
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede akihutubia wakati wa uzindizi wa programu tumizi ijulikanayo kama PFZ uliofanyika leo jijini Dar es salaam katika viwanja vya Soko Kuu la Kimataifa la Feri, (Picha na Vincent Mpepo).
Na Vincent Mpepo
Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imezindua programu tumizi ijulikanayo kama PFZ itakayorahisisha shughuli za uvuvi na kuwanufaisha wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa shughuli hizo ikiwemo wavuvi, wafanyabiashara, wachakataji, wachuuzi na wateja hivyo kuongeza tija itakayochochea ukuaji uchumi katika sekta ya uvuvi nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo Feri jijini Dar es salaam leo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede alisema programu tumizi hiyo itasaidia wavuvi kufanya shughuli zao kwa uhakika na kuondokana na uvuvi wa kubahatisha.
“Uvuvi ni moja ya sekta ambayo inakuwa kwa kasi ikizingatiwa kuwa asilimia 75 ya mazao yake yanauzwa kwenye soko la Ulaya na imeendela kutoa mchango mkubwa kwenye lishe na chakula”, alisema Dkt. Mhede.
Alisema baada ya kufanyiwa mjaribio mfumo umeonesha matokeo mazuri ya uhakika wa zaidi ya asilimia 75 kutambua aina ya samaki anaowahitaji kwa mahitaji ya soko, umbali walipo na hali ya hewa ili kuwa na uhakika wa usalama wao wakiwa baharini.
“Mvuvi atajisajili bure na atatakiwa kuweka taarifa zake za msingi ikiwemo taarifa leseni ili atambuliwe na taasisi mbalimbali na kwamba taarifa zake zitalindwa kwa mujibu wa sheria”, alisema Dkt. Mhede.
Alisema programu tumizi hiyo itarahisisha upatikanaji wa taarifa za wavuvi na utambuzi wao utasaidia kudhibiti uvuvi haramu na kutoa fursa kwa taasisi za fedha kuwakopesha wanawake, vijana na wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi.
Alisema mfumo huo umefungamanishwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) hivyo kumhakikishia mvuvi kuwa na taarifa za hali ya hewa kitu kitakachomhakikishia usalama na namna bora ya kujilinda au kuepuka changamoto zitokanazo hali ya hewa hatarishi baharini.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimirei alisema shughuli za utafiti zilianza Mwaka 2011 kupitia Mradi wa kutafuta maeneo ya uvuvi baharini kwa msaada na ushirikiano kutoka Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alisema wavuvi watumie mfumo huo kwa kuwa ni wa serikali na kwamba anawapongeza watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na Maliasili za Bahari (ZAFIRI) kwa kazi hiyo nzuri.
Mkurugenzi wa jiji la Dar es salaam, Helihuruma Mabelya alisema Soko Kuu la Kimataifa la Feri ni moja ya chanzo kikubwa cha mapato kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na kwamba kwa kuthamini mchango huo halmashairi itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa mindombinu ya msingi ili kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wateja.
Leave a comment