Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego akiongea na wananchi wa Mkoa wa Singida katika maadhimisho ya miaka 60 ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mji Mdogo wa Kiomboi, Wilaya ya Iramba, Mkoani Singida.

Na Sylvester Richard, Singida

Watanzania wamekumbushwa kuuenzi muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya kazi kwa maarifa na juhudi ili kujiletea maendeleo.

Wito huo umetolewa na  Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika yaliyofanyika leo maeneo ya kituo cha mabasi kilichopo katika Mji Mdogo wa Kiomboi, Wilaya ya Iramba Mkoani Singida huku wito wake ukiwa ni kufanya kazi zaidi.

Dendego aliwapongeza wasanii waliosherehesha katika maadhimisho hayo zikiwemo kwaya, ngoma za asili, mziki wa kizazi kipya na wachoraji na kuwataka kudumisha utamadini, mila na desturi za mtanzania.

“Sanaa ni furaha, ni afya, ni kazi na ni ajira”, alisema Dendego.

Aidha, katika maadhimisho hayo Dendego alipokea zawadi zilizoandaliwa na baadhi ya wasanii huku pia yeye akikabidhi zawadi kwa makundi mbalimbali kama zilivyoandaliwa na kamati ya maadhimisho hayo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga ambaye alihudhuria maadhimisho hayo aliwaasa wananchi wa mkoa huo kuendeleza mshikamono walionao katika nyanja zote ili kujijenga na kukua kiuchumi kama muungano unavyotaka kwa maendeleo yao na mkoa kwa ujumla.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga akiongea na
wananchi katika maadhimisho ya miaka 60 ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika katika Mji Mdogo wa Kiomboi, Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.

Maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa na kwa ngazi za mikoa na wilaya kwa namna mbalimbali huku yakiongozwa na kauli mbiu isemayo,”Tumeshikamana  na tumeimarika, kwa maendeleo ya taifa letu”.

Posted in

Leave a comment