Sehemu ya picha katika matukio ya hivi karibuni wakati wa kukabidhi misaada ya vifaa katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam tukio lililohudhuriwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambao ni wenyeji, wahadhiri na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Norway, walimu na wanafunzi wa shule hiyo. Vifaa hivyo vitapunguza tatizo la uhaba wa nyenzo za kufundishia, kujifunzia na vinakadiriwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni tisa na nusu za kitanzania.
Picha2: Bidhaa za kazi za mikono zinazotenegezwa na Kikundi cha Uhuru Mamas ambacho kinajumuisha akina mama wenye watoto wa mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo jijini Dar es salaam ambacho ni sehemu ya mradi unaotekelezwa kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na vyuo vikuu vya Molde na Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi Shirikishi vya Norway(Picha na Vincent Mpepo, OUT.


Na Mwandishi wetu, OUT
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Mariana Makuu, ameishauri Serikali kuajiri wataalamu wa ustawi wa jamii katika shule za msingi jumuishi ili kuwaweka sawa kiakili na kisaikolojia watoto hao wawapo shuleni.
Wito huo umetolewa wakati wa kukabidhi misaada ya vifaa katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko huko Dar es Salaam leo jijini Dar es salaam na kuhuduriwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambao ni wenyeji, wahadhiri na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Norway, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.
Dkt. Makuu ameeleza kwamba kuwepo kwa wataalamu wa ustawi wa jamii katika shule hizo kutaweza kusaidia kikamilifu watoto wenye mahitaji maalum ambao mara nyingi wanakosa mtu wa karibu kuelewa mahitaji yao wanapokuwa shuleni. Anasisitiza kuwa matunzo, uangalizi, na malezi kwa watoto hawa yanakabiliwa na changamoto nyingi, na hivyo kuna haja ya kuwa na wataalamu wa kutosha katika eneo hilo.
“Kuajiri wataalamu wa ustawi wa jamii kutapunguza athari hasi katika malezi na makuzi ya watoto hao, na hivyo kuwasaidia kufikia ndoto zao kielimu”, alisema Dkt.Makuu.
Alisema, kwa kuzingatia majukumu mazito ya walimu katika kutekeleza mtaala upo umuhimu wa kuwa na wataalamu wa ustawi wa jamii ambao watasaidia katika mambo mengine yanayohusiana na malezi na makuzi ya watoto hususani wenye mahitaji maalumu.
Aidha, alisisisitiza kwamba idadi kubwa ya watoto wenye mahitaji maalum katika shule wanakabiliwa na changamoto za kielimu kutokana na kukosa uangalizi maalum hivyo kukwama au kutofika mbali katika elimu.
Kwa upande wake, mwanafuzni wa ustawi wa jamii kutoka kutoka Norway, Marianne Valsvik alisema wanajisikia vizuri kuwa sehemu ya kuwafariji watoto kwa vifaa mbalimbali vitakavyosaidia katika kusoma, usafi na mahitaji mengine.
“Nimejifunza mengi hapa Tanzania kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii na namna watoto wenye mahitaji maalumu wanavyoishi”, alisema Marianne.
Mwakilishi wa wanafunzi kutoka Norway, Karoline Lie alisema msaada huo unajumisha vifaa mbalimbali ikiwemo vya usafi, madaftari, kalamu za risasi na wino, maboksi ya vifaa vya msaada wa kwanza, viti vya na vinagharimu zaidi kiasi cha shilingi milioni tisa na nusu za kitanzania.
“Vifaa vingine ni pamoja na makabati ya kuhifadhia vifaa vya walimu, vifaa vya ichezo mbalimbalimbali, matanki, mabeseni na vifaa vingine vya jikoni”, alisema Karoline
Tanzania imesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa ya watu wenye ulemavu ikiwemo mkataba wa haki za mtoto, CRC mwaka 1989 ambapo mataifa yalikubaliana kuwa na sheria na kanuni za kulinda haki za watoto kwa mataifa
Leave a comment