Na Grace Mwakalinga, Dodoma

Wadau wa sekta ya Sanaa wamekutana jijini Dodoma kujadili vikwazo wanavyokabiliana navyo wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Kikao hicho kimefanyika leo jijini humo kimewahusisha wadau ikiwemo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Taasisi ya Hakimiliki (COSOTA) ili kupata suluhu ya masuala yanayohusu haki na maslahi  ya wasanii Tanzania.

Agness Kahamba, msanii wa maigizo nchini amesema wanapitia changamoto nyingi wakati wa kutekeleza majukumu yao na kwamba vinapoandaliwa vikao kama hivyo vinatoa fursa kueleza wanayoyapitia ili kupata suluhu kwa wadau wao.

“Tunatamani kufanya Sanaa yetu kibishara kwa kuuza bidhaa tunazozizalisha ndani na nje ya nchi  lakini  changamoto ni maslahi duni na kukosa mitaji ya kuandaa kazi bora zenye ushindani. Tunaimani Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia ziara alizozifanya mataifa mbalimbali zinaendelea kutangaza sanaa zetu,” amesema Agness.

Mkuu wa Idara ya Sheria wa Kituo cha Kutetea Haki za Wasanii Tanzania (TARO), Ally Ramadhan, amesema wameendesha vikao mbalimbali kuhusu wasanii na kupokea mapendekezo yao.

Amesema baada ya mapendekezo hayo watayachakata na hapo baadae watayapeleka bungeni kwa ajili kufanyiwa maboresho na kutungwa kwa sheria zitakazoendelea kuwalinda wasanii nchini.

Kwa upande wake wakili wa Baraza la Sanaa la Taifa,    Joseph Ndosi, amesema wao kama    walezi wa sekta ya Sanaa wataendelea kuwashauri wasanii namna bora ya kuzalisha kazi zenye ushindani ili kufikia malengo waliyokusudia.

Posted in

Leave a comment