
Sehemu ya wadahiliwa wapya waliohudhuria mafunzo elekezi katika Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Mkoa wa Arusha Leo, (Picha na Amos Majaliwa).
Na Vincent Mpepo, Dodoma
Wanafunzi wapya wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania waliodahiliwa katika shahada ya awali ya Mawasiliano ya Umma wameelezea matarajio yao katika muda watakaokuwa masomoni na kuainisha sababu za kukichagua chuo hicho.
Wakizungumza katika nyakati tofauti kupitia mahojiano ya kimtandao hawakusita kuelezea hisia zao.
Upendo Sumary wa kituo cha chuo hicho Mkoa wa Ruvuma ambaye ni mdahiliwa wa shahada ya mawasiliano ya umma alisema aliamua kusoma katika chuo hicho kwa kuwa ni chuo cha umma kinachotambulika kitaifa na kimataifa na kwamba anaamini kupitia chuo hicho atafikia ndoto zake.
“Nimependa kusoma OUT kwa kuwa ni chuo chenye sifa nzuri ya ufundishaji na ninaamini kufanikisha ndoto zangu”, alisema Upendo.
Alisema anategemea kufanya vyema katika masomo yake kwani atajitahidi kufuatilia masomo kwa kadiri ya uwezo wake na atakuwa makini ili afanikishe malengo yake.
Esther Nurben wa Dar es salaam ambaye ni mdahiliwa wa shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa umma alisema alifikia uamuzi wa kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutokana na sifa za kuaminika kwa kutoa wahitimu mahiri kwenye kwenye fani mbalimbali siyo tasnia ya habari pekee.
“Ni mategemeo yangu kuwa nitahitimu shahada yangu kwa muda muafaka bila ya changamoto zozote”, alisema Ester.
Alisema sababu nyingine muhimu ambayo ilimvutia kusoma chuo hicho ni fursa ya kuendelea na masomo huku anafanya kazi na unafuu wa ada.
Anjela Mhilu wa Kituo cha Mkoa cha Ilala alisema aliamua kusoma katika chuo hicho ili kujiongezea maarifa na ujuzi kwenye programu aliyoomba na ni katika harakati za kujiongeza na kutafuta zaidi.
Kwa upande wake, Abishagi Mpoki alisema uwezekano wa kufanyia mitihani mahali popote atakapokuwa hata akiwa na majukumu ya kikazi nje ya kituo chake cha kazi ndiyo sababu iliyomvutia kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
“Elimu bora na kuniwezesha kusoma huku nafanya kazi ni kitu kilichonifanya nikichague chuo hiki”, alisema Abishagi.
Mwandishi amebaini kuwa taarifa za matangazo ya chuo hicho zinaufikia umma kupitia matangazo kwa njia za mitandao ya kijamii, wanafunzi wanaoendelea na masomo na kupitia wahitimu wa chuo hicho ambao ni wafanyakazi katika taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Ni ukweli usiopingika kuwa chuo hicho kina deni na wajibu wa kutimiza ili kuendana na matarajio ya wadahiliwa hao kwa kuboresha huduma zake ikiwemo huduma ya mtanado ambayo ndiyo uti wa mgongo wa elimu masafa, uboreshaji wa mifumo ya Tehama na huduma kwa wateja.

Leave a comment