
Sehemu ya wanafunzi na walimu kutoka Norway wakifurahia zawadi kutoka Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii zilizotolewa leo katika hafla fupi ya kuwaaga katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania leo jijini Dar es salaam, (Picha na Vincent Mpepo,OUT).
Na Vincent Mpepo, OUT
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimeelezea kuridhishwa kwake na huduma za walimu na wanafunzi kutoka Norway ambao walikuwa nchini katika mafunzo kwa vitendo ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya ushirikiano kati ya chuo hicho na vyuo vikuu kutoka nchini Norway.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Ustawi wa Jamii ya Chuo hicho, Dkt.Mariana Makuu wakati wa hafla fupi ya kuwaaga walimu na wanafunzi iliyofanyika leo katika ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es salaam na kuhudhiriwa na wanataaluma na wanafunzi wa pande zote mbili.
Alisema idara yake imepokea mrejesho chanya kutoka shule ambako wanafunzi na walimu hao walikuwa wanafanya mafunzo kwa vitendo na kwamba wameelezea kuridhishwa na huduma zilizofanyika kwa ajili ya walimu na watoto.
“Walimu wametoa shukrani kwa ujuzi na maarifa mliyoyatoa ya namna ya kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu”, alisema Dkt.Mariana.
Aidha alisema ushirikiano uliooneshwa na wanafunzi na wasimamizi wao umerahisisha kazi ya utekelezaji na tathimini ya kazi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya walimu kutoka Norway, Mwalimu Anne Gutteberg alisema kwa muda aliokaa Tanzania amepata uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo utofatui wa kiutamaduni kati ya Norway na Tanzania.
“Imekuwa fursa nzuri kwa wanafunzi kutoka Norway kujifunza kwa vitendo na kubadilisha uzoefu,” alisema Mwalimu Anne.
Akitoa shukrani kwa niaba ya idara, Mkufunzi Msadizi, Fauzia Kitenge alisema washiriki kutoka Norway wamefanya kazi nzuri kwa juhudi na maarifa kitu ambacho kimeleta matokeo mazuri kupitia kazi zao.

Mkufunzi Msadizi, Idara ya Sosolojia na Ustawi wa Jamii ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Fauzia Kitenge akitoa neno la shukrani kwa wageni kutoka Norway,kushoto ni Mkuu wa Idara hiyo, Dkt.Mariana Makuu. (Picha na Vincent Mpepo).
Naye Mwanafunzi kutoka Norway, Ina Fagerdal aliwashukuru wenyeji wao ambao ni idara ya sosholojia na ustawi wa jamii kwa ukarimu na msaada wao wa karibu katika muda wote waliokuwa hapa nchini.

Mwanafunzi Ina Fagerdal kutoka Norway akielezea uzoefu wake katika mafunzo kwa vitendo alipokwa hapa nchini, (Picha na Vincent Mpepo).
Leave a comment