

Na Vincent Mpepo, OUT
Wahadhiri, wakufunzi na wanafunzi katika taasisi za elimu ya juu wameishauri serikali kuhusu utekelezaji wa sera, kanuni na haki za watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo watoto wenye ulemavu ili kufanya maisha yao yawe mazuri.
Ushauri huu umetolewa na wataalamu hao wakati wa tathimini ya mradi wa NOREC unaohusisha wahadhiri, wakufunzi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi na vyuo vikuu vya Norway iliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dkt. Mariana Makuu alisema watoto wenye mahitaji maalumu wanahitaji kuthaminiwa kwani wakipata huduma hizo zikiambatana na upendo wanaweza kusonga mbele na kufanya vitu vya tofauti kwa jamii zao.
“Alisema jamii inatakiwa kutambua haki za watoto wenye mahitaji maalumu na kujua kuwa watoto hao ni binadamu kama binadamu wengine wana roho na uhai na wakithaminiwa hali zao zinabadilika”, alisema Dkt.Makuu.
Alisema kupitia mradi huo wa NOREC kumekuwa na mabadiliko chanya hususani katika Shule ya Msingi Uhuru Mchangayiko ambapo watoto walioanza nao katika mradi hivi sasa wameanza madarasa ya kawaida na wengine wamefaulu kwenda sekondari.
Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Leah Makundi aliikumbusha kuajili walimu wa mahitaji maalumu ili kuwapunguzia walimu mzigo wa kufundisha watoto wengi ikwemo wenye ulemavu.
Alisema vyuo vya elimu maalumu ikwemo Patandi vinazalisha walimu wengi lakini wanaoajiriwa ni wachache huku uhitaji wao kwenye shule za elimu maalumu ni mkubwa ili watoto wenye mahitaji maalumu wapate haki yao.
“Natambua juhudi za serikali katika kuhakiksha inatengeneza mazigira rafiki kwa jamii hususani watoto wenye mahitaji maalumu niwaombe waangalie na upande wa ajira ”, alisema Bi Makundi.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Anita Kway alizungumzia changamoto za upatikanaji elimu kwa watoto wenye ulemavu ambazo zinatokana na muktadha, upungufu wa vifaa saidizi na kukosekana kwa kwa walimu wenye maarifa ya ufundishaji watoto wenye ulemavu mchanganyiko.
“Changamoto nyingine ni uwiano usio sawa kati ya wanafunzi na walimu, ukosefu wa rasilimali watu na fedha pamoja na miundombinu stahiki kwa watoto wenye ulemavu”, alisema Bi.Kway
Mwakilishi wa wanafunzi kutoka Norway, Tora Rosnes alisema uwepo wao nchini Tanzania wamejifunza vitu vingi ikiwemo ari na utayari wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu kujifunza na namna walimu wanavyoweza kuchangamana na wanafunzi wakati wa kufundisha.
“Changamoto nilizokutana nazo ni pamoja na utofauti wa kiutamaduni kati ya nchi yangu na hapa Tanzania hususani Lugha na mimi sijui Kiswahili”, alisema Tora.
Aidha alisema anafurahishwa na uwepo wa nyimbo nyingi na michezo mbalimbali ya watoto na kitu cha pekee anachoondoka nacho ni furaha.
Leave a comment