Na Grace Mwakalinga, RUKWA

MKUU wa Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa, Lazaro Komba, ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama  wilayani humo kuhakikisha vinadhibiti mienendo inayolenga kuhatarisha ustawi wa watoto  wakiwemo wenye ualbino katika jamii.

Komba alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa kujadili masuala ya  kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto ili kulinda haki ya msingi ya kuishi.

“Imani potofu zimesababisha watoto  wenye ulemavu hususani wenye ualbino kufanyiwa ukatili kama vile kuuawa na kunyofolewa baadhi ya viongo  kwenye miili yao”, alisema Komba.

Kutokana na suala hilo kuripotiwa katika baadhi ya maeneo nchini, Komba alisema tayari wilaya ya Kalambo imeanza kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa  kwa kuweka mikakati kuanzia ngazi ya kitongoji kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kuthibiti vitendo hivyo.

“Ulinzi na usalama kwa watoto wenye mahitaji maalum ni jukumu la kila mmoja wetu, tushiriki kuhakikisha wanalindwa dhidhi ya ubaguzi, unyanyasaji na ukatili wa aina zote ikiwemo mauaji ya watoto wenye ualbino,” alisema Komba.

Aliongeza kuwa tayari baadhi ya wadau wanaendelea kutekeleza jukumu la ulinzi na usalama wa watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo wenye ualbino ambao ni Child Support Tanzania (CST), kukemea na kupinga ukatili na mauaji dhidi ya watu wenye Ualbino yaliyoripotiwa hivi karibuni likidai vitendo hivyo vinajenga hofu na kutishia usalama kwa makundi hayo.

Mratibu wa shirika la Child Support Tanzania (CST), Nemes Temba alisema wananchi wanapaswa kuachana na imani potofu dhidi ya watu wenye ualbino kwa kuwa kuendeleza imani hizo ni kwenda kinyume na maagizo ya vitabu vitakatifu, katiba ya nchi na mikataba mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ambayo inasisizita haki ya kuishi kwa kila mtu bila kujali hali aliyonayo.

Alisema jukumu la jamii ni kufungua fursa za kielimu  na kuweka mazingira rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

“Tulikuwa na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika hapa mkoani Rukwa ambayo ilikuwa mahsusi kujadili na kuangalia masuala ya kuyatekeleza ili kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto wenye mahitaji maalum.

Alisema miongoni mwa miradi wanayotekeleza ni kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapelekwa shule kuanza masomo, uboreshwaji wa miundombinu ya shule  jumuishi zilizopo mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi pamoja na utoaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kulingana na ulemavu wa kila mmoja.

“Kauli mbiu ya mtoto wa Afrika  mwaka huu inazungumzia Elimu Jumuishi kwa watoto izingatie  maadili na maarifa na stadi za maisha inahimiza jamii kutoa elimu yenye usawa kwa watoto wote, wenye ulemavu na wasio na ulemavu,” alisema Temba.

Posted in

Leave a comment