Mwalimu Bupe Mwabenga akifundisha  wakati ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe jijijini Dar es salaam

Na Vincent Mpepo, Kwembe

Wanandoa wamekumbushwa kuishi kwa kadiri ya mpango wa maagizo ya Mungu ili kuepuka migogoro inayotokana na mwingiliano wa majukumu kati yao.

Wito huo umetolewa Jumapili  na Mwalimu Bupe Mwabenga wakati akifundisha katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe na kubainisha kuwa sababu mojawapo ya migogoro katika ndoa ni kwa baadhi ya wanandoa kutoishi kwa utaratibu uliowekwa na Mungu.

Alisema si vibaya kwa wanandoa kuamua kusaidiana majukumu lakini kusaidiana huko kuwe katika utaratibu ambao unatambua haki na wajibu wa kila mwanandoa ili kupata tafsiri sahihi ya anayesaidia na anayesaidiwa.

“Wanawake wamejengewa uwezo, wamewezeshwa na wanatambua haki zao hatahivyo bado haiwapi nafasi ya kuwa wanaume”, alisema Mwalimu Mwabenga.

Aliikumbusha jamii kuwa makini na mafundisho ya mitandaoni kuhusu masuala ya ndoa kwani siyo kila maudhui yanalenga ustawi wa ndoa badala yake ni upotoshaji ambao matokeo yake ni kuwa na ndoa zenye migogoro ambayo inazorotesha ustawi wa taasisi muhimu ya ndoa.

Akizungumzia malezi ya watoto ambao kila familia inajaaliwa alisema huwa wanakuja na changamoto hivyo aliwataka wazazi na walezi kutokawakatia tamaa watoto wao kwa kuwa watoto hao wamebeba kusudi la Mungu.

“Malezi ya watoto huwa yanaambatana na changamoto mbalimbali katika hatua za malezi tangu utoto hadi utu uzima”, alisema Mwalimu Mwabenga.

Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwajulisha washarika kuhusu ujio wa vijana zaidi ya mia mbili (200) ambao walikuja siku hiyo kwa ajili ya mkutano kwa ajili ya mipango yao ya shughuli za vijana.

“Niliipokea taarifa ya mkutano huo kwa kwa shukrani japo nlijiuliza ikiwa Kwembe imeonwa kuwa yaweza kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa kama huo”, alisema Mwinjilisti Mzava.

Mwenyekiti wa Kwaya Kuu ya Mtaa huo, Jonas Mnkeni aliwajulisha washarika wa mtaa huo kuhusu uzinduzi wa albamu ya kwanza ya picha mjongeo (video) ambao unatarajiwa kufanyika Jumapili ya Tarehe 23 Februari 2024.

“Ninaomba washarika mtuunge mkono ili kuendeleza kuitangaza injili kupitia albamu hii ya kwanza ya toleo la video”,alisema Mnkeni.  

Sehemu ya jengo la Kanisa Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe ambalo linaendelea kujengwa, (Picha zote na Michael Mwambage).

Posted in

Leave a comment