Na Vincent Mpepo, Kwembe

Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT amewakumbusha wanawake kuvaa mavazi ya heshima kanisani ili kuendelea kuwa walezi wazuri kwa watoto na jamii.

Mchungaji Dkt.Mwatumai Mwanjota aliyasema hayo wakati akihubiri katika ibada ya Jumapili Mtaani hapo na kuwataka wajijengee heshima kwa mwenendo mwema ikiwemo mavazi.

“Wakati mwingine akina mama tunajishushia heshima yetu wenyewe kwa aina ya mavazi tuyavaayo”, alisema Mchungaji Dkt.Mwanjota

Aidha, alisema tabia hiyo ni sehemu ya mwenendo mbaya katika jamii na kwamba kwa kufanya hivyo wanakiuka majukumu waliyopewa kwa jamii japo pia alibainisha kuwa wapo wanaume ambao pia huvaa vibaya.

“Utakuta mwanaume mzima anavaa suruari chini ya kiuno”, alisema Mchungaji Dtk. Mwanjota.

Aidha aliwakumbusha wanawake kutambua nafasi ya mwanume katika familia kwa kuwa wapo baadhi ambao wakijaaliwa kuwa na nafasi nzuri kiuchumi au madaraka huwadharau waume zao.

Hata kama una madaraka na nafasi nzuri zaidi ya mume wako tambua nafasi yake kuwa ni kichwa, alisema Mchungaji Dkt.Mwanjota.

Kwa upande wake, Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwakumbusha washarika wa mtaa huo kupitia jumuiya zao kufanya usafi katika maeneo yao kanisani hapo ili kuweka mazingira ya kanisa hilo katika hali ya usafi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi Mtaani hapo, Exaud Mchome amewakumbusha washarika kutimiza ahadi zao ili kazi ya ujenzi iendelee bila kukwama.

Aliwaomba washarika kuendelea kumtolea Mungu ili kufanikisha kazi ya ujenzi na kwamba kiuhalisia hakuna ambaye anaweza kutamka hana cha kumpa Mungu kwa kuwa wema wake umeendelea kuwa katika maisha yao.

“Hata pumzi na uhai tulivyonavyo vinadhirisha upendo wa Mungu kwetu na tunapaswa kumshukuru”, alisema Mzee Mchome.

Katika ibada hiyo huduma kadhaa zilitolewa ikiwemo sakramenti ya ubatizo na meza ya bwana huku pia familia mbili zikimshukuru Mungu kwa makuu aliyowatendea katika nyakati mbalimbali.

Matukio mbalimbali katika picha ikiwemo ubatizo, jengo la Kanisa linaloendelea kujengwa na familia ya Wasiwasi Mwabulambo mara baada ya ubatizo wa mtoto wao. (Picha na Vincent Mpepo)

Kwaya ya vijana ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe ikihudumu wakati wa ibada Siku ya Jumapili. (Picha na Vincent Mpepo)

Posted in

Leave a comment