Na Grace Mwakalinga, Dar es Salaam
Vyuo vikuu viwili kutoka nchini Norway vimetoa msaada wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalum, Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati kukabidhi vifaa hivyo, Profesa Bente Dale Malones, alisema vifaa hivyo vitapunguza tatizo la uhaba wa nyenzo za kufundishia, kujifunzia na vifaa vya michezo shuleni hapo na kwamba vinagharimu kiasi cha shilingi milioni 9.5.
Alisema shule hiyo ambayo ni ya mfano kutembelea imekuwa na mambo mengi mazuri ya kujifunza kama vile uwezo watoto hao darasani na ari ya walimu kufundisha kitu kinachopaswa kuigwa.
Alianisha vifaa walivyovitoa kuwa ni madaftari, kalamu za wino na risasi, viti mwendo, vifaa vya usafi, mipira, sabuni, maandishi ya nukta nundu, midoli, ndoo za kuhifadhia maji na vifaa vingine.
“Tumefurahia mazingira ya shule kwa kipindi hiki cha wiki mbili tulichokaa na kuwafundisha watoto na tunaahidi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuendeleza ushirikiano katika eneo hili la kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu,” alisema Bente Dale.
Akipokea msaada wa vifaa hivyo, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Hajrati Kashakara, alisema vitasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa wa vifaa hivyo kwa watoto hao,aliomba ushirikiano huo uendelee ili wapate vitu vingi kwa ajili kuwasaidia kusoma katika mazingira mazuri.
Mwalimu asiyeona, Saada Kiponza ambaye anafundisha wanafunzi wasioona hatua ya kwanza hadi ya tatu, alisema anafurahia kazi yake kwa sababu anafundisha watu wenye changamoto kama yake na kwamba anapofundisha anahakikisha wanamuelewa kwa sababu anajua mbinu za kuwasiliana nao.
Aliongeza kuwa licha ya kufurahia kuwafundisha watu wenye tatizo kama lake lakini anakabiliwa na tatizo la vifaa vya kufundishia,kujifunzia na miundombinu ya shule kutokuwa rafiki kwao hali inayohatarisha afya na usalama wao.
“Nimekuwa mwalimu kwa miaka 22 sasa nikifundisha mikoa mbalimbali naipenda kazi yangu na ninamshukuru Mungu watoto wangu wananielewa na wanafanya vizuri kwenye mitihani yao”, alisema Saada.
Aidha alisema kuna changamoto katika ufundishaji kwa baadhi ya watoto wenye wenye ulemavu zaidi ya mmoja hali ambayo ni ngumu kumudu lakini kama walimu wanajitahidi kwa sababu wanafunzi hao ni marafiki zao wa ukweli.
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dk. Mariana Makuu alisema mahitaji ya kutunza watoto wenye mahitaji maalum shuleni ni makubwa kwa wakati huu kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto katika jamii.
“Tunaiomba serikali kuajiri maofisa ustawi wa jamii kwenye shule zote jumuishi ili kuongeza nguvu ya kuwasaidia watoto hao,kielimu, kiakili na kiafya ili kuwa sawa kama watoto wengine”, alisema Dkt.Makuu.
Alisema idadi kubwa ya watoto wenye mahitaji maalumu shuleni wanashindwa kutimiza ndoto zao za elimu kwa sababu ya kukosa uangalizi maalumu ili kusoma vizuri kama watoto wengine hivyo uwepo wa wataalamu wa ustawi wa jamii utasaidia kuwahakikishia ustawi na maendeleo yao.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho kinatekeleza programu za kuwasaidia watu wenye ulemavu nchini kina ushirikianio na taasisi za elimu ya juu ndani na nje ya nchi ikiwemo kutoka Norway ambapo kinahusisha kubadilishana uzoefu kwa wahadhiri na wanafunzi katika maeneo ya ufundishaji na mafunzo kwa vitendo.
Leave a comment