimu wakati mwingine kuwa omba omba kwa wadau hali ambayo amesema imekuwa ikiwadhalilisha.
Leave a comment