Na Tabia Mchakama

Ujumbe wa watu 12 kutoka Eswatini ukiongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Nchi hiyo Madala Mhlanga umezuru ofisi ndogo za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dar es salaam kwa lengo la kupata uzoefu wa masuala mbambali ya kibima ikiwemo usimamizi wa soko na maswala ya kisheria.

Akiongoza kikao hicho kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania, Mkurugenzi wa Usimamizi kutoka TIRA, Christopher Mapunda aliwapitisha wageni hao katika mada mbalimbali ikiwemo hali ya soko la bima nchini, usimamizi wa soko la bima, sheria zinazotumika kusimamia soko la bima, mamlaka ya kamishna kwenye kusimamia soko la bima na mifumo ya tehama.

Aidha mjadala ulijikita kwenye kwenye vipaumbele mbalimbali vya mamlaka vikiwemo utekelezwaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHI) na Uanzishwaji wa konsotia ya bima ya kilimo (TAIC).

Awali Naibu Spika wa Nchi hiyo Madala alieleza kuwa wapo katika mchakato wa uboreshaji wa sheria ya nchini humo na hivyo wamechagua Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazofanya vizuri katika masuala ya bima ili kujifunza.

 “Zaidi tunaishukuru TIRA kwa elimu na uzoefu mliotupatia na tunahaidi kuendeleza ushirikiano kwa siku zijazo”, alisema Naibu Spika Madala.

Baadhi ya wageni hao ni viongozi katika bunge la nchi hiyo, wizara ya fedha na mamlaka ya masuala ya huduma za fedha zisizo za kibenki ambapo waliungana na wataalamu wengine kutoka TIRA ili kubadilishana na kupeana uzoefu wa namna ya usimamizi na udhibiti katika soko la bima kwa pande zote mbili.

Posted in

Leave a comment