Washiriki wa tathimini ya mafunzo kwa vitendo unaohusisha wahadhiri, wakufunzi na wanafunzi wa Tanzania na Norway uliofanyika jana katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (Picha na Vincent Mpepo, OUT).

Na Vincent Mpepo, OUT

Utekelezaji wa mradi wa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi na vyuo vikuu vya Norway umeonesha mafanikio chanya ya namna watoto wenye mahitahji maalumu wanavyoweza kusaidiwa ili kuboresha maisha yao.

Hayo yamebainishwa na washiriki wa mjadala wa tathimini ya mafunzo kwa vitendo unaohusisha wahadhiri, wakufunzi na wanafunzi wa Tanzania na Norway uliofanyika leo katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania huku mafaniko na changamoto kadhaa zikiainishwa ili kufikia malengo ya mradi huo.

Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Dunlop Ochieng alisema ushirikano huo umeleta mafaniko chanya na kwamba chuo chake kinathamini juhudi na mchango wa ushirkiano huo unaolenga kuboresha maarifa na ujuzi wa namna ya kuwadumia watoto wenye mahitaji maalumu.

“Ninatambua kazi nzuri inayofanyika katika shule za Uhuru Mchanganyiko na Sinza Maalumu”, alisema Dtk.Ochieng.

Alisema utekelezaji wa makubaliano ya mradi huo yanaenda sambamba na matakwa ya mikataba ya kimataifa na sheria za nchi kuhusu haki za watoto na watu wenye ulemavu.

Alisema ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo umesaidia kuwapa wahadhiri na wanafunzi wa kitanzania na Norway jukwaa la kutekeleza kwa vitendo wakifundishacho na kusoma darasani katika mazingira halisi ya jamii kwa pande zote mbili.

Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Dkt. Mariana Makuu alisema ushirikano huo unasaidia kupatikana kwa suluhu za changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu kwa kubadilishana uzoefu kati ya wageni na wenyeji.

“Kwa kawaida huwa tunafanya tathimini ili kuona kama wahusika wameweza kutekeleza malengo ya mradi na ikiwa kuna changamoto tuone namna ya kutatua ili malengo ya mradi yafanikiwe”, alisema Dkt.Makuu.

Aidha alisema bado kuna umuhimu wa uwepo wa maafisa ustawi wa jamii kwenye shule za msingi na sekondari ili wasaidiektika utoaji huduma kwa watoto kwa kuwa walimu wana majukumu ya kutekeleza mtaala na hawezi kuangalia ustawi wa watoto kwa undani.

Mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Leah Makundi alisema kutokana na ushiriki wake kwenye mradi huo amejifunza vitu vingi ikiwemo mbinu mbadala za kuwafundisha walimu wanafunzi bila kuwaadhibu watoto.

“Wametusaidia namna mbalimbali mbadala za kuepuka matumizi ya fimbo kama njia pekee ya kumuonya na kumuelekeza mtoto”, alisema Bi Makundi.

Alisema wao wanatamani na wanajitahidi sana sisi tufundishe walimu waache kuwachapa watoto na tutumie mbinu mbadala katika kufundisha.

Mwakilishi wa wanafunzi kutoka Norway, Erlend Hoibo alisema uwepo wao nchini Tanzania wamejifunza vitu vingi ikiwemo namna walimu wanavyotumia rasilimali kidogo walizonazo ili kufundisha watoto wenye mahitaji maalumu kitu ambacho kinaonesha upendo na kujali.

“Nafikiri wanahitaji kupata usaidizi na serikali iajiri maofisa ustawi wa jamii ili kurahisha kazi za walimu za kutoa huduma stahiki kwa watoto hao”, alisema Hoibo.

Aidha, alisema amefurahishwa na namna watoto wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji  maalumu wanavyosaidiana bila ya kujali aina ya ulemavu walionao kitu kinachodhihirisha upendo, kujali na uwajibikaji wa kila mmoja kwa mwenzie.

Kwa mujibu Mkufunzi katika Idara ya Ustawi wa Jamii ya Chuo kikuu Huria cha Tanzania, Fauzia Kitenge tathimini hiyo inahusisha wanafunzi waliopo Tanzania kutoka Norway wanaotoa mrejesho wa shughuli za mafunzo kwa vitendo katika shule tano za Dar es salaam na Arusha.

“Kwa Dar es salaam ni shule za Uhuru Mchanganyiko na Sinza Maalumu wakati kwa Mkoa wa Arusha ni Shule za Msingi na Sekondari za Patandi na Kiloleni”, alisema Bi Fauzia.

Alisema shughuli za mafunzo kwa vitendo zitahusisha makongamano katika shule hizo kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo ulinzi wa watoto, haki za watoto na mengine ambayo yenye msalahi kwa ustawi wa watoto.

Posted in

Leave a comment