Na Vincent Mpepo, Kwembe

Eneo ambalo lililopangwa kutumika kama soko limebadilishwa matumizi na kuwa machinjio na mnada wa mifungo kitu kinachotajwa kitaongeza idadi ya wasafiri kuja na kutoka mtaani hapo na kuchochea maenedeleo ya Mtaa wa Kwembe Ubungo jijini Dar es salaam.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwembe Rajabu Koba wakati wa mkutano wa wa kwanza wa wananchi uliofanyika jana katika ofisi za mtaa huo ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa huku kubadili matumizi kwa eneo la soko na urasimishaji ardhi zikiwa ni ajenda ambazo zilivuta makini ya wananchi wa mtaa huo.

Koba alisema maamuzi ya kubadili matumizi ya eneo hilo kuwa machinjio na mnada limefikiwa kufuatia vikao na kamati mbalimbali za mtaa huo na limewasilishwa kwa diwani ili kwenda kwenye ngazi za juu kwa maamuzi zaidi na kwamba tangu lilipofanywa kama soko hakuna kilichofanyika mpaka sasa.

Alisema maamuzi ya kubadili eneo matumizi limezingatia vitu vingi ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ambayo itavutia wafanyabiashara ya usafirishaji kama daladala kuja na kutoka kutokana na abiria wakakaokuja kwa shughuli mbalimbali za kibiashara.

“Ili kupata abiria wa kutosha lazima kuwe na eneo ambalo litavuta watu kuja na kutoka huku pia miundombinu yetu ikiwa imeboreshwa”, alisema Koba.

Aidha aliwataka wananchi wa Mtaa huo kuchangamkia fursa za ujasiriamali katika mradi mkubwa unaotarajiwa kuanza hivi karibuni katika eneo la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila.

“Wanacnhi wa maeneo jirani wajiandae kwa kazi mbalimbali ikiwemo vibarua na ujasiriamali kama mama lishe katika mradi huo”, alisema Koba.

Alisema fursa hizo ni matokeo ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya juu kwa Mageuzi ya Kichumi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unahusisha ujenzi wa majengo sita ambapo tayari kandarasi zimekwishatolewa kwa makampuni mawili na utagharimu kiasi cha dola za kimarekani milioni 30.5.

Mtendaji wa Mtaa huo, Kennedy Kuwendwa alisema Wananchi wa mtaa huo wajenge utaratibu wa kwenda ofisini ili kupata taarifa sahihi na kutoa taarifa mbalimbali kwa kero ili zifanyiwe kazi badala ya kupeana maneno mitaani ambayo wakati mwingine hayana uhakika.

“Ninawashukuru Wananchi wa mtaa huu na nitoe rai ikiwa kuna jambo hulielewi njoo ofisini utasaidiwa kupata ufumbuzi”, alisema Kennedy.

Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kwembe, Bi Ramla Mustafa aliwakumbusha wananchi wa mtaa huo kuhusu fursa za mikopo asilimia kumi (10%) ambayo hutolewa na serikali kupitia Halmashauri ya Ubungo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Vigezo vya kuapata mikopo hiyo ni mtu mwenye umri wa miaka 18 hadi 45 na mwenye Uwezo wa kufanya kazi na kujiingizia kipato, alisema Bi Ramla.

Mkutano huo ulikuwa na ajenda nyingine ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Kwembe, Ujenzi wa Kituo cha Polisi, Suala la Ulinzi Shirikishi na umaliziaji wa ofisi ya mtaa huo.

Hata hivyo uchunguzi wa mwandishi umebaini kutokuwepo kwa hamasa ya kutosha ya Wananchi kushiriki katika mikutano ya mtaa huo suala linalotajwa limetokana na taarifa kutowafikia Wananchi.

Posted in

Leave a comment