Na Vincent Mpepo, Kwembe

Vijana wa kike na kiume nchini wametakiwa kujishughulisha na kuzalisha kipato kitakachowasidia hata kama hawakupata ajira kwenye mifumo rasmi iwe serikalini au sekta binafsi.
Wito huo umetolewa na Mwalimu Bupe Mwabenga wakati akihubiri katika ibada siku ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe na kusisitiza kuwa bado wana wajibu kama wanajamii kujibiidisha ili kufikia maono ya ndoto zao.
Alisema kufanya kazi na kuzalisha baada ya kuhitimu masomo kutawasaidia kuepuka utegemezi kwa wazazi na walezi ambao wamejitoa kuwafikisha hatua hiyo.
Alisema vijana wanatakiwa kujisimamia katika maisha na kuwakumbusha kujenga mahusiano mema na Mungu na wanajamii wanaowazunguka.
Aidha,aliwapongeza washarika wa Mtaa huo kwa ujenzi wa nyumba ya Mungu huku akitanabaisha kuwa ujenzi siyo rahisi na kuwatia moyo kwa kuwa wanafanya jambo jema machoni pa Mungu.
“Kujenga siyo rahisi iwe kwenye ngazi ya familia au taasisi”, alisema Mwalimu Mwabenga.
Mwinjiisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava alimshukuru Mwalimu Mwabenga mafundisho mazuri kwa kuwa kilichofundishwa kimegusa maeneo mengi na kwa washarika wa rika zote kiasi kwamba kila aliyehudhuria amepata kwa sehemu yake.
Aidha, aliwakumbusha washarika kuhusu harambee ya kuchangia kituo cha Udiakonia cha watoto wenye mahitaji maalumu ambacho kitahamishwa kutoka Kijichi Kwenda Kitopeni-Bagamoyo kutokana na changamoto za kimazingira mahali kiliposasa.
“Tuhusike kwenye harambee hii kama sehemu ya kumshukuru Mungu kwa kutujalia Watoto”, alisema Mwinjisti Mzava.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mtaa huo, Exaud Mchome aliwashukuru washarika kwa kuendelea kuchangia ujenzi wa kanisa huku akiwataka kutokata tamaa na kazi hiyo.
Alisema kazi inayofuata ni kutengeza mifumo ya uwekaji paa ambapo kuna uhitaji wa matofali ya kawaida 5,000, ya ruva 1500 na mifuko ya saruji ipatayo 1,500.
Leave a comment