
Na Vincent Mpepo, Dar es salaam
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda amewapongeza wakuu wa idara chuoni hapo kwa kufanya kazi kwa bidiii hivyo kuendelea kukifanya chuo hicho kutoa huduma nzuri.
Pongezi hizo alizitoa jana jijini Dar es salaam wakati wa Mhadhara wa Kitaaluma na kusaini makubaliano na kati ya chuo chake na Chuo Kikuu cha Blelefeld cha Ujerumani ambapo miongoni mwa masuala katika makubaliano hayo ni ushirikiano katika tafiti.
Profesa Bisanda alisema wakuu wa idara ndiyo watekelezaji wakuu wa shughuli za kitaaluma chuoni hapo kwa kuwa wana majukumu ya kusimamia mitaala na ufundishaji.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza wakuu wa idara kwa kazi nzuri wanayofanya ambayo inaendelea kukifanya chuo hiki kuendelea na majukumu yake ya msingi”, alisema Profesa Bisanda.
Alisema Ujerumani ni miongoni mwa nchi zilizoendelea katika masuala mengi ikiwemo sayansi na teknolojia hivyo kushirikiana nao kunatoa fursa ya kunufaika katika masuala mbalimbalki ikiwemo ujuzi na maarifa katika tafiti.
Akiwasilisha mada kuhusu namna ya kuratibu timu ya watafiti, Profesa.Dr. Tobias Hecker wa Chuo Kikuu cha Blelefeld cha Ujerumani alisema ni muhimu sana kwa Mtafiti Mkuu kutambua uwezo, sifa na ubunifu kwa kila mtafiti ili atumie talanta hizo katika kufanikisha utafiti.
Alisema jambo jingine muhimu ni kwa mtafiti mkuu ni kujishusha na kuwa kiwango sawa na watafiti wengine kwani kufanya hivyo kutasaidia upatikanaji wa mawazo kutoka kwa watafiti wote bila kujali kiwango cha elimu walichonacho.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Profesa Alex Makulilo alisema makubaliano hayo na vyuo vikuu vya Ujerumani ni ya awamu ya tatu na kwamba mara zote utekelezaji wake umekuwa ni wa uhakika.
“Ni muhimu kubadilishana uzoefu ili kukuza na kuongeza maarifa na ujuzi katika kuratibu timu za utafiti”, alisema Profesa Makulilo.
Naibu Makamu Makamu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anayeshughulikia Huduma za Mikoani naTeknolojia ya Kujifunzia, Profesa Leonard Fweja alishauri wanataaluma kuungana na kufanya tafiti badala ya kufanya mmojammoja.
“Ushirikiano katika utafiti una tija kwa kuwa unasaidia kupunguza gharama na ni rahisi kutumia maarifa, ujuzi na ubunifu wa mwngine katika kuboresha na kupata matokeo mazuri zaidi”, alisema Profesa Fweja.

Leave a comment