
Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa wa Kwembe, Emeline Mzava na Mtendakazi Anna Mauki pamoja na wanakwaya wa kwaya hiyo wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa Albamu ya kwanza ya Kwaya Kuu ya Mtaa huo Siku ya Jumapili, (Picha na Vincent Mpepo).
Na Vincent Mpepo, Kwembe
Viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe wamewashukuru washarika wa Mtaa huo kwa namna wanavyojitoa katika kazi ya Mungu.
Shukrani hizo zimetolewa na viongozi hao wakati wa ibada ya Jumapili katika vipindi mbalimbali huku wakitanabaisha kwamba wanajisikia amani kufanya kazi katika Mtaa huo.
Akizungumza wakati wa ahadi za changizo za ujenzi wa kanisa unaoendelea Mtaani hapo, Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava alisema anawiwa kumshukuru Mungu kwa ajili ya washarika hao kwa namna wanavyojitoa katika shughuli mbalimbali kanisani hapo na zaidi anawaombea ili utumishi wao uendelee.
“Sina cha kusema zaidi ya kumshukuru Mungu kwa ajili yenu,” alisema Mwinjilisti Mzava.
Aidha aliwakumbusha washarika wa mtaa huo kuhusu changizo la ujenzi wa nyumba ya watoto wenye mahitaji maalumu huko Kitopeni-Bagamoyo ambayo inahamishwa kutoka Mtoni kijichi.
Akiongezea uzito wa kauli hiyo, Mtendakazi wa Mtaa huo Anna Mauki alisema anaguswa na namna washarika wanavyowajibika.
Aidha katika mahubiri yake alizungumzia umuhimu wa neno la Mungu sawa na silaha ambayo hutumika kujilinda dhidi ya adui akisimamia kichwa kisemacho ‘Neno ni Silaha Imara’ na kwamba neno la Mungu ni pumzi inayoishi na imeandikwa kwa watu ambao wamepewa uwezo na Mungu.
“Tuanze kuliishi neno katika familia zetu kwa kusali pamoja asubuhi, mchana na usiku,” alisema Mtendakazi Anna.
Alisema kuwafundisha watoto neno Mungu ni urithi mkubwa zaidi ya aina ya urithi mwingine kwakuwa mtu akijawa na wingi wa neno la Mungyu atapata kibali na kukubalika katika mazingira ambayo kibinadamu asingeweza.
“Wakati mwingine tumekuwa na mashaka kuhusu utendaji wetu kwa baadhi ya vitu jambo muhimu ni kuamini kuwa aliyetupa uhai ndiye anayetuwezesha,” alisema Bi Anna.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Mtaa huo, Exaud Mchome aliwashukuru washarika kwa kuendelea na michango kwa ajili ya ujenzi na alitangaza kuanza kwa awamu ya uchangiaji kwa kwanza ambayo ni Februari mpaka Mei na awamu ya pili itaanza Mwezi Juni hadi Disemba 2025.

Baadhi ya Wafadhiri wa Kwaya Kuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe wakiunga mkono kwa kununua albamu ya Kwanza ya Video ya kwaya hiyo Jumapili, (Picha na Vincent Mpepo).
Leave a comment