Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dkt. Mariana Makuu akisisitiza jambo wakati wa kikao cha tathmini  ya kutekeleza program za kuwasaidia watu wenye ulemavu kikiwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo, wahadhiri, walimu, maofisa maendeleo ya jamii na wafadhili kutoka nchini Norway iliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni katika ukumbi wa chuo hicho.

Na Grace Mwakalinga, Dar es salaam

Serikali imeshauriwa kuajiri wataalamu wa ustawi wa jamii kwenye  shule  za  msingi jumuishi  ili kuwahudumia kikamilifu watoto wenye mahitaji maalum ambao wakati mwingine hukosa  mtu wa karibu kujua mahitaji yao wawapo shuleni.

Mapendekezo hayo yametolewa na Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dkt. Mariana Makuu wakati wa kikao cha tathmini  ya kutekeleza program za kuwasaidia watu wenye ulemavu kikiwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo, wahadhiri, walimu, maofisa maendeleo ya jamii na wafadhili kutoka nchini Norway iliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni katika ukumbi wa chuo hicho.

Alisema mahitaji ya matunzo kwa  watoto wenye mahitaji maalumu kwenye jamii na waliopo shuleni ni makubwa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hivyo kuna uhitaji wa walimu kuongezewa nguvu kutoka kwa wataalamu wa ustawi wa jamii ambao watafanya kazi pamoja na walimu hao ili kuhahikisha ustawi wa watoto katika mazingira ya shule na jamii kwa ujumla.

“Walimu peke yao hawawezi kwani wana majukumu ya  kutekeleza mtaala lakini hili la kuwasaidia kwa mambo mengine linaweza kufanyiwa kazi vyema na wataalamu wa ustawi wa jamii”, alisema Dtk. Makuu.

Alisema kutokana na changamoto hiyo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinaishauri serikali kuajiri wataalamu wa ustawi wa jamii kwenye shule zote jumuishi ili kuongeza nguvu ya kuwasaidia watoto hao kielimu, kiakili na kiafya ili  wawe sawa kama watoto wengine.

“Idadi kubwa ya watoto wenye mahitaji maalum shuleni wanashindwa kutimiza ndoto zao kutokana na kukosa uangalizi maalum ili kusoma vizuri kama watoto wengine, alisema Dkt.Makuu.

Mwalimu wa shule ya msingi jumuishi ya Uhuru Mchanganyiko, Catherine Chitanda, alisema utaratibu huo  utakuwa mwarobaini wa kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum shuleni kwa kupata usaidizi wa karibu kutoka kwa wataalamu wa ustawi wa jamii ambao watakuwepo shuleni kuwahudumia.

Aidha Catherine alisema katika kufanikisha hilo, lazima serikali ikubali kushirikiana na jamii, walimu na wataalamu wa ustawi wa jamii ili kutimiza kikamilifu jukumu la  kuwatunza  na kuwalea watoto wenye mahitaji maalum shuleni.

Mtalaam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Stella Shayo, alisema katika kutekeleza programu hiyo chuo kimejipanga kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia kwa wazazi, walezi na jamii juu ya athari za vitendo hivyo ili kuwaweka sawa kisaikolojia watoto hao wawapo shuleni.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kinondoni, Silider Ussuma alisema anaunga mkono jambo hilo na kwamba litasaidia kuwaweka sawa kiakili watoto wenye mahitaji maalumu.

Alisema sababu mojawapo inayosababisha changamoto kwa watoto ni migogoro ya mara kwa mara kwa baadhi ya wanandoa ambayo ina athari hasi kwa watoto na wakati mwingine kutofanya vizuri kitaaluma na hivyo uwepo wa wataalamu wa ustawi wa jamii utasaidia kuwapa ushauri watoto ili wawe sawa kiakili.

Tanzania imesaini  mikataba mbalimbali ya kimataifa ya watu wenye ulemavu  ikiwemo mkataba wa haki za mtoto, CRC mwaka 1989 ambapo mataifa yalikubaliana kuwa na sheria na kanuni za kulinda haki za watoto kwa mataifa wanachama.

Sehemu ya washiriki wa kikao cha tathmini  ya kutekeleza program za kuwasaidia watu wenye ulemavu kikiwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo, wahadhiri, walimu, maofisa maendeleo ya jamii na wafadhili kutoka nchini Norway iliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni katika ukumbi wa chuo hicho.

Posted in

Leave a comment