
Na Vincent Mpepo, OUT
Imeelezwa kuwa ujio wa teknolojia mpya unapaswa kuchukuliwa kwa mapokeo chanya ili isadie katika mifumo ya ujifunzaji na usomaji katika ngazi zote za elimu badala ya kuweka vizuizi vingi katika utekelezaji wake.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda wakati wa kusaini makubaliano kati ya Chuo Kikuu Huriacha Tanzania na Chuo Kikuu cha Masafa cha Sayansi Tumizi cha Uswisi yaliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa chuo hicho Kinondoni jijini Dar es salaam.
Akizungumzia masharti na vizuizi vya wanafunzi kutumia teknolojia mpya ikiwemo ya AI na ChatGPT katika ujifunzaji alisema wakati umefika kwa walimu na wahadhiri kuuliza maswali ambayo yatasaidia kuwashughulisha wanafunzi badala ya yale yaliyozoeleka.
“Muulize maswali yatakayomfanya atafute majibu nje ya AI na ChatGPT, siyo yale ya kujadili au kutoa fasili ya dhana fulani”, alisema Profesa Bisanda.
Profesa Bisanda alisema kwa sasa ufundishaji na ujifunzaji katika elimu ngazi zote unapaswa kuhusisha teknolojia ili kuwafikia wahitaji wengi na kwa muda mfupi lakini pia kurahisisha mchakato wa elimu tofauti ilivyokuwa hapo awali.
“Watu wanaanza kuwa na woga na AI na ChatGPT sawa na kwa waliosoma zamani kidogo ambapo ilikuwa ni kosa la jinai kutumia kikokotoo au kompyuta lakini kwa sasa vimekuwa vitu vya kawaida”, alisema Profesa Bisanda.
Alisema mazingira ya kazi yanapaswa kuendana na mazingira ya kusoma yanayotawaliwa na simu janja na kompyuta badala yake tuwafundishe wanafunzi ili wapate maarifa, ujuzi na stadi za kazi au taaluma wanazosomea.
Afisa Mwandamizi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.Evaristo Mtitu alipongeza jitihanda za chuo hicho katika uwekezaji kwenye Tehama na teknolojia nyingine wezeshi katika masuala ya ujifunzaji na ufundishaji.
“Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinapoingia kwenye mkataba wa maelewano ya kushirikiana kwenye maeneo ya makubaliano inasaidia kubadilishana uzoefu kwenye maeneo ya ushirikiano”, alisema Dkt.Mtitu.
Alisema vyuo vyote vinatakiwa kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia ili kurahisha mchakato wa kujifunza na kufundishia.
Aliongeza kuwa wizara inaamini kuwa teknolojia zinasaidia kuwa na rasimali watu inayoweza kutumika kuwafikia walengwa wengi kwa muda mfupi mfano walimu wa sayansi.
“Teknolojia ikitumika vizuri inatoa nafasi kwa mwanafunzi kushiriki vizuri kwenye kipengele cha ujifunzaji mwenyewe”, alisema Dtk.Mtitu.
Leave a comment