Na Vincent Mpepo, Dodoma

Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wametakiwa kuendelea kumtolea Mungu sadaka bila kukata tamaa huku wakiziombea ili zifanye kazi yake na pia wapate baraka kupitia sadaka hizo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Ujenzi wa Madarasa ya Watoto na Ofisi za Usharika  wa Betheli Dayosisi ya Dodoma, Makao Makuu Lilian Uroki wakati akihamasisha utoaji wa sadaka hiyo katika ibada ya kwanza usharikani hapo Jumapili.

Alisema washarika wenyeji na wageni wanapaswa kufanyia kazi suala hilo na kwamba hawapaswi kuiita michango bali ni sadaka.

“Ni muhimu sana kuhakikisha kabla ya kutoa unaziombea ili Mungu afanye kitu kwa ajili yako”, alisema Lilian

Mhubiri wa Siku hiyo, ambaye ni Katibu wa Usharika huo, Dkt.Denis Ringo aliwaasa wakristo kutokujisahau kwa kuwanyenyekea watumishi badala ya Mungu aliyewatuma na kwamba wanatumika ili kusudi la Mungu litimie.

“Ni hatari kumwamini aliueagizwa badala ya aliyemuagiza”, alisema Dkt.Ringo

Alisema kuna wakati wakristo hujisahau hususani wanapopata kitu iwe ni baraka ya kichumi, kupanda cheo au manufaa fulani badala ya kumtumikia Mungu hurudi nyuma kwa sababu mbalimbali ikwemo madai ya kukosa muda wa kufanya zake na matokeo yake huwa ni kusahaulika.

“Ni mara ngapi tunatumika kwa Bwana kwa nafasi zetu, vyeo vetu au hali njema tulizonazo?” Aliuliza Dkt.Ringo

Alisema Mungu hutumia watu au vitu vya kawaida au vinyonge ili kusudi lake litimie badala ya watu wenye mamlaka au umaarufu ambao wakati mwingine hutumia nafasi zao ili tu wapate sifa na kusahau kuwa Mungu ndiye aliyewapa nafasi hizo.

Alisema mkristo anapoitwa kutumika na ikiwa atatumika sawasawa na kusudi la Mungu atainuliwa na kuheshimishwa.

Alisema wakristo wanapopitia katika nyakati ngumu busara, hekima, unyenyekevu na upole vitaendelea kuwa ndiyo silaha nzuri na kwamba Mungu anajua kesho yao hivyo waendelee kumtegemea yeye na wasiondoke katika kusudi la Mungu.

Mchungaji kiongozi wa Usharika huo, Gershon Ngewe aliwashukuru washarika kwa sadaka mbalimbali ambazo wanaendelea kuzitoa na kuwaombea kwa Mungu ili afanyike Baraka kupitia sadaka hizo.

Posted in

Leave a comment