Na Martha Joachim,Tanga

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar, imelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa utendaji kazi madhubuti katika usimamizi wa sheria na kanuni za usalama, ulinzi na utunzaji mazingira  wa usafiri majini.

Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Yahya Rashid Abdulla, walipotembelea Ofisi za TASAC mkoani Tanga na kufanya kikao na watumishi wa TASAC pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).

“Tumefurahishwa na utendaji kazi mzuri wa TASAC katika udhibiti na usimamizi wa safari kwa njia ya maji hasa katika Bandari ya Tanga”, alisema Mhe. Abdulla

Alisema usimamizi mzuri umesaidia kurahisisha usafiri kati ya Tanzania Bara na Visiwani kwa eneo la mwambao ambalo lilikua na changamoto kubwa ya usafiri kwa njia ya maji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu TASAC, Meneja Mafunzo na Utoaji vyeti Mhandisi Lameck Sondo ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kuendeleza weledi, ufanisi na ushirikiano na taasisi nyingine katika kudhibiti na kusimamia shughuli za usafiri majini kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mhandisi Sondo alisema Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeendelea na utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa usalama wa usafiri katika Ziwa Victoria  ambao ni mradi unaoshirikisha nchi za Uganda na Tanzania katika kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, ameeleza kuwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imefanikiwa katika ukaguzi wa meli za kigeni pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu hayo kwa weledi.

Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi, Mawasiliano, Ardhi na Nishati Zanzibar ilifanya ziara hiyo mwanzoni mwa wiki hii ili kujifunza utendaji kazi na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na TPA mkoani Tanga ikiwemo Bandari za Tanga, Pangani na Kipumbwi.

Posted in

Leave a comment