Na Vincent Mpepo, OUT

Jamii imetakiwa kuwatambua na kuwathamini watoto wenye mahitaji maalumu ili kuwajengea uwezo na kujiamini kitu kitakachosaidia ustawi wao kimalezi, kimakuzi na kitaaluma.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dkt. Mariana Makuu wakati wa tathimini ya mradi wa NOREC unaohusisha wahadhiri, wakufunzi na wanafunzi wa vyuo Tanzania na Norway iliyoanza jana katika ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es salaam.

Alisema jamii inatakiwa kutambua haki za watoto wenye mahitaji maalumu na kujua kuwa watoto hao ni binadamu kama binadamu wengine wana roho na uhai na wakithaminiwa hali zao zinabadilika.

“Tumeshuhudia pale Uhuru Mchangayiko watoto tulioanza nao katika mradi huu wa NOREC sasa hivi wameshaanza madarasa ya kawaida na wengine wamefaulu kwenda sekondari”, alisema Dkt.Makuu

Alisema watoto wenye mahitaji maalumu wanahitaji kuthaminiwa kwani wakipata huduma hizo zikiambatana na upendo wanaweza kusonga mbele na kufanya vitu vya tofauti kwa jamii zao.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Mtumishi wa Taasisi ya Mafunzo ya Afya na Sayansi Shirikishi Huruma iliyopo Kilimanjaro, John Kihine alisema Tanzania tuna sera nzuri zinazowahakikishia ulinzi watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo watoto wenye ulemavu shida ni utekelezaji.

Alitolea mfano sera ya elimu inayosema mtoto hatakiwi kuchapwa viboko zaidi ya vinne na anayetakiwa kufanya hivyo ni Mwalimu Mkuu na mwalimu mwingine akimchapa anapaswa kuandika kwa nini amemchapa na akahoji ikiwa sera ingesema mtoto hatakiwi kuchapwa badala yake atafutiwe adhabu nyingine ingefuatwa.

“Jambo lingine ambalo tunaweza kulifanya ili kuleta matokeo mazuri kwa watu wenye ulemavu ni kuhakiksha tunaendelea kuwa na miundombinu mizuri itakayofanya wao kupata huduma stahiki kama elimu na afya”, alisema Kihine.

Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Leah Makundi aliitaka jamii kuendelea kuwathamini watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwa wanastahili kupata haki zao kama watoto wengine.

Alisema anatambua juhudi za serikali katika kuhakiksha inatengeneza mazigira rafiki kwa jamii hususani watoto wenye mahitaji maalumu na kuitaka kuajili walimu wa mahitaji maalumu ili kuwapunguzia walimu mzigo wa kufundisha watoto wengi ikwemo wenye ulemavu.

“Patandi tunazalisha walimu wengi sana lakini wanaoajiriwa ni wachache huku uhitaji wao kwenye shule za elimu maalumu ni mkubwa ili watoto wenye mahitaji maalumu wapate haki yao”, alisema Mkufunzi Makundi.

Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Dunlop Ochieng, alisema utekelezaji wa makubaliano ya mradi huo wa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi na vyuo vikuu vya Norway yanaenda sanjali na matakwa ya mikataba ya kimataifa na sheria za nchi kuhusu haki za watoto na watu wenye ulemavu.

Posted in

Leave a comment