Na Vincent Mpepo

Watu wenye mahitaji maalumu ni kundi la watu ambao hawawezi kujipatia mahitaji yao ya msingi wao wenyewe kutokana na changamoto kadha wa kadha.

Changamoto hizo husababishwa na vitu mbalimbali kama vile ulemavu wa kimwili, kihisia, kitabia, au kujifunza au kuharibika ambazo husababisha mtu kuhitaji huduma za ziada au maalum au malazi kama vile elimu au burudani.

Ili kundi hili lipate mahitaji huduma za msingi kama walivyo binadamu wengine ni lazima jamii ihusike kwa namna moja au nyingine ili kuhakikisha kuwa jukumu hili linatekelezwa.

Utekekezaji wake huhusisha serikali, jamii, makundi mbalimbali, taasisi za dini, mashirika na taasisi za umma na binafsi.

Ushirikiano wa taasisi mbalimbali unasaidia kuwa na nguvu ya pamoja ili kuhakikisha kundi hili muhimu linapata stahiki na haki za kibinadamu ili kuwa na jamii yenye ustawi bora, isiyo na wanaoachwa au kutengwa kwa namna yoyote.

Ushirikiano huu unawaleta pamoja wadau mbalimbali kwa namna ya uwezo na aina ya huduma wanazotoa ili kwa pamoja kuwa na uwezeshaji wa hali na mali katika ngazi mbalimbali. Kwa mfano taasisi za elimu kama Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kina idara maalumu inayohusika na watu wenye mahitaji maalumu.

Sanjali na kitengo hicho, idara ya sosholojia na ustawi wa jamii nayo imekuwa ikifanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna bora za kusaidia watu wenye mahitaji maalumu.

Idara hiyo, imekuwa na makubaliano na taasisi za ndani na nje ya nchi ili kupata msaada wa kitaaluma wa namna ya kuongeza wigo wa maarifa kuhusu elimu ya watu wenye mahitaji Maalumu ikigusa eneo la ualimu wa elimu Maalumu na ufundishaji.

Idara hiyo kupitia ushirikiano na vyuo vikuu vya nje ikiwemo Norway kupitia Mradi wa Norec ambao umesaidia masuala mbalimbali ikiwemo programu za kubadilishana uzoefu zinazowahuhisha wahadhiri, wanafunzi, maofisa maendeleo ya jamii na wadau mbalimbali wa maswala ya ustawi wa jamii.

Kwa mujibu wa Daktari Mariana Makuu, mtoto mwenye mahitaji maalum awapo shuleni anatakiwa kulelewa vyema ili apate huduma tatu muhimu ikiwemo elimu, afya na msaada wa kisaikolojia na kijamii.

“Kundi la watoto wenye mahitaji maalumu linakabiliwa na ukatili wa aina mbalimbali unaosababisha watoto hawa kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia”, anasema Dkt.Mariana.

Uwepo wa wataaam wa ustawi wa jamii shuleni wenye jukumu la kuangalia masuala ya kijamii kwa watoto hawa wakisaidiana na walimu utasidia kuibua na kuzuia ukatili na matatizo mengine yanayowakabili watoto hususani wenye ulemavu.

“Serikali ione umuhimu wa kuaajiri wataalam hawa ili kuendana na mabadiliko ya jamii kwa sasa,” anasema Dkt. Makuu.

Wakati huohuo, ushirikiano wa serikali na taasisi za dini nao una nafasi nzuri kuhaikisha jamii na husani ya wenye mahitaji maalumu wanajaliwa ili kuwa na jamii inayojali watu wote bila kujali ulemavu wa aina yoyote.

Hivi karibuni tumeshuhudia mazungumzo kati ya kiongozi mkuu wa nchi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ulioongozwa na Mkuu kanisa na Mkuu wa Dayosisi hiyo Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa Ikulu jijini, Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Samia pamoja na viongozi hao walijadili kuhusu utoaji wa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum hususan wenye changamoto ya afya ya akili.

Viongozi kanisa wameipongeza na kuishukuru serikali kwa ushirikiano inaotoa kwa kanisa kwani serikali imeahidi kushirikiana na kanisa ili kujenga Kituo kikubwa zaidi kitakachohudumia watoto wenye changamoto ya afya ya akili ili watoto wengi waweze kupata huduma hiyo.

Wakati serikali, taasisi za umma na binafsi za ndani na nje zikifanya kila linalowezekana kusaidia kundi la watu wenye mahitaji Maalumu swali ni kwa jamii tunafanya nini kuunga mkono kwa sehemu yetu?

Ni dhahiri kuwa bado elimu inahitajika ili masuala ya watu wenye mahitaji Maalumu yapate wigo mpana wa kuelezwa kwa umma kupitia majukwaa mbalimbali ya vyombo vya habari, mikutano mbalimbali na kila ambapo fursa ya kufanya hivyo itajitokeza.

Posted in

Leave a comment