Na Vincent Mpepo, Morogoro
Wakristo wakatoliki nchini wamekumbushwa kuienzi imani yao na kuepuka kufuata upepo wa mijuiza hivyo kudumu na kutohamahama.
Hayo yamebainishwa wakati mahubiri na tafakari katika ibada ya Jumuiya Ndogondogo ya Mtakatifu Alfonsi iliyofanyika kwa mwanajumuiya Dkt.Issaya Lupogo wa Kihonda na kuhudhuriwa na wanajumuiya hiyo kama ilivyo kawaida ya kanisa hilo.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Elisha Emmanuel alisema wakati umefika kwa wakristo kutambua kuwa ukombozi ulioletwa na Yesu Kristo haukuja ili kuondoa shida, dhiki na mahangaiko duniani badala yake ni jukumu la wakristo kutambua uwepo wa changamoto hizo na ziwape ari ya kupambana nazo kwa imani.
“Shida na matatizo ni sehemu ya maisha ya mwanadamu”, alisema Elisha.
Aidha aliwakumbusha wanajumuiya kuendelea kulitegemeza kanisa kwa zaka, sadaka na michango mingine.
Mwenyekiti Msaidizi wa Jumuiya hiyo, Dkt.Issaya Lupogo alisema wakristo wanatakiwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu ili kuandaa maisha ya umilele na ili kufanikisha hilo hawana budi kusoma neno la Mungu na kulielewa ili kulinasibisha kimwili na kiroho.
Alisema hata katika maisha ya kawaida hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi bila watu kufanya kazi kwa bidii, maarifa na juhudi.
“Mchakato wowote wa kimaendeleo unahusisha kutumia nguvu, akili na wakati mwingine kutoka jasho”, alisema Dkt.Lupogo.
Jumuiya ya Mtakatifu Alfonsi ni mojawapo ya zilizopo katika Parokia Teule ya Mtakatifu Benedicto Jimbo Katoliki la Morogoro.


Sehemu ya wanajumuiya ya Jumuiya ya Mtakatifu Alfonsi katika Parokia Teule ya Mtakatifu Benedicto Jimbo Katoliki la Morogoro (Picha na Vincent Mpepo).
Leave a comment