Na Grace Mwakalinga, Dar es Salaam
Idadi ya watoto wenye ulemavu wanaosoma katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyikoiliyopo jijini Dar es Salaam imeongezeka baada ya Chuo Kikuu Huria Tanzania kwa kushirikiana na vyuo vikuu kutoka Norway kuanzisha programu ya kuwawezesha wanawake wenye watoto shuleni hapo kujifunza shughuli za ujasirimali ili kujiingizia kipato.
Hayo yamebainika wakati kukabidhi misaada ya vifaa katika
Shule hiyo hivi karibuni iliyohudhuriwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambao ni wenyeji na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Norway, walimu na
wanafunzi wa shule hiyo.
Katibu wa kikundi cha Uhuru Mamas, Caroline Nyamala alisema
ongezeko la watoto wenye mahitaji maalumu shuleni hapo limetokana na fursa ya akina mama kuwezeshwa kiuchumi kupitia kufanya kazi za mikono ambazo wanaziuza ili kujikwamua kiuchumi.
Alisema kabla ya fursa hiyo walikuwa wanakutana shuleni hapo
wakielezana vikwazo na madhila wanayokumbana nayo kifedha na kisaikolojia baada ya kuachwa na wenza wao kwa sababu ya kupata watoto wenye mahitaji maalumu lakini kwa sasa wanamshukuru Mungu kwa kuwa mambo yamebadilika.
“Lakini baada ya kupata ufadhili wa kupata mafunzo ya kutengeneza bidhaa mbalimbali za mikono tumeungana na tunafanya shughuli zetu huku tukiendelea kuwasubiri watoto wamalize vipindi vya darasani,” alisema Caroline.
Alisema kikundi hicho kimekuwa hospitali ya akina mama wenye
watoto wa mahitaji maalum na wanaita kitengo kwa sababu kimeponya majeraha yao na kuwaweka sawa kisaikolojia huku pia wakijikwamua kiuchumi.
Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Herieth Kabende alisema kwa sasa wamefikia 35 na kwamba wameunganishwa na wadau mbalimbali kwa ajili kupitia bidhaa wanazozitengeneza na kuzuiza ikiwemo vikiwemo vikapu.
Aidha, aliiomba serikali kusaidia matibabu bure kwa watoto wenye ulemavu kwa kuwa kuwa gharama za kuwahudumia ni kubwa ukilinganisha na watoto wa kawaida.
Alisema asilimia kuwa ya wanaowahudumia watoto hao ni wanawake ambao wameachwa na waume zao bila kuwa na chanzo cha uhakika cha mapato hivyo wanapitia wakati mgumu pindi wanapougua.
“Mtoto mwenye ulemavu akiumwa gharama zake ni kubwa sana kwa
sababu atahitaji kutibiwa ugonjwa unaomsibu , viungo vyake na mahitaji mengine”, alisema Herieth.
Alisema kwa taratibu za sasa ambazo zinawalazimu kujikusanya
hadi kufikia 100 ndipo wakate bima zimekuwa ngumu na kuomba serikali iwasaidie.

Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Vincent Mpepo akifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Kikundi Uhuru Mamas Collection, Herieth Kabende hivi karibuni katika viwanja vya Shule ya Msingi Mchanganyiko iliyopo jijini Dar es salaam wakati wa kukabidhi misaada ya vifaa katika Shule hiyo iliyohudhuriwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya Norway, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.(Picha na Solfrid Raknes kutoka Norway).
Leave a comment