
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni (kushoto). Kulia ni Katibu wa Baraza Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli ( PURA) Ebeneza Mollel wakati wa Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro.
Morogoro
Serikali imeitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuendelea kuvutia uwekezaji katika vitalu vilivyo wazi vya mafuta na gesi asilia ili kuongeza kiasi cha nishati hiyo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa mwanzoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga wilayani Morogoro, Mkoa wa Morogoro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kilicholenga kujadili mipango na bajeti ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Alisema mamlaka hiyo ikifanikiwa kuvutia wawekezaji wa utafutaji wa mafuta na gesi nchi itaongeza ugunduzi wa rasilimali hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kufikia futi za ujazo wa gesi inayopatikana nchini.
“Mkiendelea kuvutia uwekezaji kupitia Duru ya Tano ya kunadi vitalu itakayozinduliwa mwezi Machi mwaka huu pamoja na faida zilizopo mtakuwa mmeendeleza jitihada za serikali kuifungua Tanzania kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi”, Alisema Kapinga.
Alisema wizara inatambua umuhimu wa tukio la Duru ya Tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini pamoja na kutambua kazi kubwa ambayo imekwishafanyika kuelekea uzinduzi wa tukio hilo muhimu.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukizungumzia ugunduzi wa futi za ujazo trilioni 57.54 pekee wakati umefika ili kuongeza ugunduzi wa rasilimali hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa”,Alisema Kapinga
Aidha, aliupongeza uongozi wa uongozi wa PURA kwa kuendelea kuwashirikisha watumishi wake katika kujadili, kupanga na kupitisha mipango na bajeti ya taasisi hiyo kwa uwazi kupitia baraza hilo ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Majadiliano ya Pamoja katika Utumishi wa Umma.
Alisema kufanyika kwa vikao hivyo ni ishara tosha ya utawala bora mahala pa kazi kwa kuwa watumishi wanapata fursa ya kuchangia mawazo yao kuhusu uendeshaji wa taasisi hivyo kuendelea kuwa ni sehemu muhimu ya taasisi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni, alisema duru ya tano (5) ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na
gesi asilia nchini inatarajiwa kuzinduliwa mwezi Machi, 2025 Jijini Dares salaam wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EAPCE’25).
Alisema PURA itaendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa gesi asilia katika vitalu mbalimbali nchini ili kuhakikisha watanzania wazawa wanashirikishwa kikamilfu kwenye miradi mbalimbali ya mkondo wa juu wa petroli nchini.

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (katikati) katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli( PURA) wakati wa Kikao cha Baraza hilo kilichofanyika Tarehe 18 na 19 Februari 2025, mkoani Morogoro. Kushoto Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Mhandisi. Charles Sangweni.
Leave a comment