Na Vincent Mpepo, Kwembe

Wataalamu mbalimbali wanaoishi na kufanya kazi katika Mtaa wa Kwembe Ubungo Jijini Dar es salaam wamebainisha fursa na changamoto mbalimbali za kimaendeleo katika Mtaa huo huku huduma za jamii na miundombinu zikitajwa.

Hayo yamejitokeza katika mkutano wa kwanza wa serikali ya Mtaa uliofanyika jana katika ofisi za mtaa huo jana huku fursa na changamoto mbalimbali zikitajwa katika kuchochoea au kurudisha nyuma maendeleo ya Mtaa huo.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwembe Rajabu Koba alisema ni wakati sasa Wananchi kuamka kuunganisha nguvu zao, kwa kuishauri serikali yao kwa hoja madhubuti ili kwa ushirikiano zifanyiwe kazi kwa manufaa ya Mtaa huo.

Alitaja vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi Kwembe ili kupunguza mrudikano wa watoto katika madara yaliyopo ambayo hayatoshi na Kituo cha polisi ili kuimarisha ulinzi na usalama.

“Vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama kupitia ulinzi shirikishi, kubadili matumizi ya eneo la soko kuwa machinjio na mnada wa mifugo”, alitaja Koba.

Aliongeza vipaumbele vingine kuwa ni kukamilisha ujenzi wa ofisi ya serikali ya Mtaa huo na masuala ya urasimishaji ardhi katika Mtaa huo.

Akizungumzia ajenda ya ulinzi na usalama aliwataka Wananchi kwenye mitaa na zone mbazo bado hazijaanzisha ulinzi shirikishi kufanya hivyo ili kutowapa wezi na wadokozi fursa ya kuwaibia.

“Ulinzi shirikishi ni kwa ajili ya kuwanyima fursa wezi na wadokozi kujipatia kipato au faida kwa kazi isiyo halali”, alisema Koba.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwembe, Lwitiko Mwakisole alisema changamoto kubwa inayoikabili shule yake ni uhaba wa madarasa ya kusomea na madawati ambao hauendani na idadi ya wanafunzi waliopo matokeo yake bbadhi ya wanafunzi kulazimika kusomea nje na kukaa chini.

“Shule ya Msingi Kwembe ina wanafunzi zaidi ya 2000 huku miundombinu ya madarasa tuliyonayo ni 12 tu”, alisema Mwalimu Mwakisole.

Aliwaasa wazazi kutembelea shule yao ili kujionea uhalisia wa kinachosemwa ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo kwa maslahi ya kizazi cha wanakwembe.

Akizungumzia malezi, Mwakisole alisema kumekuwa na changamoto za malezi katika jamii na familia kutokana na baadhi ya walezi na wazazi kutokubali watoto wao kuadhibiwa suala ambalo linaleta mustakabali mbaya kwa jamii na kizazi cha sasa.

“Kimsingi, tukubali kuna changamoto za malezi zinazotokana na malezi mabovu katika familia zetu hivyo kusababisha watoto wenye tabia mbaya”, alisema Mwalimu Mwakisole.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Amani, Dkt.Nikodemus Ngwembe aliwataka Wananchi wa mtaa huo na mitaa ya jirani kukitumia kituo hicho ambacho kinapandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya kutoka Zahanati kwa kuwa mindombinu inaboreshwa ili kuendana na hadhi hiyo.

“Kwa sasa kituo chetu kimejenga jengo la wazazi kwa gharama ya Tsh milioni 300 ambalo lina vitanda 30 huku vitanda vya chumba cha wazazi ni 10inatoa huduma masaa 24 na ina vitanda 10”, alisema Dkt. Ngwembe.

Alisema kwa sasa kituo hicho kinaendelea na ujenzi wa wodi ya upasuaji na kwamba kitahudumia kata ya Kwembe na Kibamba huku mashine na mitambo mingine ikiwemo Utra-Sound ikiwa mbioni kuletwa katika kituo hicho ambayo imegharimu Tsh milini 22.

Akizungumzia masuala ya urasimishaji ardhi katika Mtaa huo, Mkandarasi Demetrius Sangu alisema tangu zoezi hilo lianze tayari wameshatambua viwanja 4015 na viwanja vilivyopangwa kwa mujibu wa ramani ya mipango miji ni 6207 wakati viwanja vilivopata namba za ploti ni 2116 wakati ni viawanja 20 pekee ambavyo bado havijapandwa mawe.

“Changamoto za kuendelea na zoezi hili ikiwemo upandaji wa mawe unatokana na uhaba wa fedha”, alisema Mkandarasi Sangu.

Aidha, uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebani kuwa kuchelewa kwa zoezi la urasimishaji kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuzorota kwa uchangiaji wa fedha kwa wananchi kutokana na kukosa hamasa au matamko mbalimbali ya serikali kwa nyakati zilizopita.

Posted in

Leave a comment