Na Vincent Mpepo, Kwembe
Serikali ya Mtaa wa Kwembe imeishukuru serikali kwa namna inavyojali wananchi kupitia uboreshaji wa miundombinu na huduma za afya.
Hayo yamebainishwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwembe Rajabu Koba wakati wa mkutano wa wa Kwanza na wa wananchi wa Mtaa huo uliofanyika hivi karibuni katika ofisi za mtaa huo ambapo masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo pongezi kwa serikali.
Koba alisema serikali imetoa pesa ili kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo katika Mtaa wake na kupitia wataalamu wa sekta mbalimbali mtaani kwake.
Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Amani, Dkt.Nikodemus Ngwembe alibainisha maboresho mbalimbali yaliyofanyika na yanaendelea kufanyika katika Kituo hicho cha Afya ambayo yanafanya kipandishwe hadhi kutoka Zahanati ili kuendana na hadhi hiyo.
“Kwa sasa kituo chetu kimejenga jengo la wazazi kwa gharama ya Tsh milioni 300 ambalo lina vitanda 30 huku vitanda vya chumba cha wazazi ni 10 na tunatoa huduma masaa 24”, alisema Dkt. Ngwembe.
Alisema kwa sasa kituo hicho kinaendelea na ujenzi wa wodi ya upasuaji na kwamba kitahudumia kata ya Kwembe na Kibamba huku mashine na mitambo mingine ikiwemo Utra-Sound ikiwa mbioni kuletwa katika kituo hicho ambayo imegharimu Tsh milioni 22.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kwembe, Lwitiko Mwakisole alisema changamoto kubwa inayoikabili shule yake ni uhaba wa madarasa ya kusomea na madawati ambao hauendani na idadi ya wanafunzi waliopo matokeo yake badhi ya wanafunzi kulazimika kusomea nje na kukaa chini.

“Shule ya Msingi Kwembe ina wanafunzi zaidi ya 2000 huku miundombinu ya madarasa tuliyonayo ni 12 tu”, alisema Mwalimu Mwakisole.
Aliwaasa wazazi kutembelea shule yao ili kujionea uhalisia wa kinachosemwa ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo kwa maslahi ya kizazi cha wanakwembe.
Akizungumzia malezi, Mwakisole alisema kumekuwa na changamoto za malezi katika jamii na familia kutokana na baadhi ya walezi na wazazi kutokubali watoto wao kuadhibiwa suala ambalo linaleta mustakabali mbaya kwa jamii na kizazi cha sasa.
“Kimsingi, tukubali kuna changamoto za malezi zinazotokana na malezi mabovu katika familia zetu hivyo kusababisha watoto wenye tabia mbaya”, alisema Mwalimu Mwakisole.
Aliwataka wazazi na walezi wa mtaa huo kushirikiana na walimu ili kuendelea kuboresha tabia na maadili ya watoto kwa faida ya kizazi kijacho na taifa kwa ujumla.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kwembe, Bi Ramla Mustafa aliwakumbusha wananchi wa mtaa huo kuhusu fursa za mikopo asilimia kumi (10%) ambayo hutolewa na serikali kupitia Halmashauri ya Ubungo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.
“Vigezo vya kuapata mikopo hiyo ni mtu mwenye umri wa miaka 18 hadi 45 na mwenye uwezo wa kufanya kazi na kujiingizia kipato”, alisema Bi Ramla.
Aidha aliwataka Wananchi kutosikiliza maneno ya mtaani badala yake waende ofisini kwa maelezo na maelekezo sahihi.

Posted in

Leave a comment