Na Ruth Kyelula, Mbulu

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Joseph Mandoo amewataka madiwani na  wakuu wa idara kushirikiana ili kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shule kabla ya muda uliopangwa kuisha.

Mandoo aliyasema hayo wakati akifungua baraza la madiwani katika robo ya pili ya Octoba-Desemba 2024/2025 iliyofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa halmashauri ya Wilaya hiyo huku akitanabaisha kuwa serikali hutumia fedha nyingi katika kuboresha miundombunu ya shule huku idadi ya wanaosoma ni chache.

“Wanafunzi wote waliofaulu Kwenda kidato cha kwanza wahimizwe Kwenda shule”, alisema Mandoo

 Aliwataka maafisa elimu na watendaji wa kata na vijiji kushirikiana ili kufanikisha jambo hilo.

Aidha, aliwakumbusha watumishi hao kujitathimini na kujua sababu zinazochangia shule za msingi za umma kutofanya vizuri katika mitihani ya taifa hivyo kuja na mikakati madhubuti ili kunusuru hali hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Abubakar Kuuli alisema uandikishaji wa wanafunzi wa elimu msingi na wanafunzi wa sekondari wanaoripoti bado hauridhishi licha ya kuwashirikisha watendaji wa kata kwenye zoezi hilo.

“Hadi sasa ni asilimia 51 ya wanafunzi wa elimu msingi ndio wameandikishwa huku asimilia 52 ndio wameripoti shule kwa upande wa sekondari.

Akitoa ripoti ya ufaulu kwa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2024 alisema ufaulu umefika asilimia 98.7 ambapo umeongezeka kwa asilimia 3.7 kutoka matokeo ya mwaka 2023.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay aliwapongeza madiwani na wakuu wa idara wote kwa kazi kubwa kufuatia ufaulu huo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu, Paulo Bura aliutaka uongozi wa  Halmashauri kuhakikisha wanafunzi wanaripoti mapema katika Shule ya Sekondari ya Eshkesh huku pia akitoa makataa ya kuripoti kuwa March 31, 2025.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Mbulu, Melkiadi Nar aliwashukuru viongozi kwa kazi kubwa  wanayofanya huku pia akitoa rai ya kuongezwa kwa shule za sekondari za kidato cha tano (5) na cha sita(6).

Posted in

Leave a comment