
Na Farida Mkumba, Dodoma
Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo) kinatarajia kudahili wanafunzi 9,300 katika ngazi za stashahada, stashahada na ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa ameeleza hayo jana Aprili 16 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/2026.
Alisema chuo hicho ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kimepanga kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 7.77 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mengineyo.
“Shughuli zilizopangwa kutekelezwa na chuo hiki ni kudahili wanafunzi 9300 na kuanza kutoa mafunzo ya shahada ya kwanza ya nyaraka na kumbukumbu kwa kudahili wanafunzi 100 baada ya mtaala kukamilika” Alisema Mchengerwa.
Alisema chuo kitazijengea uwezo mamlaka za serikali za mitaa 40 na taasisi tano kupitia mafunzo ya muda mfupi ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema shunguli nyingine zitakazofanywa na chuo hicho kwa kipindi hicho ni kufanya tafiti 6 na machapisho 30 ya kitaaluma katika majarida mbalimbali yenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika mamlaka za serikali za mitaa na wadau wengine.
“Eneo lingine litakaloangaziwa ni ukarabati wa mabweni, nyumba za watumishi na miundombinu ya maji”, alisema Mh.Mhengerwa.
Alisema kiasi cha shilingi milioni 575 kitatumika kufanya ukarabati wa mabweni manne ya wanafunzi, nyumba saba za watumishi ikiwa ni pamoja na miundombinu ya maji na umeme.
Aidha, kuhusu kuwaendeleza watumishi wa chuo waziri Mchengerwa alisema kwa mwaka 2025/26 watumishi 27 wataendelezwa kielimu katika ngazi mbalimbali ambapo watano ni shahada, 11 Uzamili na Shahada ya Uzamivu 11.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI, Mh. Justine Nyamoga alisema kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 Chuo cha Serikali za Mitaa kilikadiriwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 10.5.
Aidha, aliipongeza serikali kwa utekelezaji wa ushauri, maoni na mpendekezo 13 yaliyotolewa na kamati yake.
“Kwa maeneo ambayo hayajatekelezwa kikamilifu, kamati inasisitiza yaendelee kufanyiwa kazi ikiwemo suala la shule za mchepuo wa Kiingereza”, alisema Mh. Nyamoga.
Leave a comment