Mwalimu Israel Mmari wa KKKT Usharika wa Mji Mpya akihubiri jana katika Ibada katika Mtaa wa Kwembe (Picha na Vincent Mpepo).

Na Vincent Mpepo, Kwembe

Wakristo wametakiwa kuombea akili kwa kuwa ndiyo inayowezesha watu kufanya maamuzi katika masuala mbambali  iwe katika ngazi ya mtu binafsi, ngazi za familia, jamii na taifa kujiepusha na majanga au matokeo ya matumizi mabaya ya akili ambayo mara nyingi huwaingiza watu kwenye majuto na shida.

Wito huo umetolewa leo na Mwalimu Israel Mmari wa Kanisa la Kiinjili la Kiutheri (KKKT) Usharika wa Mji Mpya jijini Dar es salaam wakati akihubiri katika Mtaa Kwembe na kwamba siyo kila matatizo dawa yake ni maombi au kufunga.

Alisema zipo changamoto ambazo kimsingi zimetokana na matumizi mabaya ya akili na kutotambua majira na nyakati hivyo wakati mwingine kuaomba na kufunga ni kujitesa kwa kuwa shida imeanzia kwenye akili iliyofanya maamuzi mabaya.

Alisema kila kitu katika maisha kimefungwa na nyakati na nyakati ni kibebeo cha mafanikio ambayo Mungu huachilia katika mafanikio ya mwanadamu hivyo busara, hekima na akili sahihi husaidia kufanya maamuzi sahihi kwa wakati husika ili kuwa na matokeo chanya.

 “Kuna majira na nyakati kwa ajili ya kujiliwa kwako na hata kama hukufanya maandalizi Mungu huachilia baraka zake sasa inategemea akili yako imetambuaje na kutumia vyema baraka hizo kwa nyakati hizo”, alisema Mwalimu Mmari.

 “Kabla ya mabaya Mungu huwa na tabia ya kutanguiza mema sasa akili na hekima zinaweza kuamua vyema kwa ajili ya baadaye lakini akili isiyoweza kuamua vyema huleta majanga”, alisema Mwalimu Mmari.

Akitolea mifano ya ushoga, usagaji na wanaume wanaoishi na wanawake waliowazidi umri kwa kigezo cha kulelewa kuwa hayo yote ni matumizi mabaya ya akili na kwamba wanaotenda hayo wamefikia mwisho wa namna za kutumia akili zao.

“Hata baadhi ya matatizo katika taasisi za umma, binafsi na kwa watu binafsi wakati mwingine yanatokana na uzembe wa baadhi ya waliopewa dhamana kutotumia akili ipasavyo katika maamuzi fulani”, alisema Mwalimu Mmari.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Exaud Mchome aliwajulisha washarika wa Mtaa huo hatua ya ujenzi wa kanisa ambapo imefikia kwenye kuezeka na kwamba tayari kamati yake imeshalipia mabati kwa ajili ya jengo hilo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Exaud Mchombe akifafanua jambo wakati akizungumza na washarika wa KKKT Mtaa wa Kwembe Jana (Picha na Vincent Mpepo)

Alisema kila mmoja anatakiwa kuwa sehemu ya historia katika ujenzi wa jengo hilo na aone fahari kwa jambo hilo la kumjengea Mungu mahali pa kuabudia. 

Aidha, aliwakumbusha viongozi mbalimbali katika mtaa huo kuendelea kuwa mfano kwa washarika ili kuongoza vyema katika masuala mbalimbali ikiwemo uchangiaji katika ujenzi na kwamba kiongozi mzuri ni yule anayeongoza kwa mfano na matendo yake.

“Kimsingi hakuna masikini anayeweza kukiri kuwa hana cha kumtolea Mungu kwa kuwa wema wake bado ni ushahidi kuwa bado tunapaswa kumrudishia yeye hata kwa kidogo alichotujaalia”, alisema Mchome.

Katika hatua nyingine, wawakilishi wa watoto wa shule ya Jumapili katika ibada hiyo huku masuala mbalimbali yakiwekwa mikononi mwa Mungu ikiwemo amani na usalama wa nchi hususani wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu, waliwaombea viongozi mbalimbalimbali wa dini na wa kisiasa ili waongoze kwa hekma za kimungu.

Wawakilishi wa watoto wa Shule ya Jumapili ambao walifanya maombi kwa niaba ya wenzao jana katika Mtaa wa Kwembe, nyuma yao ni Mwinjilisti Kiongozi wa KKKT Mtaani hapo, Emeline Mzava. (Picha na Vincent Mpepo).

Maombi mengine yalielekezwa kwenye mamlaka mbalimbali zinazohusika na utoaji wa haki ikiwemo mahakama na magereza, ustawi wa familia na mtoto, umoja wa makanisa na Uchumi wa nchi.

Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwakumbusha washarika wa Mtaa huo kuwa mawakili wema katika utoaji wa sadaka ya mfuko wa elimu na kwamba ikiwa kila mmoja atakuwa mwaminifu katika sadaka hiyo itasadia sekta ya elimu.

Kwaya ya akinababa ya KKKT Mtaa wa Kwembe ikihudumu katika ibada ya Jumapili. (Picha na Vincent Mpepo).

Posted in

Leave a comment