Na Tabia Ally, DSM

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) itashirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania katika utekelezaji wa mikakati ya kuimarisha usalama barabarani ili kupunguza ajali.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamanda SACP William Mkonda katika Ofisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) zilizopo Mtendeni, Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii.

Kamanda SACP William Mkonda alisema lengo la ziara hiyo kujadili na kuweka mikakati ya ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na Jeshi la Polisi Tanzania ikiwa ni maandalizi ya Kikao Kazi cha Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa Mikoa na Wilaya kinachotarajiwa kufanyika jijini Dodoma Februari 2025.

“Kikao hicho kinalenga kuweka mikakati madhubuti ya kupunguza ajali za barabarani na madhara yake kwa watumiaji wa barabara”, alisema Kamanda SACP Mkonda.

Alisema kuna umuhimu wa elimu ya bima kwa makamanda wa polisi wa usalama barabarani wa wilaya na mikoa hususani katika uhakiki wa bima kupitia mifumo rasmi.

Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware alisema hatua ya kuunganisha mifumo ya TIRA na Polisi itasaidia upatikanaji wa taarifa za ajali mara zinapotokea.

“Hatua hii inalenga kuhakikisha waathirika wa ajali wanapata fidia zao kwa haraka, kwani taarifa za ajali zitasomwa moja kwa moja na kampuni za bima kupitia mfumo wa TIRA”, alisema Kamishna Dkt.  Saqware.

Mkutano makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani wa mikoa na wilaya utafanyika jijini Dodoma wiki ya tatu ya Mwezi Februari 2025 huku Mkuu wa Mkoa huo, Bi. Rose Senyamule anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

Posted in

Leave a comment