Na Vincent Mpepo, OUT

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeeleezea nia yake ya kuendelea kuenzi uhusiano mwema na vyuo vikuu inavyoshirikiana navyo kutoka Norway kutokana faida ya mahusiano hayo katika ustawi wa watoto wenye mahitaji maalumu kitu kinachoongeza thamani na faraja katika maisha yao.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii ya chuo hicho, Dkt. Dunlop Ochieng wakati wa kuwakaribisha wahadhiri na wanafunzi kutoka Norway iliyofanyika Kinondoni, jijini Dar es salaam leo ambao watakuwa nchini kwa mafunzo ya vitendo kwa muda wa miezi mitatu.

Alisema chuo chake kinathamini uhusiano huo na kwamba kitaendelea kutoa ushirikiano kwa wahadhiri na wanafunzi hao ili kuhakikisha uwepo wao hapa nchini unaendelea kuwa na tija lakini zaidi kutimiza malengo ya uanzishwaji wa ushirikiano huo ambao una maslahi kwa watoto wenye mahitaji maalumu.

“Nitumie fursa hii kueleza kuwa kama wadau wa mradi huu, tupo makini na tutafanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kuwa malengo ya mradi huu yanatimia”, alisema Dkt.Ochieng.

Aidha alieleza kuwa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni taasisi ya umma ambayo inatoa huduma ya elimu kwa njia ya huria na masafa na kwamba inawafikia watu walipo kutokana na uwepo wa vituo vya mikoa nchi nzima.

Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii ya chuo hicho, Dkt.Mariana Makuu alisema mradi huo umeanza kutekelezwa kwa awamu ya pili ambapo awamu ya kwanza ilianza mwaka 2022 hadi mwaka 2024 na kwamba baada ya utekelezaji wenye mafanikio wadau wa pande zote wamekubaliana kuongeza muda wa utekelezaji wake kwa wamu ya pili ambao ni kuanzia mwaka 2025 hadi 2027.

“Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo uliihusisha Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko pekee lakini kwa awamu hii mradi huo huo utaihusiha Shule ya Sinza Maalumu na kufanya idadi ya shule nufaika kuwa mbili”, alisema Dkt.Makuu

Alisema kundi la kwanza la watekelezaji wa mradi awamu ya pili linahusisha wahadhiri na wanafunzi 10 kutoka Norway ambao watafanya kazi na walimu wa shule tajwa kusaidia watoto wenye ulemavu kwa muda wa miezi mitatu.   

Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Sosolojia na Ustawi wa Jamii, Alexander Ndibalema alielezea masuala ya haki, sheria na sera kuhusu watu wenye ulemavu nchini na kwamba kumekuwa na mitizamo tofauti kuhusu hali ya ulemavu ambayo inatafsiriwa kwa milengo ya hasi na chanya.

“Mtizamo hasi ni ule unaomuona mtu mwenye ulemavu kama tegemezi, asiye na msaada na ikihusishwa na laana au mikosi”, alisema Ndibalema.

Kwa upande wake Profesa Mshiriki Karen Reimers ambaye ni msimamizi wa wanafunzi kutoka Norway alisema katika nchi yake kuna sera na sheria madhubuti zinazotekelezwa ili kuhakikisha ustawi wa mtoto hususani mwenye mahitaji maalumu anapata usaidizi wa karibu katika ngazi mbalimbali kutoka kwenye familia hadi shuleni. “Masuala ya watoto yamewekwa kisheria ili kumhakikishia mtoto apate huduma zote muhimu ikiwemo elimu bora na kwenye mazingira rafiki”, alisema Profesa Reimers

Posted in

Leave a comment