Na Mwandishi Wetu

Sehemu ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoani Arusha ‘Arusha Women in Media’ katika picha za pamoja katika ukumbi na viwanja vya Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyofanyika hivi karibuni.

Waandishi wa habari wanawake mkoa wa Arusha wametakiwa kuchangamkia fursa kwa kujiunga na chama cha waandishi wananawake mkoani humo ili kuwa na umoja wenye nguvu na sauti moja katika kujikomboa kiuchumi.

Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Off we Go safaris Ltd Genevive Mollel ametoa wito huo wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Arusha kijulikanacho kwa jina la ‘ARUSHA WOMEN IN MEDIA’ ulifanyika jijini Arusha na kuhudhuliwa na wanawake waandishi wa mkoa huo, wanafunzi wanawake wa tasnia hiyo na wadao mbalimbali.

Alisema uandishi wa habari ni tasnia mtambuka ambayo yenye fursa nyingi zikiwemo za kiuchumi na kijamii hivyo waandishi wa habari waache kujifungia sehemu moja ili kuona fursa katika maeneo mengine ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuacha utegemezi.

Mwenyekiti Arusha Women in Media Jamillah Omar amesema lengo umoja huo ni kutumia fursa mbalimbali zitolewazo na serikali, wakala wa serikali, makampuni na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya wanawake ikiwemo mikopo  yenye masharti nafuu na isiyo na riba.

Alisema waandishi wa habari wanawake kama walivyo wanawake wengine wanakabiliwa na changamoto ya kipato kutokana na majukukumu ya familia hivyo umoja huo utawasaidia kuzifikia fursa hizo kwa pamoja na hatimae kujikwamua kimaisha.

“Waandishi wenzangu hasa wanawake mnatambua namna ambavyo mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amejipambanua kuwawezesha wanawake kiuchumi hivyo na sisi tujiongeze tutumie fursa hizo tuwe na vyanzo mbadala vya kujiongezea kipato”alisema Jamillah.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha Cloud Gwandu aliwataka waandishi wa habari wanawake kujiunga na umoja huo ili wawe na sauti moja itakayosaidia kufikia malengo yao.

Alisema waandishi wa habari wengi sasa hivi wanapitia changamoto ya ajira ambapo asilimia kubwa hawana ajira wala mikataba ya kazi jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa maisha yao.

“Tasnia ya habari kwa sasa inapitia wakati mgumu kwa kuwa kazi nyingi za serikali zimekuwa zikifanywa na maafisa habari wa serikali badala ya kutumia waandishi wa habari”, alisema Gwandu.

Wakati huo huo Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Vincent Mpepo aliwakumbusha waandishi kuzingtia maadili na weledi katika kazi zao na kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia amabyo yana changamoto kadha wa kadha.

Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Arusha, Amulikiwa Massawe alisema uzinduzi wa umoja huo umekuja wakati mwafaka ambapo benki ya CRDB  imetenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwakopesha wanawake kwa masharti nafuu .

“Habari njema kwa sasa ni kwamba CRDB ina akaunti maalum kwa ajili ya wanawake ikiwemo akaunti za Malkia na Imbeju ambazo zina masharti nafuu”, alisema Massawe.

Kwa mujibu wa matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika barani Afrika na nchini Tanzania zinabainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya habari ikiwemo kuyumba kiuchumi kwa vyombo vingi vya habari hivyo kushindwa kuwapa waandishi wa habari stahiki zao kwa muda muafaka ikiwemo mishahara na mikataba ya ajira za uhakika hivyo kuwafanya waendelee kuwa tegemezi jambo linaothiri pia misingi ya uandishi wa habari ambapo kuna wakati waandhi wa habari wanakuwa wasemaji wa watu badala ya umma.

Posted in

Leave a comment