Wanafunzi wakiuliza na kujibu maswali mbalimbali katika mafunzo yaliyotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.

Na Okello Thomas

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetembelea wanafunzi na walimu wa shule mbalimbali za sekondari wilayani Mafia na kutoa elimu kuhusu vinasaba katika jinai ikiwemo upatikanaji wa haki kwenye matendo ya ubakaji, ulawiti pamoja na kuzifahamu kemikali na madhara yake.

Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa alisema  madhumuni ya elimu ya vinasaba na kemikali kwa wanafunzi ni kuhamasisha wapende masomo ya sayansi na kuwa mabalozi katika kuelimisha jamii inayowazunguka kuhusu vinasaba na kemikali.

Meneja wa Mamlaka, Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa (aliyesimama) akielezea majukumu mbalimbali ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Kirongwe Aprili 9, 2025

“Kupitia elimu ya vinasaba, tunaamini wanafunzi wamepata uelewa juu ya nini cha kufanya ikitokea mwanafunzi mwenzao amekumbwa na tatizo la ubakaji au ulawiti pamoja na kutatua changamoto za ajali za kemikali,” alisema Mkapa.

Afisa Elimu Maalumu Sekondari Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Musa Abdallah ameishukuru Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwafikia wanafunzi ambao ndio walengwa wa masuala mbalimbali katika jamii lakini pia kuwa viongozi na wanasayansi wa baadae.

Naye mwalimu wa masomo ya sayansi katika shule ya sekondari Baleni, Eddy Mjige amesema ujio wa wataalam kutoka GCLA utakuwa na manufaa makubwa kwa walimu wa masomo ya sayansi hususani uendeshaji wa maabara na matumizi sahihi ya kemikali kwenye wakati wa elimu kwa vitendo.

Sambamba na hayo, mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Kilindoni, Yahya Hafidhi ameiomba Mamlaka kuendelea na utoaji wa elimu kuhusu majukumu yao na mbinu za kuwawezesha wanafunzi kutoa elimu kwa jamii inaowazunguka.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalifanyika kuanzia Aprili 9 hadi 10, 2025 kupitia Ofisi ya Kanda ya Mashariki.

Mtumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Emmanuel Jacob, akitoa elimu kuhusu masuala ya alama na madhara ya kemikali kwa wanafunzi wa shule ya Sekondari Kidawendui Aprili 10, 2025

Posted in

Leave a comment