
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson akiongea na waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye jengo la ofisi za madini Mkoa wa Singida Mei 15, 2024
Na Sylvester Richard-Singida
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson amesema serikali itaendelea kushirikiana na waandishi wa habari wa Mkoa wa Singida ili kulinda na kukuza demokrasia nchini ikiwa ni namna ya kuhakikksha kuwa wananchi watapata taarifa kuhusu nini serikali yao ili kuharakisha maendeleo kupitia vyombo vya habari.
Apson aliyasema hayo Mei 15, 2024 wakati wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari kwa Mkoa wa Singida yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano jengo la ofisi za madini Mkoani hapo.
Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wanahabari katika kukuza uchumi wa Taifa na wa Mtu mmoja mmoja na ndiyo maana imetoa uhuru kwa wanahabari kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya kazi za pamoja na sheria zilizowekwa.
Alisema uhuru huo wa vyombo vya habari umeenda sambamba na uhuru wa kufanyika kwa mikutano ya hadhara, vikao na maandamano kwa vyama vyote vya siasa ambapo wanahabari wamekuwa wakiandika habari juu ya mikutano hiyo yenye lengo la kuikosoa na kuishauri serikali iliyopo madarakani.
Mwenyekiti wa Klabu ya wanahabari Mkoa wa Singida (SINGPRESS, Elisante John akitoa taarifa ya Klabu kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi katika maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari Mkoa wa Singida.

Mwenyekiti wa Klabu ya wanahabari Mkoa wa Singida ( SINGPRESS) Elisante John alisema Klabu hiyo ilianzishwa Julai 16, 2023 kwa lengo la kuwaunganisha wanahabri wa Mkao huo ili kufanya kazi chini ya mwamvuli mmoja unaoongozwa na katiba ya Klabu.
Alisema Klabu hiyo ina malengo ya kukuza demokrasia katika jamii kupitia fursa sawa zinazotolewa na vyombo vya habari kwa kutoa taarifa sahihi katika masuala ya elimu kwa makundi mbalimbali ikiwemo wanawake, watoto, vijana, wazee na wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Research and Development organization (ReDO),Hudson Kazonta aliwataka waandishi wa habari kuandika habari mazingira ili kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa Wananchi na utambuzi wa mabadiliko ya tabia nchi.
Maadhimisho hayo yalifanyika kimkoa baada ya kufanyika kimataifa Mei 3, 2024 Jijini Accra Ghana na kitaifa jijini Dodoma yalibebwa na kauli mbiu isemayo ” Uandishi wa Habari na Changamoto za Mabadiliko ya Tabia Nchi” na yamefanyika mara 31 tangu kuanziahwa kwake mwaka 1993.
Leave a comment